TPDC yatoa elimu ya gesi, mafuta kwa wanafunzi Lindi

Ofisa uhusiano mwandamizi kutoka TPDC, Alfred Mpokela akitoa elimu ya mafuta na gesi kwa wanafunzi wa Sekondari ya Lindi. Picha na Bahati Mwatesa.
Muktasari:
- Juhudi za TPDC katika kutoa elimu ya mafuta na gesi kwa wanafunzi zina mchango mkubwa katika kuwaandaa wataalamu wa siku zijazo.
Lindi. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa elimu kuhusu mafuta na gesi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lindi kwa lengo la kuwahamasisha kujiandaa kuwa wataalamu wa sekta hiyo katika miaka ijayo.
Akizungumza na wanafunzi hao jana, Jumamosi Februari 22, 2025, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa TPDC, Alfred Mpokela, amesema shirika hilo lina jukumu la kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi ili baadaye wawe wataalamu wa mafuta na gesi.
"Licha ya shughuli za utafiti wa mafuta na gesi, pia tunawajibika kutoa elimu katika shule za sekondari ili kuwahamasisha wanafunzi. Tunahitaji wataalamu wa kutosha katika miaka ijayo," alisema Mpokela.
Sada Juma, mwanafunzi wa kidato cha pili na mwanachama wa Klabu ya TPDC shuleni hapo, amesema klabu hiyo inawasaidia kutambua faida za mafuta na gesi pamoja na fursa za ajira katika sekta hiyo.
"TPDC itatusaidia kupata ajira katika kampuni zinazoshughulika na mafuta na gesi. Nawaomba wanafunzi wenzangu wajiunge na klabu hii kwa sababu ina manufaa makubwa," amesema Sada.
Kwa upande wake, Juma Shabani, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, amesema elimu waliyopewa itamsaidia kufikia malengo yake ya kuwa mtafiti katika sekta ya mafuta na gesi.
"Baada ya kupata elimu hii, nitasomea masomo ya sayansi ili kutimiza ndoto yangu ya kuwa mtafiti wa mafuta na gesi," amesema Shabani.
Kwa mujibu wa TPDC, shirika hilo linaendesha shughuli zake katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo kitalu cha Ruvu na mradi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki (EACOP). Hata hivyo, Lindi na Mtwara ndizo mikoa pekee zinazozalisha gesi asilia, ambayo imechangia ukuaji wa uchumi kwa kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa matumizi ya viwanda na majumbani.
Klabu ya TPDC katika Shule ya Sekondari Lindi ilianzishwa miaka 10 iliyopita na imekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu mafuta na gesi, kuwaunganisha na taasisi za elimu ya juu zinazofundisha masuala ya nishati, pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi.