Tigo, mwanzo ilibadili majina sasa imeuzwa

Tigo, mwanzo ilibadili majina sasa imeuzwa

Muktasari:

  • Baada ya mmiliki wa kampuni ya mawasiliano ya Tigo, MIC kusema amekubali kuuza hisa zake zote kwa ubia unaoongozwa na Axian, Tigo imesema mabadiliko yaliyotokea mwanzo yalikuwa ni jina la biashara pekee si mwanahisa.

 Dar es Salaam. Baada ya kubadili majina mara tatu ndani ya miaka 26, kwa mara ya kwanza sasa, hisa za kampuni ya Tigo zinauzwa wa mwekezaji mwingine.

Mkurugenzi mtendaji wa Tigo Tanzania, Simon Karikari amesema tangu mwaka 1995 kampuni hiyo ilipoanza kutoa huduma nchini ikiitwa Mobitel halafu Buzz na sasa Tigo, ilikuwa inamilikiwa na Millicom International Cellular (MIC) ambayo mwaka 2018 ilinunua hisa za Zantel.

“Ni kweli majina ya kibiashara yalibadilika lakini mmiliki aliendelea kubaki Millicom. Tigo ni kampuni ya kibunifu inayoheshimika sokoni. Kutokana na ufanisi wake, inavutia wawekezaji wengi wa kimataifa,” amesema Karikari.

Aprili 19, Millicom ilitanga ilitangaza kuuza hisa zake zote kwa ubia wa kampuni kadhaa unaoongozwa na Axian ya Madagascar ikikamilisha mpango wake wa kuondoka kabisa barani Afrika baada ya kuwekeza kwa muda mrefu. Kampuni ya Millicom ilianzishwa mwaka 1990 na miaka mitano baadaye ikawekeza nchini.

Tayari, Axian  inayotoa huduma pia katika mataifa ya Madagascar, Reunion na Mayotte, Comoro, Senegal na Togo imesema imeyabaini maeneo manne ya kipaumbele.

Kampuni hiyo inakusudia kuboresha ujenzi wa miundombinu ili kufikisha huduma kwa wananchi wengi zaidi, kutanua wigo wa upatikanaji wa huduma nafuu za mawasiliano, kuboresha huduma za fedha na kuimarisha weledi wa wafanyakazi wake.

Ofisa mtendaji mkuu wa Axian, Hassanein Hiridjee anasema: “Tunaenda kufungua ukurasa mpya Tanzania na Zanzibar utakaodumu kwa muda mrefu. Tumejiridhisha kwamba mfumo wetu utasaidia kuongeza matumizi ya simu na kusaidia kukuza uchumi.”

Axian yenye zaidi ya wafanyakazi 5,000 katika mataifa inakotoa huduma, ilikuwa miongoni mwa kampuni nane zilizoomba kununua hisa za Tigo na Zantel kutoka Millicom.

Kwa takriban miongo mitatu ya kutoa huduma nchini, Tigo imepitia mabadiliko kadhaa yaliyoboresha husuma kwa wananchi.

Miaka mitano baada ya kuanzishwa nchini, ilizindua huduma za Tigopesa, mwaka 2010 na miaka mitatu baadaye ikawa na usajili wa watoto wanaozaliwa kidijitali halafu m waka 2014 ikazindua Facebook kwa Kiswahili na 2015 ikawa na simu ya kisasa kwa Kiswahili.

Nembo ya mawasiliano ya kampuni ya Axian inayohudumu zaidi katika nchi zinazozungumza Kifaransa ni Telma hivyo, Tanzania ikiwa ya kwanza isiyotumia Kifaransa kuwa na huduma za Telma.

Hata hivyo, Karikari anasema sekta ya mawasiliano inabadilika kwa kasi kubwa duniani kote kutokana na maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia. “Siwezi  kusema moja kwa moja kuwa nembo ya Tigo itabadilika,” anaeleza.