Tulia aelezea mbinu zilizotumika kupata ushindi

Muktasari:

  • Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amerejea baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), nchini na kupokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine wa chama na Serikali huku akielezea nanma alivyopata ushindi huo.

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema uchaguzi wa kuwania urais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) uliokuwa mgumu lakini Rais Samia Suluhu Hassan aliweka nguvu kubwa kuupata ushindi huo.

 Dk Tulia ameyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 30, 2023 baada ya kurejea kutoka katika uchaguzi wa Rais wa IPU uliofanyika Luanda nchini Angola.

Dk Tulia ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM) alichaguliwa kuwa Rais wa 31 wa IPU baada ya kuwashinda wagombea kutoka Senegal Adjidiarra Kanoute aliyepata kura 59, Catherine Hara wa Malawi aliyepata kura 61 na Marwa Hagi kutoka Somalia aliambulia kura 11.

Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma, Dk Tulia amemshukuru Rais Samia kwa kumuunga mkono kuwania nafasi hiyo kwa kuwa ni lazima mgombea kupata ridhaa ya nchi yake katika kuwania nafasi hiyo.

“Lakini yeye (Rais Samia) amefanya kampeni kubwa sana, nchi kadhaa wakati wa kuja kupiga kura kule, walikuwa tayari na maelekezo kutoka nchi zao, sote kwa pamoja tumshukuru Rais kwa jambo kubwa kama hili,”amesema.

Amesema wagombea walitoka nchi tofauti hivyo haikuwa kazi rahisi kwa yeye kupata ushindi huo, Rais Samia alimsaidia kwasababu wako wabunge walifika wakisema kuwa Serikali zao zimewaomba kura na wamekuja na maelekezo.

“Ilibidi pia kuzunguka baadhi ya maeneo katika kutafuta hizi kura maana hii ni dunia nzima nchi 180 siyo kazi rahisi,”amesema.

Amewashukuru Watanzania kwa maombi yao na kwa kumtia moyo katika kuwania nafasi hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko amesema siri ya ushindi aliuupata unachangiwa na uwezo wa Dk Tulia katika kujieleza na kujibu maswali kwa ufasaha anapoulizwa.

“Pia ushindi huu unatokana na mabalozi mbalimbali waliokuja kuungana nasi, wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na timu kampeni yenyewe ukianza na wabunge wa IPU, baadaye wabunge wengine mahiri waliongezeka na kikubwa ni mahusiano chanya ndani ya Afrika na Duniani kote,”amesema.

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema Rais Samia amejipambanua kuwa ni kiongozi mahiri lakini pia ameonyesha kuwa anaungwa mkono na maraisi wengine duniani.

“Hata maraisi wanakuwa na interest (wanavutiwa) na nani anakuwa Rais wa Mabunge Duniani hiki nikielelezo cha ushirikiano mkubwa alio nao na marais wengine duniani, wanatambua uwezo wake udhubuti wake na uimara wake,”amesema.

Amesema ushindi huo ni kielelezo cha Tanzania ilivyotoa kipaumbele kwa vijana kwa kiasi kikubwa.

Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta amesema kuchaguliwa kwa Dk Tulia pamoja na kwamba ni sifa kwa Tanzania lakini pia ametoa moyo wa ushujaa kwa watoto wa kike nchini.

“Siyo rahisi, kwa hiyo mimi nampongeza sana watoto wa kike kwa kuona mfano wake, sasa nao wataiga kujitokeza na kuwa na moyo wa kujiamini kugombea nafasi kama hizi. Zaidi ya yote mimi nampongeza san asana,”amesema.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema  hawana  shaka kuwa Dk Tulia ni mbobezi katika masuala ya kibunge na nafasi yake ya kuwa Rais wa IPU haitamnyima nafasi ya kuendelea kuhudumu katika Bunge la Tanzania.

“Tunaamini kuwa atafanya kazi zote mbili kwa ustadi mkubwa, kwa uadilifu na uzalendo wa hali ya juu kwasababu anauelewa mkubwa, anaweledi mkubwa sana… Anauwezo wa kufanya kazi katika mabunge yote mawili katika sifa na heshima kubwa kabisa,”amesema.