TET yaadhimisha siku ya kimataifa ya kujua kusoma na kuandika

Vitabu vya kujifunzia na kufundishia vikiwa vimepangiliwa vizuri katika kabati.
Muktasari:
- Kila ifikapo Septemba 8, Tanzania huungana na mataifa mengine duniani katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kujua kusoma na kuandika.
Kila ifikapo Septemba 8, Tanzania huungana na mataifa mengine duniani katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kujua kusoma na kuandika.
TET inachukulia kwa uzito na umuhimu mkubwa siku hii muhimu duniani na kwa nchi yetu.
Siku hii inatukumbusha umuhimu wa kuhakikisha kuwa tunatekeleza kwa umakini mkubwa majukumu yetu ya kuandaa mitaala, kuandaa vifaa saidizi vya kutekeleza mitaala na kutoa mafunzo kazini kwa walimu yenye lengo la kuwawezesha kufanikisha ujifunzaji na ufundishaji kwa umahiri na kuwawezesha wanafunzi kumudu stadi za kusoma na kuandika katika umri husika.

Vitabu vya kiada kwa ajili ya kujifunzia na kufundishia kwa ngazi ya elimu ya sekondari
Ikumbukwe kuwa kusoma na kuandika ni nyenzo muhimu ya kuwasiliana na kujipatia maarifa na taarifa mbalimbali.
Aidha, moja ya stadi muhimu za karne ya 21 ni kuwasiliana.
Hivyo, kujua kusoma na kuandika ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha Watanzania kuwasiliana kwa ufasaha na hivyo kumudu maisha na kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo katika karne ya 21.
TET katika kuadhimisha siku hii, itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa vitabu na machapisho mbalimbali yanayolenga kusaidia kukuza stadi za kusoma na kuandika.
Ili kuhakikisha kuwa machapisho mbalimbali yanapatikana kwa urahisi, TET imetengeneza maktaba mtandao yenye machapisho mbalimbali yanayopatikana bure kupitia tovuti ya www.tie.go.tz.
Taasisi pia inashirikiana na wachapaji binafsi kuhakikisha upatikanaji wa vitabu vya hadithi, riwaya na vitabu vingine vya ziada.

Watoto wakijisomea maktaba.
Taasisi inasisitiza matumizi ya machapisho haya ili kukuza uwezo wa mwanafunzi kujua kusoma na kuandika.
TET pia imeandaa vipindi mbalimbali vya televisheni na redio vyenye lengo la kukuza uwezo wa watoto kujenga stadi za kusoma na kuandika.
Pia, TET inaendelea kuandaa maudhui ya kieletroniki kwa kutengeneza vikaragosi vyenye lengo la kumsaidia mtoto kujifunza kusoma na kuandika kwa kuona uundaji wa herufi na namna ya kusoma matamshi ya herufi mbalimbali.
Vikaragosi ni njia inayosaidia kumfanya mtoto kuji-funza hali akifurahia kwa kuangalia picha za vikaragosi.
Aidha, Taasisi inafanya kazi kwa karibu sana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa mwanafunzi anajenga stadi za kusoma na kuandika katika umri husika. Baadhi ya wadau hao ni Room-To-Read, Right To Play, Jifunze Uelewe na Plan International.
Kwa kushirikiana na wadau hawa TET imeweza kutoa mafunzo kwa walimu yenye lengo la kuwawezesha kumudu njia shirikishi za ufundishaji unaolenga kuwawezesha wanafunzi kupata umahiri wa kusoma na kuandika katika umri uliokusudiwa.
Taasisi inawakumbusha wazazi kuwa tunaposherehekea siku hii tukumbuke juu ya jukumu letu la kuwasaidia watoto wetu kujua kusoma na kuandika katika umri unaokusudiwa.
Wazazi wawape watoto nafasi ya kujisomea wawapo nyumbani, wawapatie makala mbalimbali za kujisomea, wawahimize kuhudhuria shuleni na kushiriki shughuli mbalimbali nje ya mtaala zenye lengo la kukuza stadi za kusoma na kuandika.
Aidha, wazazi washiriki katika kujenga utamaduni wa watoto kupenda kujisomea kwa kuwanunulia machapisho mbalimbali yatakayo wasaidia katika kukuza stadi za kusoma na kuandika.
TET inasisitiza kuwa suala la kuhakikisha kuwa watoto wanajua kusoma na kuandika ni jukumu la jamii nzima, hivyo sote tushirikiane kuhakikisha kuwa watoto wote katika umri wa miaka 5-6 wanamudu kwa ufasaha stadi za kusoma na kudika.
Kuhusu TET
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ni Taasisi ya Umma iliyo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 13 ya Mwaka 1975 (Sura ya 142 Marejeo ya 2002).
Kwa mujibu ya Sheria hiyo majukumu makuu ya TET ni:
1. Kubuni, kuandaa na kuboresha mitaala ya Ngazi ya awali, msingi, sekondari na elimu ya ualimu (Astashahada na Stashahada).
2. Kuandaa vifaa saidizi vya kutekeleza mitaala kama vile vitabu vya kiada, viongozi vya mwalimu, miongozo mbalimbali ya kufundishia na moduli. Kazi hii pia inahusisha kusimamia taratibu za uidhinishwaji wa vitabu vya ziada.
3. Kutoa mafunzo kazini kwa walimu na wasimamizi wa utekelezaji wa mitaala (wadhibiti ubora, maofisa elimu wa mikoa, wilaya na kata) ili kuwawezesha kutekeleza mitaala kadri ya matarajio.
4. Kufanya utafiti na kutoa ushauri elekezi kwa Serikali na wadau wengine wa elimu juu ya mitaala na masuala mengine yanayohusiana na ubora wa elimu.