TCD yawakutanisha Kinana, Mbowe, Lipumba na Zitto

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Abdulrahman Kinana akisalimiana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe leo Jumanne, jijini Dar es Salaam. Wakati wa kikoa cha TCD kinachoundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo, CCM, CUF na Chadema. Vyama vyote vitano vimeshiriki kikao hicho.

What you need to know:

  • Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kinachoundwa na vyama vya CCM, NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo, CUF na Chadema kimefanya kikao na kuwakutanisha vigogo wa vyama hivyo vyote vitano chini ya Uenyekiti wa Abdulrahman Kinana.

Dar es Salaam. Viongozi wa vyama vya siasa nchini ambao ni wajumbe wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) wamekutana katika kikao cha ndani kujadilina masuala mbalimbali.

TCD inaundwa na CCM, NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo, CUF na Chadema ambavyo vina wabunge na madiwani na Mwenyekiti wake ni Abdulrahman Kinana ambaye ni makamu mwenyekiti wa CCM-Bara.

Katika kikao hicho kimefanyika leo Jumanne, Machi 28, 2023 katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, CCM iliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wake Bara, Abdulrahman Kinana ambaye ndiye Mwenyekiti wa TCD.

Viongozi walioshiriki kikao hicho kilichoanza saa 10 jioni ni, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Anamringi Macha, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu na Kiongozi wa chama, Zitto Kabwe.

Kadhalika, aliyehudhuria kwa upande wa Chadema ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, John Mnyika.

Profesa Ibrahim Lipumba ndiye aliyeiwakilisha CUF katika kikao hicho kilichodumu kwa takriban saa mawili.

Katika kikao hicho, Duni alikuwa wa kwanza kuingia majira ya saa 9:40, akifuatiwa na Profesa Ibrahim Lipumba, baadaye Mbowe kisha Zitto.

Kinana alikuwa wa mwisho kuingia katika kikao hicho, alifika saa 10:06 jioni na moja kwa moja aliingia ukumbini humo.

Kikao hicho kilikuwa na agenda 13 huku suala la Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi ikiwa si sehemu ya mjadala kwenye kikao.

Kikao hicho kiliongozwa na ajenda ya kufungua kikao, kuthibitisha ajenda za kikao cha Machi 28, 2023, muhtasari wa kikao cha SUMMIT cha Oktoba 24, 2022.

Nyingine ni yatokanayo na kikao cha SUMMIT cha Oktoba 24, 2022, taarifa ya kazi ya Kituo kutoka Oktoba 2022 hadi Machi 2023, taarifa za program zijazo.

Pia, ilikuwemo ajenda ya marekebisho ya Katiba ya TCD, ripoti ya exchange visit ya Burundi na Tanzania ya Februari 27 hadi Machi 2, mwaka huu na muongozo wa majadiliano wa vijana.

Ajenda nyingine ni bajeti ya Kituo ya mwaka na bajeti ya mishahara ya watumishi kuanzia Oktoba 2022 hadi Juni 2023.

Tamko la kumpongeza Rais, Mengineyo na kufunga kikao ni ajenda nyingine zilizokuwepo.