Tembo zaidi ya 50 wavamia Handeni

Muktasari:
- Tembo zaidi ya 50 wamevamia kwenye mashamba ya wananchi wa kijiji cha Nkale kata ya Segera wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga na kuharibu michungwa, mikorosho na mazao mengine huku wananchi wakikimbia nyumba zao.
Handeni. Tembo zaidi ya 50 wamevamia kwenye mashamba ya wananchi wa kijiji cha Nkale kata ya Segera wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga na kuharibu michungwa, mikorosho na mazao mengine huku wananchi wakikimbia nyumba zao.
Mashuhuda wamesema walianza kugundua uwepo wa tembo hao saa saba mchana na baadaye walivyofuatilia walibaini ni zaidi ya 50 na tayari wameanza kushambulia mazao yao na kwa hofu wameanza kukimbia makazi.
Mkazi wa eneo hilo, Victor Robert amesema majira ya asubuhi alipewa taarifa na jirani yake kuna tembo wamevamia eneo lao ambapo alipanda juu ya mti kufuatilia na kwa mahesabu ya haraka alibaini wapo zaidi ya tembo 50.
"Kwa macho yangu nilipopanda juu mti na kuwahesabu wapo Tembo zaidi ya 50, tunashukuru hakuna madhara kwa binadamu ila mazao ya majirani zetu kama michungwa na mengine yameharibiwa," amesema Victor.
Aidha, Elizabeth Abel amemuomba mkuu wa wilaya kuongea na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (Tawa) kuhakikisha wanafukuza Tembo hao kwani ni muda mrefu wanasumbua maeneo mbalimbali ila hatua hazichukuliwi.
Mkuu wa wilaya ya Handeni (DC), Siriel Mchembe amefika eneo hilo na kuwataka wananchi kuwa watulivu huku akiwataka Tawa kufika haraka kuangalia uwezekano wa kwenda kuwathibiti ili wasilete madhara zaidi.
"Tembo hawa wamevamia mashamba na makazi ambayo yapo karibu na mashamba yao, wakina mama na watoto wamekimbia wamebakia vijana ambao wanaangalia mwenendo wa Tembo na kutoa taarifa kuwa wanaelekea wapi, Tawa wafike haraka sana kuja kuwaokoa wananchi wangu na Tembo hawa," amesema Mchembe.
Naye Katibu tawala wilaya ya Handeni, Mashaka Mgeta amewataka maofisa tarafa,watendaji wa kata pamoja na wenyeviti wa vijiji kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa Tembo hao kwenye maeneo yao na wakiona dalili za kutokea madhara watoe taarifa mapema.