Tunasherehekea Krismasi na ujumbe wa amani au siasa?

Tunasherehekea Krismasi na ujumbe wa amani au siasa?

Muktasari:

Tunapoelekea kusherehekea sikukuu inawagusa Watanzania wengi wakiwamo wazee, vijana na watoto ambayo ni siku ya kuzaliwa Yesu Kristu wa Nazareti, ni muhimu kutafakari ujumbe tunaoupata kutokana na sikukuu hii.

Tunapoelekea kusherehekea sikukuu inawagusa Watanzania wengi wakiwamo wazee, vijana na watoto ambayo ni siku ya kuzaliwa Yesu Kristu wa Nazareti, ni muhimu kutafakari ujumbe tunaoupata kutokana na sikukuu hii.

Wahuubiri wetu wanaojumuisha maaskofu, mapadre au manabii wamejiandaa kutuletea ujumbe murua wa Krismasi. Suala la msingi kujiuliza ujumbe huo utakuwa wa imani au wa kisiasa.

Kazi ya nabii ni kuhubiri wakati unaofaa na usiofaa. Nabii hapangiwi cha kufundisha waumini wake. Yeye anatumwa na Mwenyezi Mungu.

Wapo viongozi wanaofundisha bila kuogopa, wanakosoa na kuonya, wanaohimiza haki, wema na huruma. Wengine wanaogopa kujitokeza hivyo kujificha kwenye sikukuu kama hizi kutoa ujumbe wenye utata au usioeleweka vizuri.

Wanaogopa kuitwa wapinzani au wasaliti kama si vibaraka wa mabeberu. Badala ya kutoa ujumbe wa imani na wa kinabii wanaishia kuhubiri siasa.

Wengine wanafikiri viongozi wa dini wanajiingiza kwenye siasa. Lakini, tujiulize, kuhubiri maisha ya kiroho ndani ya jamii ni kuhubiri siasa?

Kuna wanaofikiri viongozi wa dini nchini wamekaa kimya sana, wanaogopa kusema na wananajipendekeza kwa watawala. Ukichukulia mifano kama ya akina Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini na maaskofu wa Latin Amerika waliokufa wakitetea wanyonge na maskini, wanaona viongozi wa dini hapa kwetu bado wako kimya.

Kwa upande mwingine, kuna ambao wana maoni kwamba Yesu wa Nazareti hakujishughulisha na mambo ya kisiasa. Hakuwachochea watu kugoma bali aliwahimiza kulipa kodi kwa Warumi.

Kwamba yeye alisisitiza ufalme wa kiroho hivyo akataka ya Kaizari yaende kwa Kaizari. Mafundisho yake yalikuwa ya kiroho na mashitaka ya kisiasa juu yake yalipikwa na Wayahudi waliomchukia.

Hata hivyo, ukweli wa Yesu haukujikita kwenye maoni ya pande hizi tofauti. Kuna ukweli kwamba Wayahudi hawakutofautisha siasa na dini.

Kile tunachokiita siasa, masuala ya kijamii, uchumi na dini, kwao ilijulikana kama Mungu na sheria. Hakuna kitu chochote katika jamii ya Wayahudi kilichojitegemea bila kuegemea kwa Mungu na sheria.

Mungu aliyaongoza maisha yao, aliwalisha, aliwanywesha, aliwalaza na kuwaamsha hata kuwahamisha kutoka nchi moja hadi nyingine na akawapa nchi nzuri yenye maziwa na asali.

Hakutaka wawe na uhusiano na Miungu wengi au wafanye mambo yasiyompendeza. Hivyo siasa tunayoifahamu leo haikuwapo katika maisha ya Wayahudi. Ndio maana walipigana kufa na kupona kuuondoa utawala wa Warumi uliokuwa ukitenga siasa na dini.

Yesu alitaka kuikomboa Israeli kutokana na utawala unaotenga dini na siasa. Yeye alikuwa na maoni tofauti na wengine. Aliamini ukombozi ungewezekana kama Israeli ingebadilika kutoka rohoni.

Ni lazima kutenda wema, haki na huruma. Bila hivyo hata kama wangefanikiwa kuwapindua na kuwafukuza Warumi, watawala wa Kiyahudi wasingekuwa tofauti.

Yesu alionyesha wazi maisha ya kitabaka yaliyokuwapo miongoni mwa Wayahudi yalikuwa ni ya kiunyanyasaji zaidi ya utawala wa Kirumi. Hivyo la msingi si kubadilisha utawala bali roho za watu kwani kama sivyo hakuna ukombozi wa kweli.

Hapa ndipo kwenye somo hata kwa Tanzania. Watu na wanasiasa wamekuwa na shauku ya kubadilisha utawala kutoka CCM kwenda vyama vingine ili kuleta mabadiliko katika utendaji na kupambana na rushwa na ufisadi.

Maaskofu wanafikiri elimu ya uraia inaweza kusaidia kupambana na rushwa na ufisadi. Kama ilivyokuwa wakati wa Yesu, hata sisi mabadiliko yetu hayawezi kuleta matunda mema, kama hakuna mabadiliko kutoka rohoni.

Ni lazima Tanzania ibadilike kutoka rohoni. Ijenge mifumo ya kuhimiza wema, haki na huruma. Kinyume na hapo, vyama vingine vitatenda kama CCM.

Hoja ya msingi aliyoishughulikia Yesu ni unyanyasaji. Aliguswa zaidi na unyanyasaji uliokuwa ukiendelea miongoni mwa Wayahudi. Aliguswa na umaskini, magonjwa, njaa na ubaguzi wa kupindukia. Hakuangalia kama anayesababisha hayo yote ni Mrumi au Myahudi. Aliuchukia uovu.


Waliopinga utawala wa Warumi na kuendeleza unyanyasaji na ubaguzi kwa Wayahudi hawakuwa na tofauti na Warumi. Hivyo Yesu alibadilisha mwelekeo wa mapambano kutoka kupinga utawala wa Warumi na kutetea maskini.

Ukombozi wa kweli, kama alivyoonyesha Yesu, ni kuuthamini ubinadamu. Kumpenda adui ni msimamo wa kuthamini mshikamano wa binadamu wote. Huu ndio ujumbe tunaoutegemea kwenye Sikukuu ya Krismasi.

Nawatakia baraka za Krismasi na Mwaka Mpya wenye mafanikio na matumaini.

Hoja za Karugendo