Tanzania kushiriki tuzo za Oscar kwa mara ya kwanza

Muktasari:

  • Tanzania mwaka huu 2022 itakuwa miongoni mwa nchi zitakazoshiriki tuzo maarufu za filamu duniani za Oscar.

T:



S.



Nasra Abdallah Mwananchi


Dar es Salaam. Tanzania mwaka huu itakuwa miongoni mwa nchi zitakazoshiriki tuzo maarufu za filamu duniani za Oscar.

Katika tuzo hizo, imepewa nafasi ya kushiriki katika kipengele cha filamu za nje ya Marekani (Foreign Film).

Hii ni baada ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kukubaliwa kamati yake iliyoiunda ya kuchuja filamu itakayoshindanishwa katika tuzo hizo ambapo itahusisha filamu zilizotaka Januari 1, 2022 hadi Novemba 30, 2022.

Akizungumza leo Jumatatu Julai 25, 2022, Katibu Mtendaji wa bodi ya filamu, Dk Kiagho Kilonzo amesema mchakato wa kupendekeza kamati hiyo ulianza tangu mwaka 2019 na hatimaye imekubaliwa mwaka huu.

Dk Kilonzo amewataja wajumbe wanaounda kamati hiyo ambao wapo kumi ni pamoja na Dk Mona Mwakalinga ambaye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Wengine ni Simon Peter (Katibu), Profesa Martin Mhando, Single Mtambalike 'Rich Rich', Binay Gokan, Zamaradi Nzowa, Adam Juma, Daniel Menege, Florence Mkinga na Vyonne Cherie'Monalisa'.

"Kamati hiyo ina majukumu ya kupokea na kuchuja filamu zitakazowasilishwa kwa waendesha tuzo hizo za oscar nchini Marekani," amefafanua Dk Kilonzo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Mona Mwakalinga amesema vigezo vya kushiriki kwenye tuzo ni pamoja na filamu iwe imetayarishwa nje ya Marekani.

"Kigezo kingine iwe imeonyoshwa kwenye kumbi za sinema za biashara angalau siku saba mfululizo iwe na urefu kuanzia dakika 40 na iwe imetumia lugha mbali na kingereza kwa zaidi ya asilimia 50 na tafsiri sahihi za kingereza.

"Pia iwe katika muundo wa Digital Cinema Package(DCP) kwa ubora angalau 2040 kwa 1080 pxels(2k),iwe na sauti ya kipimo cha 5.1 au 7.1 au iwe yenye chanel 3 za sauti(left,right and centre)," amesema Dk Mona.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo amesema filamu ambazo zilisambazwa au kufanyiwa maonyesho nje ya kumbi za sinema hazitakidhi vigezo kwenye tuzo hizo.

Maonyesho hayo ni pamoja na cable televisheni, DVD, isiwe ineonyeshwa kwenye ndege na kwenye mtandao wa Internet.

Kamati hiyo inatarajia kupokea filamu hizo kuanzia Agosti 1 hadi Agosti 30, 2022 kupitia mtandao wa [email protected].

Wakitoa maoni yao kuhusiana na jambo hilo akiwemo msanii Rose Ndauka amesema ni hatua nzuri kwa tasnia ya filamu na kueleza kuwa inaenda kuwaamsha maprodyuza kutengeneza kazi nzuri kwani wengi wao walikuwa wakizitengeneza ilimradi tu.

Wakati msanii Jacob Steven'JB', amesema ni kitu kizuri ila swali lipo kwa je watengeneza filamu wapo tayari licha ya bodi ya filamu kuwa na maono makubwa ya kuisongesha tasnia hiyo kimataifa.