TPDC yaeleza utaratibu malipo wananchi ujenzi bomba la mafuta

TPDC yaeleza utaratibu malipo wananchi ujenzi bomba la mafuta

Muktasari:

  • Wananchi ambao nyumba zao zitabomolewa kupisha mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga nchini Tanzania watajengewa nyumba nyingine kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja.

Tabora.  Wananchi ambao nyumba zao zitabomolewa kupisha mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga nchini Tanzania watajengewa nyumba nyingine kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Julai 7, 2021 na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk James Mataragio wakati wa utoaji saini mkataba w amalipo ya wananchi ambao bomba hilo litapita katika makazi yao kijiji cha Sojo kata ya Igusule wilayani Nzega.

Amesema wakati wanasubiri kujengewa nyumba ,wananchi hao watapangiwa nyumba hadi nyumba zao zitakapokamilika kujengwa.

Mbali na kupangiwa nyumba, amesema wananchi hao watapewa huduma mbalimbali katika kipindi chote ambacho nyumba zao zinajengwa.

Amebainisha kuwa wananchi hao watapata malipo ya fidia na pia nyongeza ya malipo mbadala kulingana na athari ambazo watazipata na kwamba kuna kambi 14 nchi nzima na Mkoa wa Tabora ndio utakaokuwa na kambi kubwa zaidi na hata kuwalipa wananchi kutaanzia mkoani humo.

Mkurugenzi mkuu wa mradi wa bomba hilo Afrika Mashariki (EACOP), Martin Tiffen amemueleza Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani kuwa wataanza kulipa kuanzia kesho Alhamisi shughuli itakayofanyika ndani ya wiki mbili.

Imeandikwa na

Robert Kakwesi, Mwananchi