TRA yamdaka anayetuhumiwa kusambaza stempu feki
Muktasari:
- Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Mkoa wa Kilimanjaro imemkamata mfanyabiashara maarufu mjini Moshi aliyetambulika kwa jina moja la Mr Kimario kwa tuhuma za kujihusisha na mtandao wa kutengeneza na kusambaza stempu feki zenye jina la mamlaka hiyo zinazobandikwa kwenye vinywaji.
Moshi. Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Mkoa wa Kilimanjaro imemkamata mfanyabiashara maarufu mjini Moshi aliyetambulika kwa jina moja la Mr Kimario kwa tuhuma za kujihusisha na mtandao wa kutengeneza na kusambaza stempu feki zenye jina la mamlaka hiyo zinazobandikwa kwenye vinywaji.
Meneja wa TRA mkoani Kilimanjaro, Gabriel Mwangosi amesema mfanyabiashara huyo walimkamata juzi nyumbani kwake akiwa na shehena ya stempu hizo akiuza stempu 100 kwa Sh10,000 na wakati mwingine hushusha bei hadi Sh8,000.
“Huyu mfanyabiashara tumemkuta nyumbani kwake, pamoja na stempu tumekamata ethanol nyumbani kwake inayotumika kutengenezea spirit, siku zote sisi kama mamlaka ya mapato watu wa namna hii tunawachukulia hatua,” amesema Mwangosi.
Amesema stempu zinazosambazwa na mfanyabiashara huyo zinatumika kubandika kwenye vinywaji mbalimbali na kuuzwa bila kuzingatiwa taratibu.
Akizungumzia tukio hilo mkuu wa Wilaya ya Moshi, Rajabu Kundya amesema mfanyabiashara huyo amekuwa akihujumu mapato ya Serikali.
“Lazima achukuliwe hatua kali za kuihujumu nchi. Hakuna ubishi kwamba kukua kwa uchumi wa nchi yetu kungekuwa kwa kiwango cha juu sana kama kungekuwa hakuna watu wanatuhujumu kwa utaratibu huu, athari yake ni kubwa kwa uchumi wa nchi lakini kutoa vinywaji visivyofaa vikaharirishwa.”
"Mapato yaliyostahili kuingia kwenye mfumo rasmi wa Serikali yakahujumiwa kwa utaratibu huu yanakwenda kwa watu ambao hawakustahili na kuisababishia Serikali hasara," ," amesema Kundya.
Amebainisha kitendo kinachofanywa na mfanyabiashara huyo ni haramu na hatari kwa maisha ya watu,” lazima mapambano yaendelee kwa nguvu zote ili kuhakikisha jamii yetu inapata maendeleo yaliyokusudiwa na serikali yetu.”