TEF: Tunahitaji marekebisho kuimarisha tasnia

Muktasari:

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesema si sheria zote za habari zina ukakasi bali ni chache ambazo zinahitaji marekebisho yatakayoboresha zaidi tansia hiyo.

Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesema si sheria zote za habari zina ukakasi bali ni chache ambazo zinahitaji marekebisho yatakayoboresha zaidi tansia hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo, Ijumaa, Agosti 5, 2022 jijini Dar es Salaam na mjumbe wa TEF, Rashid Kejo alipowatembelea wahariri wa magazeti ya Serikali Mgaya Kingoba (Habari Leo) na Christopher Majaliwa (Daily News) kwa ajili ya kueleza kwa upana mchakato wa maboresho ya sheria ya huduma za habari.
“Mchakato huu wa mabadiliko ya sheria, haulengi kung’oa sheria zote kwa kuwa, zipo nzuri na zenye maana kubwa katika tasnia ya habari, mfano kulazimisha maofisa wa Serikali kutoa taarifa kwa waandishi, kutambua masilahi na mikataba ya waandishi, ha ya ni mambo mazuri, yapo mengi.
“Lakini kuna maeneo ambayo yana athari kubwa kwa waandishi na vyombo vya habari, maeneo hayo ni mwandishi anaweza kufungwa hata asipoitwa mahakamani, usajili wa magazeti kila mwaka, uhuru wa hakimu kumfunga mwandishi apendavyo na mengine kama hayo, ndio tunapigania yaondolewe,” amesema Kejo.
Alieleza kuwa, Sheria ya Habari ya Mwaka 2016, ina maeneo yanazuia kukua kwa tasnia hiyo akitoa mfano sheria inayozungumzia utwaaji wa vifaa vya vyumba vya Habari kwa uchunguzi, lakini pia mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Habari Malelezo ya kupeleka matangazo kule anakojisikia.
Alisema, taasisi zote zimeelekezwa kupeleka matangazo Habari Maelezo, ambao mkurugenzi wake ndiye atayeamua chombo cha habari cha kutangaza.
“Serikali ndiyo mtangazaji mkubwa, sasa chombo kitachoonekana kukosoa serikali bila shaka kitakosa matangazo, hapo ni kuua kazi ya uanahabari lakini pia kuua uchumi wa wanahabari.
“Lakini pia, tasnia ya habari inahitaji uwekezaji mkubwa, sheria yetu inambana mwekezaji wa nje ya nchi kuwekeza kwa asilimia 100, ametakiwa sizidi asilimia 49 tu, huku ni kufanya tasnia idumae. Tunatamani haya yote yabadilishwe,” alisema Kejo.
 James Marenga, wakili wa kujitegemea akizungumza na Kituo cha Radio cha Tumaini  (Tumaini FM), jijini Dar es Salaam jana alisema, mabadiliko ya sheria huwa yanachukua muda mrefu, wakati wa sasa ni mzuri kwa kuwa, rais aliyepo madarakani ameonesha dhamira hiyo.
“Mchakato wa marekebisho ya sheria iliyotungwa mwaka 2016, ulichukua miaka 10. Mchakato huo ulianza mwaka 2006, ni bahati utawala uliopo umeona kuna haja ya kupitia upya sheria hizi kama ambavyo wadau wamekuwa wakipiga kelele,” alisema Marenga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania (MISA TAN), alisema zipo sheria kadhaa zinazopigiwa kelele ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Habari Maelezo kufungia vyombo vya habari pasi na kupelekwa kesi mahamani.
“Tunaamini sheria hizi na zingine ambazo tumeorodhesha kwenye nakala yetu ya mapendekezo ya mabadiliko, wadau na serikali kwa pamoja tutapitia na kuona namna ya kunyoosha ili mapendekezo hayo yatapopelekwa bungeni, tuwe na msimamo unaofanana,” alisema.