Transfoma zahujumiwa, Tanesco yapata hasara Sh21 milioni

Baadhi ya nyaya kopa zilizokamatwa wakati wa operesheni kwenye maduka ya kuuza vyuma chakavu

Muktasari:

Transifoma mbili za umeme vyenye thamani ya zaidi ya Sh21 milioni zilizokuwa kwenye maeneo ya vyanzo vya maji zimehujumiwa kwa kuharibiwa na kuibwa nyaya za kopa.

Bariadi. Transifoma mbili za umeme vyenye thamani ya zaidi ya Sh21 milioni zilizokuwa kwenye maeneo ya vyanzo vya maji zimehujumiwa kwa kuharibiwa na kuibwa nyaya za kopa.

Tukio lilitokea la usiku wa Juni 5, 2023 katika vijiji vya Kilalo na Kasori Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu na kusababisha vijiji hivyo kukosa kwa muda huduma ya maji na umeme.

Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Simiyu, Japhet Lufano amesema  kutokana na wizi huo, maofisa wa Tanesco wakishirikiana na wenzao wa Jeshi la Polisi wameendesha msako katika maduka na vibanda vinavyouza vyuma chaavu na kufanikiwa kukamata nyaya na bidhaa mbalimbali zinazoamini kupatikana baada ya miundombinu ya shirika hilo kuhujumiwa.

Amesema watu wanne wanashikiliwa kwa mahojiano kuhusu hujuma za miundombinu ya shirika hilo.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe kuzungumzia tukio hilo ikiwemo kufahamu majina ya wanaoshikiliwa zinaendelea.

Ofisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Simiyu, Evarist Katemana amesema wizi na uharibifu wa miundombinu ya shirika hilo una athari nyingi ikiwemo hasara kwa shirika na wananchi kukosa huduma.

Amesema licha ya kulazimika kutumia gharama ya mamilioni kufanya matengenezo, shirika hilo pia hupoteza mapato kwa wateja kukosa huduma.

‘’Kukosekana kwa huduma pia hukwamisha miradi na biashara zinazotegemea nishati ya umeme; hii inarejesha nyuma juhudi za wananchi kujikwamua kiuchumi,’’ amesema Ofisa huyo

Mwenyekiti wa Mtaa wa Sima ambako baadhi ya nyaya zinazoaminika kuwa za Tanesco zimekamatwa, Sekwa Joseph amewaomba wananchi kusaidia ulinzi wa miundombinu ya miradi ya maendeleo ikiwemo ya huduma ya umeme na maji katika maeneo yao.

Kiongozi huyo wa mtaa pia ameuomba uongozi wa Tanesco kuandaa na kutekeleza kampeni ya elimu kwa umma kuwezesha wananchi kushiriki ulinzi wa miumdombinu katika maeneo yao kwa kutoa taarifa pindi wanapoona dalili za hujuma.