TCCIA wafurahishwa na mapendekezo ya bajeti

Friday June 11 2021
tcaa pic

Dar es Salaam. Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Paul Koyi, amesema uamuzi wa Serikali kupunguza baadhi ya tozo  zilizokuwa zinaathiri  sekta ya kilimo na viwanda kunachochea na kuweka mazingira wezeshi na ukuaji wa viwanda vya  ndani.

 Taarifa ya chemba hiyo imetolewa leo Ijumaa Juni 11,2021 ikiwa ni siku moja imepita  baada ya Serikali kuwasilisha  bungeni mapendekezo ya bejeti  kwa  mwaka 2021/2022 ya Sh36.33 trilioni.

Koyi amesema  kufanya hivyo  kunaonyesha kuwa nchi inaweka sera ya kulinda viwanda vya ndani ambavyo vinatumia malighafi za ndani na  bidhaa zitakazotengezwa zitalinufaisha taifa moja kwa moja kupitia kodi.

 “Serikali imefanya vizuri kuzuia uingizwaji holela wa bidhaa kutoka nje ya nchi kwasababu kutakuwa na usawa  hali itakayochochea  ushindani kati ya viwanda vya ndani na vya nje,”amesema Koyi

Koyi amepongeza utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma Liganga  na bomba la mafuta ghafi.


Advertisement

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo utachochea maendeleo katika sekta binafsi, ajira na kkuendeleza viwanda pamoja na biashara kupitia miradi ya kushirikiana kati ya sekta binafsi na Serikali.

Koyi amesema katika suala la kodi licha ya kupunguzwa lakini ni vema vyombo vinavyohusika  na ukusanyaji kodi vikatumia njia  rafiki itakayomfanya  mfanyabiashara kutimiza wajibu wake  wa kulipa kodi bila kushurutishwa.

“Kwa siku za nyuma  kulikuwa na malalamiko vyombo hivyo  vilikuwa vinatumia nguvu  kwenye ukusanyaji kiasi kwamba mfanyabiashara alikuwa anaona kulipa kodi ni kama adhabu, naiomba Serikali inawezekana kupunguza kodi isiwe shida lakini watu wanaohusika wanatakiwa kutumia njia sahihi ,”amesema Koyi


Advertisement