Tanzania kurejesha hadhi ya reli ya Tazara
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akikata keki pamoja na viongozi mbalimbali kwenye hafla ya chakula cha jioni ya kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya Tazara iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Maboresho yake yanalenga kuiwezesha reli hiyo kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye, sambamba na kuongeza mchango wake katika maendeleo.
Dar es Salaam. Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha miundombinu ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ili irejee kuwa mhimili muhimu wa uchumi, biashara na ujumuishaji wa kikanda, wakati reli hiyo ikiadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Ahadi hiyo ilitolewa jana Jumanne, Julai 14, 2026, na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, katika hafla ya chakula cha jioni ya kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya Tazara iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema maboresho yanayofanywa yanalenga kuiwezesha reli hiyo kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye, huku ikiongeza mchango wake katika maendeleo ya Tanzania, Zambia na nchi za Kusini mwa Afrika.
Profesa Mbarawa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha reli hiyo inarejeshewa hadhi yake kama moja ya njia muhimu za usafirishaji barani Afrika.
“Ushirikiano wa kimkakati kati ya Tazara na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) umefungua ukurasa mpya wa maendeleo ya reli hiyo.
Kwa kuwa ushirikiano huo hauhusishi ukarabati wa miundombinu pekee, bali pia unalenga kuongeza ushindani wa biashara, kuimarisha ujumuishaji wa kikanda, kuchochea maendeleo ya viwanda na kuboresha ustawi wa wananchi wa mataifa yanayonufaika na reli hiyo,” amesema.
Waziri huyo amefafanua kuwa ununuzi wa injini na mabehewa mapya, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uendeshaji wa huduma, vitasaidia kurejesha Tazara miongoni mwa reli bora barani Afrika na kuendelea kuwa kiungo muhimu kinachounganisha Bandari ya Dar es Salaam na Zambia pamoja na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika, hivyo kuchochea biashara na usafirishaji wa mizigo kwa ufanisi zaidi.
Akizungumzia maadhimisho ya miaka 50 ya reli hiyo, Profesa Mbarawa amesema tukio hilo halikuwa sherehe ya reli pekee, bali ni kumbukizi ya moja ya mafanikio makubwa ya maendeleo katika historia ya Afrika yaliyotokana na maono ya viongozi waasisi, mshikamano wa kimataifa na urafiki wa kudumu kati ya Tanzania, Zambia na China.
Amewataja Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Zambia, Hayati Dk Kenneth Kaunda, na aliyekuwa Mwenyekiti wa China, hayati Mao Zedong, kuwa viongozi walioweka msingi wa mradi huo wakati wengi walipouona kuwa hauwezekani, na maono yao yaliwezesha kujengwa kwa moja ya miradi mikubwa ya ushirikiano kati ya Afrika na China.
“Tazara haikujengwa kwa lengo la kuunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Kapiri Mposhi nchini Zambia pekee, bali ilikuwa ishara ya matumaini, uhuru na heshima kwa mataifa ya Afrika, kwa kuwa hata baada ya miaka 50, reli hiyo imeendelea kuunganisha watu, tamaduni, biashara na uchumi wa mataifa hayo, huku ikichangia ukuaji wa viwanda, biashara ya kikanda, ajira na masoko kwa wakulima na wafanyabiashara,” amesema Profesa Mbarawa.
Amesema jukumu la sasa ni kuiandaa Tazara kukidhi mahitaji ya miaka 50 ijayo kwa kuwekeza katika mifumo ya kisasa, salama na yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara ili kuendana na mahitaji ya uchumi wa kisasa.
Kwa upande wake, Naibu Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Anthony Bwalya, amesema Tazara ilikuwa njia muhimu ya kuifikia Bandari ya Dar es Salaam wakati wa harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na ilichangia kuimarisha uhuru wa kiuchumi wa Zambia.
Pia, ameishukuru Tanzania kwa kutoa ardhi na kubeba sehemu ya gharama za ujenzi, huku akiipongeza China kwa mchango wake wa fedha, utaalamu na nguvu kazi uliofanikisha ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa karibu kilomita 2,000.
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema China itaendelea kushirikiana na Tanzania na Zambia katika kuboresha miundombinu ya usafiri, kukuza biashara na kuhamasisha uwekezaji katika sekta za viwanda na kilimo.
Amesisitiza kuwa kuendeleza Tazara ni njia ya kuheshimu mchango wa wahandisi na wataalamu waliohusika katika ujenzi wa reli hiyo na kuimarisha urafiki wa China na Afrika.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tazara, Bruno Chinga'andu, amewapongeza wafanyakazi wa sasa na waliostaafu kwa kuendelea kuilinda reli hiyo licha ya changamoto zilizokuwapo.
Amesema kupitia ushirikiano kati ya Tazara na CCECC, wana matumaini ya kurejesha huduma bora, salama na zenye ufanisi zaidi, huku akiahidi kuwa miaka 50 ijayo itaongozwa na huduma zenye ubora na zinazokidhi mahitaji ya wateja.