Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yaandika historia mpya matumizi ya nishati safi

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi akizungumza katika uzinduzi miundombinu ya kuchaji magari ya umeme pamoja na mpango wa ufadhili wa majiko ya umeme wakati wa hafla iliyofanyika leo Alhamis Juni 11, 2026 jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Uzinduzi wa EV charging na majiko ya umeme waleta matumaini mapya katika kipindi ambacho dunia ikikabiliwa na changamoto ya kupanda kwa gharama za mafuta, hali inayofanya umeme kuwa mbadala salama na wa kiuchumi zaidi.

Dar es Salaam. Katika kile kinachoonekana kama hatua kubwa ya mageuzi ya sekta ya nishati nchini, Tanzania imezindua rasmi miundombinu ya kuchaji magari ya umeme pamoja na mpango wa ufadhili wa majiko ya umeme, hatua inayolenga kuharakisha matumizi ya nishati safi katika usafiri na upishi.

Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma umebeba ushirikiano wa Serikali, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ukielezwa kuwa mwanzo wa mapinduzi ya kiuchumi na kimazingira nchini.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania sasa inaingia katika hatua mpya ya matumizi ya teknolojia ya umeme kwenye vyombo vya usafiri na majiko ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taifa wa nishati safi.

Amesema mradi huo unaonyesha wazi kuwa nchi imeanza kupiga hatua kubwa katika matumizi ya magari ya umeme, bajaji na pikipiki, hatua inayoiweka Tanzania kwenye ramani ya mabadiliko ya nishati duniani.

“Huu ni mwanzo mzuri sana. Ni jambo la ubunifu linaloonyesha kwamba Tanzania sasa tumesogea mbele katika matumizi ya magari ya umeme, bajaji na bodaboda za umeme,” amesema Ndejembi.

Ameongeza kuwa mabadiliko hayo yanakuja wakati dunia ikikabiliwa na changamoto ya kupanda kwa gharama za mafuta, hali inayofanya umeme kuwa mbadala salama na wa kiuchumi zaidi.

“Ukiangalia changamoto za mafuta duniani na gharama zake, kutumia umeme wa Sh30,000 na ukasafiri kilomita 600 ni fursa kubwa sana kwa wananchi,” amesema.

Waziri Ndejembi amesema moja ya malengo makubwa ya mageuzi hayo ni kupunguza utegemezi wa mafuta na kuongeza matumizi ya umeme kwenye usafiri na kupikia, hatua itakayosaidia kuokoa fedha za kigeni.

Amesema kupungua kwa uagizaji wa mafuta kutaiwezesha nchi kubaki na akiba ya dola kwa ajili ya matumizi mengine ya kiuchumi.

“Sasa kwa mageuzi haya tunapunguza utegemezi wa mafuta na kuimarisha uchumi wetu kwa kubaki na fedha za kigeni ndani ya nchi,” amesema.

Amesisitiza kuwa Serikali na taasisi zake zinapaswa kuwa mfano wa kuigwa, akizitaka Wizara ya Nishati, Tanesco na taasisi nyingine kuanza kutumia magari ya umeme au hybrid kama sehemu ya kuhamasisha wananchi.

Amesema pia Tanzania inaweza kufikia angalau asilimia 20 ya vyombo vya moto vinavyoingia nchini vikiwa vya umeme au hybrid kama hatua ya mwanzo kuelekea uchumi wa kijani.

Amefafanua kuwa licha ya gharama ya awali ya magari ya umeme kuwa kubwa, gharama ya uendeshaji wake ni nafuu zaidi, akitoa mfano kuwa gari la umeme linaweza kusafiri hadi kilomita 400 kwa takribani Sh27,000, tofauti na zaidi ya Sh300,000 zinazotumika kwa gari la mafuta kwa safari ya Dar es Salaam kwenda Dodoma.


Vituo 50 vya kuchaji nchi nzima

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, amesema shirika hilo limeanza utekelezaji wa mradi wa kujenga vituo 50 vya kuchaji magari ya umeme nchini, ambavyo vitatoa huduma za kuchaji za kawaida na za haraka.

Amesema vituo hivyo vitakuwa na mifumo miwili; ya kuchaji kwa muda mrefu unaofikia saa nane hadi 10 na ya haraka itakayowezesha gari kuchaji ndani ya dakika 15 hadi saa moja.

“Kwa sababu ndiyo tumeanza, tuna vituo 50 tunajenga kwenye mpango huu. Tutahakikisha pia kuna chaja za haraka ili kukidhi mahitaji ya watumiaji,” amesema Twange.

Amesema kituo kilichozinduliwa Dodoma kitakuwa cha mfano na kitatoa huduma ya bure kwa muda wa mwezi mmoja kwa watumiaji wa magari, bajaji na pikipiki za umeme, hatua inayolenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia hiyo mpya.


Majiko ya umeme kwa mfumo wa mkopo

Katika hatua nyingine Tanesco imeingia makubaliano itakayowezesha utekelezaji wa mpango wa ukopeshaji wa majiko ya umeme kupitia mfumo wa on-bill financing, ambapo wananchi watapata majiko na kulipa kidogo kidogo kupitia matumizi ya umeme.

Waziri Ndejembi amesema mpango huo utaondoa kikwazo cha gharama za awali na kuhakikisha huduma hiyo inafika hadi vijijini kupitia ushirikiano wa Tanesco na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Amesema majiko hayo yanatumia kiwango kidogo cha umeme, ambapo baadhi ya kaya hutumia chini ya uniti moja kupika chakula, hali inayopunguza gharama kwa watumiaji.

“Tunataka huduma hii ifike vijijini Rukwa, Ngara, Simiyu na maeneo yote nchini,” amesema.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi wakati uzinduzi miundombinu ya kuchaji magari ya umeme pamoja na mpango wa ufadhili wa majiko ya umeme wakati wa hafla iliyofanyika leo Alhamis Juni 11, 2026 jijini Dodoma.


Wadau waomba punguzo la kodi

Kwa upande wa wadau wa sekta ya nishati safi ya kupikia wameiomba Serikali kupunguza kodi kwenye majiko ya umeme, wakieleza kuwa zaidi ya asilimia 32 ya gharama za bidhaa hizo zinatokana na kodi mbalimbali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Positive Cooker, Atukuzwe Wilson, amesema punguzo hilo litasaidia kupunguza bei kwa mlaji wa mwisho na kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi nchini.

“Tunaiomba Serikali iangalie kodi kwenye bidhaa hizi. Tukipata nafuu ya kodi, hata wananchi wa kipato cha chini wataweza kumudu majiko haya,” amesema Wilson.

Amesema ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali umeanza kuonyesha matokeo chanya, akibainisha kuwa lengo la Taifa la kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034, linawezekana endapo mazingira yataendelea kuboreshwa.


UNDP yaipongeza Tanzania

Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limeipongeza Tanzania kwa hatua hiyo, likisema uwekezaji katika miundombinu ya kuchaji na majiko ya umeme ni uthibitisho wa uwezo wa ushirikiano kubadilisha sera kuwa suluhisho la moja kwa moja kwa wananchi.

Mwakilishi wa UNDP, Shigeki Komatsubara amesema mpango wa ufadhili wa majiko ya umeme unasaidia kupunguza changamoto ya gharama za awali ambazo zimekuwa kikwazo kwa kaya nyingi kuhamia kwenye nishati safi.

“Uhamaji wa umeme, kupikia kwa nishati safi na huduma za kidijitali si tena hiari bali ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi,” amesema Komatsubara.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za maisha, kuimarisha usalama wa nishati na kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje.