Tume ya Madini yawanoa wachimbaji wadogo Mara

Muktasari:
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Henry Nditi amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa uelewa mdogo wa kanuni za uchimbaji salama ni miongoni mwa sababu zinazochangia ajali nyingi katika migodi kwa wachimbaji wadogo nchini.
Tarime. Serikali kupitia Tume ya Madini nchini imeanza kutekeleza kampeni ya mafunzo ya uchimbaji salama kwa wachimbaji wadogo ili kudhibiti matukio ya ajali migodini.
Akifungua mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo mkoani Mara leo Julai 21, 2023, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Henry Nditi amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa uelewa mdogo wa kanuni za uchimbaji salama ni miongoni mwa sababu zinazochangia ajali nyingi katika migodi kwa wachimbaji wadogo nchini.
"Uelewa mdogo miongoni mwa achimbaji husababisha matumizi yasiyo salama ya baruti, uharibifu wa mazingira na hata athari za kiafya katika maeneo ya migodi ya wachimbaji wadogo. Serikali itaendelea kutoa elimu ya uchimbaji salama ili kupunguza na hatimaye kumaliza tatizo la ajali maeneo ya migodini,’’ amesema Nditi
Amewaambia washiriki wa mafunzo hayo yanayofanyika eneo la Nyamongo wilayani Tarime kuwa Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa nchini yenye matukio kadhaa ya ajali za migodini ambapo kwa kipindi cha mwaka 2022/23, vifo viwili vimeripotiwa katika matukio matatu ya ajali mkoani humo.
‘’Kuanguka kwa kuta za migodi na wachimbaji kukosa hewa wawapo chini ya ardhi mgodini ni miongoni mwa sababu za ajali zinazoripotiwa katika migodi ya wachimbaji wadogo. Kila mtu lazima atimize wajibu kudhibiti ajali hizi,’’ amesema Kaimu Katibu huyo
Ameonya kuwa pamoja na kutoa elimu, Serikali haitasita kufungia migodi itakayothibitika kuhatarisha usalama na maisha ya wachimbaji huku akiwahimiza wamiliki kuzingatia kanuni za usalama na uhifadhi wa mazingira maeneo ya migodini.
Amesema makusanyo ya aduhuli ya Serikali kupitia Tume ya Madini katika sekta ya madini yanaongezeka huku akitolea mfano makusanyo ya zaidi ya Sh678.04 bilioni, sawa na asilimia 82.48 ya lengo la kukusanya Sh822.02 bilioni kwa kipindi cha kati ya Julai, 2022 hadi Juni, 2023.
"Mkoa wa Mara pekee ulikusanya Sh120.57 bilioni, sawa na asilimia 80.5 ya lengo lililokusudiwa katika kipindi hicho. Bado kuna fursa ya kupata mafanikio zaidi tukiboresha uchimbaji wetu, hasa wachimbaji wadogo,’’ amesema
Kaimu Ofisa Madini Mkoa wa Mara, Byarugaba Chakupewa amesema mapato kupitia sekta ya madini mkoani humo yameongezeka kutoka Sh109.36 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2022/21 hadi kufikia Sh120.57 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2022/23.
Mchimbaji mdogo, Rashid Bogomba ameishukuru Serikali kwa mafunzo hayo akisema yatasaidia siyo tu kuboresha shughuli zao, bali pia yataongeza tija katika sekta ya madini.
‘’Pamoja na mafunzo, tunaisihi Serikali kuhakikisha huduma muhimu za maji, umeme na miundombinu ya barabara siyo zinapatikana, bali pia zinaboreshwa mara kwa mara,’’ amesema Bogomba
John Marwa, mchimbaji mwingine mdogo eneo la Nyamongo ameiomba Serikali kupitia mamlaka husika kuwezesha wachimbaji wadogo kukidhi sifa za kupata mitaji kupitia mikopo nafuu kutoka taasisi za fedha.
‘’Utafiti wa kisayansi kujua maeneo yenye madini na kiwango kilichopo ni eneo lingine muhimu tunayoiomba Serikali kuwasaidia wachimbaji wadogo ili tuondokane na uchimbaji wa kubahatisha unaotugharimu mamilioni ya fedha bila tija,’’ amesema Marwa