Tarime watangaza mkakati kudhibiti utoroshaji madini
Baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa dhahabu mkoani Mara wakiwa kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na tume ya madini mkoa wa Mara kwaajili ya kutoa elimu juu ya sheria na taratibu za ufanyaji biashara ya madini. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
Tume ya Madini mkoani Mara imesema kuanzia sasa hakuna mfanyabiashara wa madini mkoani humo atakayepewa leseni ya kuuza madini endapo atakua hana chumba cha biashara kwenye masoko manne ya madini yaliyopo mkoani Mara.
Musoma. Tume ya Madini mkoani Mara imesema kuanzia sasa hakuna mfanyabiashara wa madini mkoani humo atakayepewa leseni ya kuuza madini endapo atakua hana chumba cha biashara kwenye masoko manne ya madini yaliyopo mkoani Mara.
Hatua hiyo imechukuliwa na tume hiyo ikiwa ni njia mojwapo ya kupambana na utoroshaji wa madini ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu mkoani humo.
Akizungumza kwenye mafunzo yaliyoandaliwa kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa madini mkoni hapa, Ofisa Madini mkazi wa mkoa wa Mara, Joseph Kumburu amesema kuwa hivi karibuni kuliibuka tabia ya utoroshaji wa madini ambao ulikuwa ukisababishwa na sababu mbalimbali ikiwepo uelewa mdogo kuhusu sheria zinazoongoza biashara ya madini.
"Tumefanya operesheni hivi karibuni na tulikamata watu wengi wakihusishwa na utoroshaji wa madini hatua kadhaa zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kulipa faini sasa tumeona tutoe elimu kwa wafanyabiashara wote ili wajue nini wanatakiwa kufanya baada ya hapo atakayekwenda kinyume atachukuliwa hatua kali" amesema Kumburu bila kutoa takwimu za watu waliokamatwa kwa tuhuma hizo.
Amewataka wafanyabiashara hao kuhakikisha kuwa wanakuwa na vyumba vya biashara kwenye masoko ya madini yaliyopo wilayani Tarime, Musoma na Bunda ili kufanya biashara halali kwa mujibu wa sheria na maelekezo. Mkoa wa Mara unao jumla ya wafanyabiashara wakubwa wa madini 23 na wadogo 104.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo katibu wa soko kuu la dhahabu mkoa wa Mara, Jackson Ngasa amesema kuwa mafunzo hayo yamekuja muda muafaka kutokana na changamoto kadhaa zilizokuwa zinajitikeza kwenye masoko ya dhahabu mkoani Mara.
Amesema kuwa kufuatia operesheni iliyofanywa na tume ya madini kwa kushirikiana na vyombo vya dola mkoani Mara hivi karibuni, wafanyabiashara wengi walisitisha kuleta madini sokoni hapo kwa kuogopa kukamatwa.
"Wenye vibanda sokoni walikuwa wameazimia kufunga vibanda vyao kwasababu hakukuwa na madini kabisa hivyo walikuwa wanapata hasara kwahiyo haya mafunzo yatarejesha hali ya biashara kama ilivyokuwa awali" amesema.