Trafiki anayetuhumiwa kwa rushwa ya ngono atimuliwa

Trafiki anayetuhumiwa kwa rushwa ya ngono atimuliwa

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, limemfukuza kazi askari wake wa kikosi cha usalama barabarani kwa madai ya kujihusisha na rushwa ya ngono.

Moshi. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, limemfukuza kazi askari wake wa kikosi cha usalama barabarani kwa madai ya kujihusisha na rushwa ya ngono.

Askari huyo mwenye namba F.4958Cpl, Peter Albert Moshi alinaswa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humu Januari 6, mwaka huu kwa madai ya kuomba rushwa ya ngono kwa mama wa mtoto aliyegongwa na pikipiki ili amkamilishie taarifa ya uchunguzi wa awali.

Awali, askari huyo alikuwa akichunguza ajali ya pikipiki ambayo ilimgonga mtoto wa mama huyo na kusababisha kuvunjika mkono ambapo mpaka sasa anaendelea na matibabu.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Ronald Makona alisema tayari askari huyo wa kikosi cha usalama barabarani ameshachukuliwa hatua za kijeshi ikiwemo kumvua uaskari na kumfukuzisha kazi.

“Sisi Jeshi la polisi, askari yoyote akikamatwa na kosa la jinai kama hilo na kutakiwa kufikishwa Mahakamani, lazima tunachukua hatua za kijeshi kwanza ikiwa ni kumvua nafasi yake.

“Tayari sisi tumeshaachana naye, ataendelea na shtaka lake linalomkabili, hivyo hatuko naye tena. Tumeshamfukuza kazi, sasa hatua nyingine za kisheria zitafuata,” aliongeza Kamanda Makona.

Tukio la askari huyo kukamtwa kwa rushwa ya ngono liliibua hisia mbalimbali kwa wakazi wa Kilimanjaro na maeneo ya jirani ambapo walilaani, huku wakiendelea kuziomba mamlaka husika kuwashughulikia kwa adhabu kali askari wa namna hiyo.

Taarifa za awali za kiuchunguzi zilizofanywa na Takukuru mkoani hapa zilibaini askari huyo alikuwa akimsumbua mama wa muathirika kwa muda mrefu kuwa kama anataka haki ya mwanaye ipatikane haraka, basi hana budi kumpa rushwa ya ngono, hali ambayo ilisababisha kuchelewa kupelekwa Mahakamani na kusababisha mama wa mtoto kuzunguka kila siku kwenda kituo cha polisi bila mafanikio.

Wakati wowote kuanzia sasa askari huyo atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.