TTB yawatoa hofu wakulima wanaodai makampuni ya ununuzi tumbaku

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku nchini Stan Mnozya (wakwanza kulia) akiwa na wakulima wa tumbaku katika moja ya masoko ya tumbaku mkoani Tabora. Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

Mkoa wa Tabora ndio unaoongoza kwa kuzalisha tumbaku nyingi nchini ambao unazalisha asilimia 60 ikiwa ni zao kuu la biashara na tegemeo kiuchumi.

Tabora. Bodi ya Tumbaku nchini (TTB) imewataka wakulima wa zao hilo wanaozidai kampuni za ununuzi wa tumbaku Sh46 bilioni kuvumilia ikidai muda wowote wataanza kulipwa.

Kilo milioni 122 za tumbaku zenye thamani ya zaidi ya Sh715 bilioni zimenunuliwa na makampuni ya tumbaku kiasi ambacho kimevunja rekodi katika historia ya tumbaku nchini.

Akizungumzia madeni hayo Septemba 22, 2023; Mkurugenzi Mkuu TTB, Stan Mnozya amesema makampuni ya Mkwawa na Voedsel yameendelea kulipa madeni kwa wakulima huku kiasi kilichobaki kikitarajia kulipwa muda wowote baada ya taratibu za kibenki kukamilika.

“Nawaomba wakulima ambao bado hawajalipwa kuwa na uvumilivu wakati jitihada zinafanywa na makampuni na Serikali ili walipwe fedha zao muda wowote kuanzia sasa,” amesema

Ameeleza kuwa kampuni ya Mkwawa ilikuwa inadaiwa Sh107 bilioni siku chache zilizopita na sasa imebaki inadaiwa Sh35 bilioni wakati kampuni ya Voedsel sasa imebakiza deni la Sh11 bilioni baada ya kuuza kilo milioni 10 zenye thamani ya Sh60 bilioni.

Kampuni ya Mkwawa ambayo inatajwa kununua tumbaku nyingi, ilinunua kilo milioni 42 zenye thamani ya zaidi ya Sh240 bilioni, tayari imelipa Sh212 bilioni na kuwa kampuni iliyolipa fedha nyingi zaidi kwa wakulima ikilinganishwa na kampuni zingine zote zilizonunua tumbaku zikiwemo za JTI na Alliance One ambazo tayari zimelipa wakulima.

Mnozya amepongeza jitihada zilizofanywa na Serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuzishawishi benki nne za Azania, NMB, NBC na CRDB kulipa madeni ya wakulima kutokana na changamoto ya uhaba wa Dola na kuwa kama sio jitihada hizo ingekuwa tatizo kubwa kwa malipo ya wakulima.

Mkulima wa tumbaku, Mwanaid Hussein ameipongeza Serikali kwa kuongeza makampuni zaidi ya ununuzi wa tumbaku na kuwa yeye na wanachama wenzake wa Zugimlole wamepata malipo yao yote kutika kampuni ya JTI.

“Tunashukuru tumepata malipo yetu mapema na sasa tunajiandaa na msimu mpya huku tukisubiri pembejeo,” amesema

Naye Haruna Kasele mkulima wa Kazaroho amesema wakulima kwenye eneo lao bado wanasubiri kwa hamu malipo ili pamoja na mambo mengine waanze maandalizi ya msimu mpya.

Mkoa wa Tabora ndio unaoongoza kwa kuzalisha tumbaku nyingi nchini ambapo asilimia 60 inazalishwa likiwa ni zao kuu la biashara na tegemeo kiuchumi.