Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tendwa ashauri liundwe baraza la ushauri la uchaguzi

Msajili mstaafu wa vyama siasa nchini, John Tendwa

Muktasari:

Msajili mstaafu wa vyama siasa nchini, John Tendwa ameshauri kuundwe Baraza la Ushauri la Uchaguzi la Kitaifa litakalokuwa na jukumu la kutatua migogoro ya kisiasa ambayo haina ulazima wa kwenda mahakamani.

Dar es Salaam. Msajili mstaafu wa vyama siasa nchini, John Tendwa ameshauri kuundwe Baraza la Ushauri la Uchaguzi la Kitaifa litakalokuwa na jukumu la kutatua migogoro ya kisiasa ambayo haina ulazima wa kwenda mahakamani.

Akizungumza Dar es Salaam leo Mei 05/2022 baada ya kutoka kutoa maoni yake kwenye Kikosi Kazi, kinachokusanya maoni kuhusu Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa nchini, Tendwa amesema kwa sasa kuna migogoro mingi ya kisiasa inayopelekwa mahakamani ambayo haikuwa na ulazima huo,  badala yake inasababisha mrundikano.

“Kuanzishwa kwa Baraza hili ambalo litakuwa linafanya kazi kwa ukaribu na Tume ya Uchaguzi, litakuwa linashughulikia na kama itakuwa inashindikana basi wakikata rufaa ndipo iende mahakamani,” amesema.

Tendwa ambaye mwaka 2013 alistaafu kwa mujibu wa sheria, katika maelezo yake amefafanua kuwa baraza hilo pia litakuwa linajukumu la kutoa elimu ya siasa na kukuza demokrasia nchini.

“Baraza hilo likiundwa kutaisaidia kuipunguzia mzigo Tume ya Uchaguzi ambayo muda mwingine imekuwa ikikasimisha majukumu kwa idara zingine kutokana na kuelemewa na majukumu,” amesema

 Pia ameshauri kwamba kundi la vijana na akinamama  waendelee kupewa kipaumbele kwenye nafasi mbalimbali hususan kwenye vyombo vya maamuzi.

“Vyama vyote na serikali vinapaswa kuanzisha sera ya kukuza na kuyapa kipaumbele makundi hayo, wanatakiwa kupewa elimu ya utayari kuhusu siasa na kushiriki katika kutoa maamuzi,” amesema Tendwa.

Kuhusu Katiba Mpya ameshauri ni vizuri ikapatikana kwa sasa ili kusaidia kutuliza mijadala inayoendelea huku akidai ipatikane kwa uwazi katika mfumo ambao jamii yote itaridhia.

“Katiba mpya ni  muhimu kwa sababu imeshazungumzwa ipatikane  na  rasimu yake ilishaandikwa na  kama tunataka iliyopo  iendelee kutumika basi isahihishwe na kuongezwa mengine kuboresha kabla ya uchaguzi mkuu,” amesema Tendwa.

Asasi nyingine ya kiraia iliyojitokeza leo mbele ya kikosi hicho ni The Right Way waliopendekeza Vyama vya Siasa kujenga utamaduni wa kufanya mazungumzo pale linapojitokeza tatizo badala ya kulumbana.

"Utamaduni wa kukutana walau upatikane kila baada ya miezi mitatu ambapo wadau mbalimbali wasiasa wakusanyike kubainisha changamoto kwa uwazi na kuzitatua na mawazo yanayopatikana yanasaidia kuboresha,"amesema Mkurugenzi Mtendaji wa The Right Way, Dk Wallace Mayunga,   

Kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi taasisi hiyo imependekeza kwamba upanuliwe wigo ili na makundi mengine yaingie jambo linaloweza kusaidia kurudisha imani kwa wananchi kuhusu chombo hicho.

 "Jukumu la Tume Huru inatakiwa majukumu iliyopewa kikatiba lazima iyasimamie ipasavyo lakini tunataka Tume itamke na makundi mengine yaingie ikiwemo vijana na wawakilishi mbalimbali kama ilivyo kwenye hiki kikosi Kazi," amesema.

Hata hivyo taasisi isiyo ya kiserikali inayoshughulikia mambo ya utawala bora na maendeleo nchini (The Center for Good Governance and Development in Tanzania -CEGODETA) ili kuondoa malumbano na migogoro isiyoyalazima ni vyema nchi ikaunda serikali ya kitaifa itakayokuwa inashirikisha wapinzani kama wanavyofanya Zanzibar.

Akizungumza Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Hamad Tau amesema kuundwa kwa serikali hiyo ya mseto kutasaidia kudumisha amani na maelewano bahina ya chama tawala na vile vya upinzani.

 Pia wameshauri umuhimu wa wazee kupewa viti maalumu kwenye vyombo vya maamuzi ikiwemo Bungeni huku akitolea mfano kama nafasi hiyo inavyotolewa kwa wanawake.

“Wazee ni kundi mahimu na wanamchango mkubwa katika maendeleo ya taifa hili na wazee wakiambiwa waingie kwenye kugombea wanashindwa kushindana kwa sababu wanakosa ushawishi mbele ya vijana," alisema.