Tume ya Tehama kuendeleza wabunifu nchini

Arusha. Serikali kupitia Tume ya Tehama imeanza kutekeleza mpango wa kukuza na kuendeleza wabunifu wa Tehama nchini kwa kuanzisha vituo kila mkoa ili kuwawezesha vijana kupata sehemu maalumu ya kuweza kuendeleza bunifu zao kwa njia ya Tehama.
Hayo yamesemwa leo Februari 28, 2023 jijini Arusha Katibu Tawala msaidizi uchumi na mzalishaji Mali mkoa wa Arusha, Daniel Loiruck wakati akizungumza katika mkutano wa wadau wa ubunifu katika Tehama uliowashirikisha vijana zaidi ya 150 kutoka mkoani Arusha.
Amesema kuwa, mkutano huo unalenga kujadili mashauriano na kubadilishana uzoefu katika kuanzisha na kuendesha shughuli za ubunifu kwa kutumia TEHAMA.
Loiruck amesema kuwa kitendo cha serikali kuanzisha programu za ubunifu katika Tehama inalenga kupanua wigo wa uzalishaji wa fursa za ajira hususani kwa vijana na kuongeza mchango wa Tehama katika pato la taifa.
"Tume ya Tehama wamenijulisha juu wa mpango wa kuanzisha vituo maalumu vya ubunifu katika Tehama kwa lengo la kuhamasisha vijana kujishughulisha na ubunifu kupitia Tehama ili kunufaika na fursa za kiuchumi zitokanazo na maendeleo ya TEHAMA yanayoendelea duniani hasa katika zama hizi za mapinduzi ya nne ya kiteknolojia yaani “4th Industrial Revolution” jambo ambalo ni nzuri na litawasaidia sana vijana wetu kupambana na changamoto ya ajira," amesema
Ameongeza kuwa, wataalamu wanasema kuwa katika mapinduzi haya ya nne ya kiteknolojia, maendeleo ya Tehama yatapelekea mfumo wa kiuchumi tuliouzoea (traditional economy) kuhamia katika uchumi unaoendeshwa na mifumo ya kielektroniki yaani “Platform Economy”.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama nchini, Dk Nkundwe Mwasaga amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Tehama imeona sasa ni vema kuanza kufungua fursa za kiuchumi kupitia Tehama ambapo utekelezaji wa mpango huu kwa kuanzia katika mikoa mitano ya Arusha, Dodoma, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza.
Aidha amesema kuwa hivi sasa wako katika hatua za awali za kukutana na wadau wa mikoa na kanda husika ili kufahamu mahitaji halisi, kupata maono ya wananchi husika na namna gani vituo hivi vya ubunifu vianzishwe ili wananchi wa mikoa na maeneo husika waweze kunufaika kiuchumi kupitia vituo vya ubunifu katika Tehama.
Ameongeza kuwa, uwepo wa vituo hivyo vitaweza kutatua changamoto mbalimbali za mkoa wa Arusha na kanda ya kaskazini kwa ujumla wake ili tuweze kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi na kijamii, na hatimaye kuchangia katika maendeleo ya taifa kwa ujumla.
"Kupitia mpango huu utapelekea kuongeza kiwango cha uanzishwaji wa kampuni changa za Tehama (ICT Startups) kwani mpango unalenga zaidi vijana waliomaliza vyuo na walioko vyuoni na hata waliopo mtaani pia ili waweze kupata sehemu yao maalumu ya kufanyia maswala yao ya ubunifu" amesema.
Ofisa Tehama mkoa wa Arusha ,David Nyangaka amesema kupitia programu hiyo vijana wabunifu wa mkoa wa Arusha watanufaika kwa kiwango kikubwa sana kwani walikuwa hawana mahala tulivu pa kufanya bunifu zao na kuweza kuzitangaza kimataifa kupitia Tehama.