Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TCB yaahidi kuimarisha ushindani wa kahawa ya Tanzania kimataifa

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Profesa Kamuzora amesema uwekezaji unaofanywa na wadau katika uzalishaji, uchakataji, biashara na utoaji wa huduma mbalimbali umeendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya sekta hiyo.

Dodoma. Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya kahawa nchini ili kuhakikisha tasnia hiyo inazidi kukua na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa huku ikiongeza ushindani wa kahawa ya Tanzania katika soko la dunia.

Akizungumza leo Alhamisi Juni 4, 2026 jijini Dodoma kwenye mkutano wa 16 wa wadau wa tasnia ya kahawa, Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Profesa Aurelia Kamuzora amesema uwekezaji unaofanywa na wadau katika uzalishaji, uchakataji, biashara na utoaji wa huduma mbalimbali umeendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya sekta hiyo.

Amesema TCB itaendelea kutoa ushirikiano na msaada unaohitajika kwa wadau ili kuhakikisha tasnia ya kahawa inaendelea kuwanufaisha wakulima, wafanyabiashara na taifa kwa ujumla.

“Kwa niaba ya Bodi ya Kahawa Tanzania, napenda kuwahakikishia kuwa tutaendelea kushirikiana nanyi na kutoa usaidizi unaohitajika ili kuhakikisha tasnia ya kahawa inaendelea kukua na kuleta mafanikio makubwa zaidi kwa wakulima, wafanyabiashara na taifa kwa ujumla,” amesema Profesa Kamuzora.

Amesema mafanikio yanayoshuhudiwa katika sekta hiyo yanatokana na uwekezaji mkubwa wa wadau pamoja na mazingira mazuri ya biashara yanayoendelea kuwekwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa Profesa Kamuzora, idadi ya watu wanaoingia katika uzalishaji na biashara ya kahawa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, jambo linaloonyesha imani kubwa ya wawekezaji na wananchi katika sekta hiyo.

Aidha, amesema kahawa ya Tanzania inaendelea kupata nafasi kubwa katika masoko ya kimataifa, hali inayochochea ushindani na kuongeza mchango wa zao hilo katika uchumi wa nchi.

Akizungumzia semina ya wadau wa kahawa ya mwaka huu, amesema imeandaliwa kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu mwelekeo wa sekta hiyo, changamoto zilizopo na fursa zinazoweza kuchochea ukuaji endelevu wa tasnia ya kahawa.

Mada kuu ya mkutano huo ni “Kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji katika Sekta ya Kahawa kwa Ajili ya Kuimarisha Masoko na Maendeleo Endelevu.”

Amesema mada hiyo imechaguliwa kutokana na mahitaji yanayoongezeka ya masoko ya ndani na kimataifa yanayotaka kuona uwazi wa mnyororo mzima wa thamani wa kahawa kuanzia shambani hadi kwa mlaji wa mwisho.

“Leo walaji wa dunia hawataki tu kunywa kahawa. Wanataka kujua imetoka wapi, imelimiwa na nani, katika mazingira gani na kwa kutumia mbinu zipi. Hivyo, tunalazimika kwenda sambamba na mahitaji hayo ya soko la kimataifa,” amesema.

Amefafanua kuwa mataifa yanayofanikiwa katika biashara ya kahawa duniani yameweza kujenga simulizi za kahawa zao kwa kueleza historia ya uzalishaji kuanzia kwa mkulima, eneo la uzalishaji, pembejeo zilizotumika hadi hatua za uchakataji.

Kutokana na hali hiyo, amesema TCB imeanza utekelezaji wa mfumo wa upimaji na utambuzi wa mashamba ya kahawa ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi zinazohitajika na wanunuzi wa kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo amesema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya mazingira ya biashara ya kimataifa.

Amewashukuru wadau wa sekta ya kahawa kwa mchango wao katika kuendeleza uzalishaji na biashara ya zao hilo, akisema ushirikiano huo umechangia mafanikio makubwa yanayoendelea kushuhudiwa nchini.

“Tunawashukuru wadau wote kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa katika kuendeleza sekta ya kahawa. Ushirikiano huu umetuwezesha kufikia mafanikio mbalimbali na kuendelea kujenga hadithi ya kahawa bora ya Tanzania,” amesema Kimaryo.

Hata hivyo, amesema sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri uzalishaji wa kahawa katika maeneo tofauti nchini na duniani kwa ujumla.

“Wakulima wetu wanaendelea kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Hivyo ni muhimu kuendelea kujadili na kutafuta suluhisho la pamoja litakalosaidia sekta hii kuendelea kukua kwa uendelevu,” amesema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Thomas Mbwana amesema mkutano huo unatoa fursa kwa wadau kutafakari mafanikio yaliyofikiwa, kubaini fursa zilizopo na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ushindani wa kahawa ya Tanzania katika soko la dunia.

Amesema ushiriki wa wadau katika mijadala hiyo utasaidia kupata mapendekezo yatakayochochea ukuaji wa sekta ya kahawa na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

“Kwa pamoja tutapata mwelekeo sahihi wa mustakabali wa sekta ya kahawa kwa manufaa ya wakulima, wafanyabiashara na taifa letu kwa ujumla,” amesema.