TRA yaanza operesheni matumizi mashine ya EFD Kilimanjaro

Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Masawa Masatu (kulia) akizungumza na mmiliki wa duka la vinywaji vikali usiku wa kuamkia leo wakati wa operesheni na ukaguzi unaofanywa na maofisa wa mamlaka hiyo. Picha na Florah Temba
Muktasari:
- Mamlaka ya mapato nchini (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro imeanza operesheni ya usiku na mchana kukagua matumizi ya mashine za kielektroniki na vinywaji visivyo na stepu za kielektroniki lengo likiwa ni kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata sheria.
Moshi. Mamlaka ya mapato nchini (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro imeanza operesheni ya usiku na mchana kukagua matumizi ya mashine za kielektroniki na vinywaji visivyo na stepu za kielektroniki lengo likiwa ni kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata sheria.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ongezeko la watu katika mkoa huo kwa kipindi hiki cha sikukuu.
Akizungumza usiku wa leo Jumatano, Desemba 22, 2021 wakati wa operesheni hiyo Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Masawa Masatu mara baada ya kufanya ukaguzi katika maduka makubwa, kumbi za starehe na baa kubwa amesema wameendelea kufanya ukaguzi usiku na mchana katika maeneo ya biashara ili kuhakikisha wafanyabiashara wote wanafuata sheria.
Amesema Mkoa wa Kilimanjaro ni moja ya mikoa ambayo inakuwa na bahati ya kuwa na wageni wengi kipindi hiki cha mwisho wa mwaka hali inayosababisha changamo ya utoaji wa risiti za kielektroniki, magendo ya vinywaji, uuzaji wa vinywaji visivyo na stemp za kielektroniki na bidhaa bandia.
"Kutokana na mazingira hayo tumeanza operesheni za usiku kuwatembelea wafanyabiashara kujiridhisha kama sheria na taratibu za biashara zinazingatiwa na baada ya kuzunguka leo kufanya ukaguzi, tumeona kuna changamoto ngingi.
"Wengine tumebaini ni suala la uelewa, wengine ni kutozingatia sheria na wengine elimu wanayo na sheria wanazifahamu lakini hawazifuati, tumechukua hatua ya kuwaandikia hati za makosa wale wote tuliowabaini kuwa na makosa lakini pia wengine tumewapa elimu ili kuweza kufanya biashara zao kwa kuzingatia sheria na taratibul," amesema Masatu.
Aidha meneja Masatu ameeleza kuwa sheria inaeleza wazi kuwa wale ambao watabainika kufanya biashara bila kutoa risiti za EFD kiwango cha chini cha faini ni sh 3milioni huku kiwango cha juu kikiwa ni Sh4.5Milion na kwamba wanatakiwa pia kuitafuta kodi iliyokuwa ikipotea ili kuikomboa.
"Kwa wale ambao wanauza vinywaji ambavyo havina stemp za kielektroniki sheria imeweka kiwango cha faini ya Sh5 milioni hadi Sh50 milioni na katika ukaguzi tumeona wapo wafanyabiashara wengi ambao hawazingatii sheria za biashara bado watu wengi hawatoi risiti za kielektroniki na wanaona suala la utoaji risiti ni la kujisikia," amesema.
Akizungumza mmoja wa wafanyabiashara ambao walipitiwa usiku na maofisa wa TRA Bruno Ngoo, amewapongeza maofisa hao kwa hatua hiyo na kueleza kuwa ukaguzi huo utawafungua macho hata wafanyakazi wa maeneo hayo ambao wamekuwa ndiyo wahusika wa kutoa risiti.
"Suala la utoaji risiti wamiliki wa baa na kumbi hizi za starehe tumekuwa tukielekezwa kila wakati lakini TRA kuja kufanya ukaguzi usiku huu, kunawafanya hata wafanyakazi wetu kutambua umuhimu wa kutoa risiti kila wanapofanya mauzo maana ndiyo wanakuwa maeneo haya ya biashara," amesema Ngoo.