TBS sasa kuanza kuweka vinasaba kwenye mafuta

Tuesday May 04 2021
tbs pc

Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo

By Alfred Zacharia

Dar es Salaam. Ili kudhibiti ubora, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeanza kuweka vinasaba kwenye mafuta yanayoingizwa nchini.

Uhakiki wa vinasaba kwenye mafuta ni kitambulisho cha pekee (alama) kwa kufuata idadi ya bidhaa za petroli kwenye bohari kabla ya kusambazwa sokoni.

Alama hiyo inatumika kuhakiki ubora wa bidhaa na kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa bandia na kudhibiti ukwepaji kodi.

Bila kutaja tarehe, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo amesema TBS imeanza kuweka vinasaba mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Katikati ya mwezi uliopita, wakati wa mjadala wa hotuba ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu bungeni, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani aliliambia Bunge kuwa Serikali imesitisha mkataba na kampuni iliyokuwa ikifanya shughuli hiyo. Hata hivyo, hakumtaja aliyepewa jukumu la kuweka vinasaba baada ya kuvunja mkataba uliokuwapo.

Jana, Profesa Mkumbo aliwaambia waandishi wa habari alipotembelea makao makuu ya TBS jijini hapa kwamba shughuli hiyo sasa ipo chini ya shirika hilo.

Advertisement

“TBS ni mhakiki rasmi wa vinasaba kwenye mafuta na tayari ameanza katika mikoa mitatu. Nina imani atafanya kazi kwa ufanisi kwa faida ya nchi na watu wake. Tunaweza kukosa wafanyakazi wa kutosha wakati huu lakini nimewaruhusu kuajiri watu wenye ujuzi na kuendelea kutoa mafunzo kwa watu wa ndani ili kuziba pengo hilo,” alibainisha.

Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby alilieleza Bunge kwamba Watanzania walikuwa wakilipa kwa kuweka vinasaba kwenye mafuta hivyo Serikali inahitaji kuchunguza m wenendo wa sekta hiyo ndogo ya mafuta.

Advertisement