TMDA yaikabidhi Magereza dawa zenye thamani ya Sh20 milioni

Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Nyanda za Juu Kusini, Anita Mshighati akikabidhi dawa zenye thamani ya zaidi ya Sh20 milioni kwa Kamishna Msaidizi wa Magereza, Ismail Misama Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya.

Mbeya. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imekabidhi Magereza Kuu Ruanda Mkoa wa Mbeya dawa zenye zaidi ya thamani Sh20 Milioni.

Akizungumza jana Ijumaa Juni 23 katika makabidhiano hayo, Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Nyanda za Juu Kusini, Anita Mshighati, amesema dawa hizo zimepatikana baada ya ukaguzi uliofanywa ndani ya mwaka mmoja.

Amesema asilimia kubwa ya dawa zilizokamatwa zilikuwa zikiuzwa dukani kinyume na sheria katika baadhi ya maduka, hivyo kuliko kwenda kuziharibu bora zikatumika kwenye vituo vya afya.

"Tumechagua gereza letu la hapa kwa kutoa dawa ili isaidie kwa wafungwa na jamii inayozunguka ambao wanatumia zahanati hii.

"Asilimia kubwa ya dawa ni zile za kujipata, presha na kupunguza maumivu ambazo wengi walikuwa wakiuza kinyume na taratibu," anasema Bi Anita.

Aliongeza moja ya adhabu wanazokutana nazo wanokiuka sheria ni pamoja na kunyang'anywa dawa na kulipa faini kulingana na sheria ya nchi pamoja na sheria ya baraza la famasi.

Ameomba wamiliki wa maduka ya dawa kuwatumia wataalamu katika kusimamia maduka yao sababu ni biashara ya taaluma hivyo kuna watu ambao wamesomea na ndio maana kuna baadhi ya maduka muhimu hawaruhusiwi kuziuza.

"Kuna jambo lingine kwa hawa wataalamu wa dawa ambao hawafuati sheria kwa kuweka dawa zisizotakiwa na wanakwenda mbali kwa kutoa huduma kinyume na sheria maana tumewahi kusikia wengine wakichoma sindano watu kitu ambacho sio sahihi," anasema Bi Anita.

Kamishna Msaidizi wa Magereza, Ismail Misama Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya amesema uhitaji ni mkubwa sababu zahanati hiyo hutumiwa na watu wengi ambao huwazunguka.

"Waharifu wengi hawana bima ya afya hivyo hizi dawa zitanisaidia sana sababu wanapokwenda hospitalini huandikiwa dawa lakini hawapewi hivyo tunaanza kuhangaika."

Mganga mfawidhi Mkuu wa zahanati hiyo, Mrakibu wa Magereza Alex Buhinu amesema msaada huo itasaidia kupunguza idadi ya kuwahamisha wagonjwa kwenda hospitali kubwa kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu.