Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tundu Lissu aibua mapya, ataka apelekwe Dodoma

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu akiwa mahakamani.

Muktasari:

  • Mawakili wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu anayeshikiliwa katika mahabausu ya Gereza la Ukonga, Dar es Salaam, kutokana na kukabiliwa na kesi ya uhahini wamefungua kesi ya kikatiba kupinga kuzuiwa kumuona Lissu mahabusu.



Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameiomba Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma iamuru apelekwe Dodoma kwa ajili ya kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na mawakili wake wakipinga kuzuiwa kuonana naye na au kujadiliana naye faragha.

Lissu ametoa ombi hilo leo Jumanne, Mei 5, 2026, wakati kesi hiyo inayosikilizwa Dodoma na jopo la majaji watatu, Amir Mruma (kiongozi wa jopo), Dk Angelo Rumisha na Dk Everist Longopa, ilipotajwa, ambapo pamoja na mambo mengine mahakama imepanga kusikiliza pingamizi la awali.

Kesi hiyo ya Kikatiba namba namba 7300/2026 imefunguliwa na mawakili watatu, Kulwa Maduhu, Nashon Nkungu na Paul Kisabo, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kamishna Mkuu wa Magereza (CGP), Mkuu wa Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam na Lissu mwenyewe.

Katika kesi hiyo, mawakili hao wakipinga vikwazo wanavyowekewa na Mkuu wa Gereza la Ukonga, kila wanapokwenda gerezani kuzungumza na mteja wao, Lissu anayehifadhiwa katika mahabusu ya gereza hilo kutokana na kesi ya uhaini inayomkabili. 

Hata hivyo, AG ameibua pingamizi la awali akidai kesi hiyo ni batili, kwa kuwa wadaiwa wana njia mbadala za kupata nafuu (wanazoziomba) na hivyo inakiuka kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (BRADEA).

Kesi hiyo imetajwa kwa mara ya pili leo Jumanne, Mei 5, 2026 kwa njia ya mtandao (video conference) ambapo Lissu ameshiriki kwa njia hiyo kutoka gerezani Ukonga, mahakama imependekeza kusikiliza pingamizi hilo pamoja na shauri la msingi kwa njia ya maandishi.

Ingawa mawakili wa wadai, John Seka na Ferdnand Makore wamekubaliana na pendekezo hilo, lakini Lissu amelipinga akiomba shauri hilo lisikilizwe kwa mdomo na akaomba mahakama iamuru siku ya usikilizwaji wa kesi hiyo apelekewe mahakamani Dodoma asikilizwe ana kwa ana.

Lissu amedai ikiwa kesi hiyo itasikilizwa kwa njia maandishi atakosa haki ya kusikilizwa kikamilifu chini ya Ibara ya 13(6) (a) ya Katiba, akifafanua kwa mazingira aliyomo (mahabusu) hawezi kujiandaa vizuri kumwezesha kusikilizwa kwa haki na usawa katika kesi hiyo.

“Waheshimiwa majaji, katika mazingira niliyomo huko mahabusu sina access ya maktaba wala internet (sina fursa ya maktaba na mtandao) kwa ajili ya kufanya research (utafiti/ kwa hoja za kisheria) kujiandaa kwa ajili ya usikilizwaji kamili, wala sipati huduma ya mawakili,” amesema Lissu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Stanley Kalokola amepinga vikali maombi hayo ya Lissu akidai kukisilizwa kikamilifu si lazima mpaka aende Dodoma kusikilizwa mdomo bali hata kwa maandishi akidai ameweza kuyajibu madai kwa maandishi vizuri huku akiambatanisha nyaraka nyingi sana.

Pia wakili Kalokola amedai suala la kuamuru apelekwe Dodoma linaweza kuwa na changamoto katika masuala ya usafiri na kwamba hata sheria yenyewe inatoa fursa ya usikilizwaji wa mashauri hayo kwa njia ya maandishi.

Vilevile Wakili Kalokola amedai Lissu anakabiliwa na kesi nyingine Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu Dar es Salaam na kwamba hivyo uamuzi wa yeye kwenda kusikilizwa kwa mdomo Dodoma unaweza kuvuruga utataratibu wa usikilizwaji wa kesi hizo nyingine zikiitwa akiwa huko.

Kwa upande wake, wakili Seka amedai hoja ya Lissu kuhusu kujiandaa ni ya msingi  katika kujiandaa kuwasilisha hoja za haki zake na kwamba kama anaona atakuwa na haki ya kusikilkizwa akiwa Dodoma wao ni nani mpaka wapinge.

“Wakili Kalokola amezungumzia suala la logistici mpaka nikaanza kujiuliza kama naye amekuwa afisa wa Magereza. Akija Dodoma sidhani kama atalala hotelini bali katika magereza yaliyoko hapa,” amesema wakili Seka na kusisitiza kuwa Lissu hatakuwa mahabusu wa kwanza kusafirishwa nje ya mkoa kwa ajili ya kesi.

Wakili Makore kwa upande wake pamoja na mambo mengine amesema kuwa hakuna sababu yoyote iliyotolewa inayoweza kuzuia haki ya kikatiba ya kusikilizwa chini ya ibara ya 13(6) (a).

Akijibu hoaj za wakili Kalokola, Lissu amesema kuwa hakuna sababu za kisheria zilizotolewa na wakili Kalokola.

Amesema kuwa ni suala la kisheria na kanuni ya jumla kwamba mashauri ya haki za binadamu yanatakiwa kusikilizwa kwa mdomo hususan katika hatua ya mapingamizi kwa mujibu kifungu cha 11 (2) cha Sheria ya Utekelezaji Haki na Wajibu wa Msingi (BRADE).

Pia amerejea kanuni 9(1) ya Kanuni za Mwenendo na Utaratibu wa Mashauri hayo katika hatua ya pingamizi yanapaswa kusikilizwa kwa mdomo.

Lissu amesema kuwa ingawa kanuni ya 13 inatoa fursa ya kusikiliza shauri la msingi kwa maandishi lakini akasema kuwa kwa kuwa kanuni hiyo inakinzana na Sheria Mama basi hakiwezi kuwa juu ya Sheria Mama.

“Kwa hiyo kisheria mashauri haya yanatakiwa yasikilizwe kwa mdomo kwa sababu hizo za kisheria nilizozisema,” amesisitiza Lissu.

Kuhusu changamoto ya usafiri Lissu amesema kuwa si hoja ya msingi akisisitiza Mahakama ikiamuru kesi hiyo isikilizwe kwa mdomo hawatakuwa na namna ya uchaguzi isipokuwa kutekeleza amri hiyo.

Kuhusu hoja ya kuvuruga kesi zake nyingine zinazomkabili Dar es Salaam, Lissu  amesema kuwa kwa uzoefu usikilizwaji wa pingamizi kama hilo hauwezi kuchukua mwezi, wiki wala siku bali ni muda wa saa kadhaa tu huku kesi ya msingi pia akisema kuwa nayo haiwezi kuchukua hata siku tatu.

Lissu amehoji kuwa wakili wa Serikali anajuaje shauri la mapiti (lililofunguliwa Mahakama ya Rufani na Jamhuridi dhidi yake Lissu katika kesi ya uhaini) litasikiliza Dar es Salaam badala ya Dodoma iliko Mahakama ya Rufani.

Kuhusu hoja majibu yake ya maandishi dhidi ya madai na kuambatanisha nyaraka nyingi, Lissu amesema kuwa wakili huyo wa Serikali alipaswa kwanza amuulize yeye mwenyewe kuwa alizipataje na kwa magumu kiasi gani.

“Mimi ndiye najua viatu ninavyoviaa, machungu ya kujitetea katika mazingira niliko. Nimesema katika mazingira niliko, kujitetea kwa maandishi itakuwa ngumu sana kwangu kwa sababu nilizoeleza, sina maktaba sina internet na mawakili wangu wanazuiwa kufanya kazi yao ndio maana tumekuja mahakamani,” amesisitiza Lissu.

Pia Lissu amepinga pendekezo la Serikali njia mbadala, wengine kusikilizwa kwa maandishi na yeye asikilizwe kwa mtandao akidai kuwa hata utaratibu wa mtandao  haupo kwenye wala kwenye kanuni ndio maana hazijasema wazi.

Hata hivyo Wakili Kaloloka amedai kuwa kanuni ya 19 inatoa mazingira ya kutumia Kanuni za Mahakama Kuu kama kuna jambo ambalo haliko katika Kanuni za Mahakama ya Rufani.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote imeahirisha kesi hiyo mpaka Mei 21, 2026 itakapotoa uamuzi wa maombi hayo ya Lissu.

Wadai wanajitambulisha kuwa washauri wa kisheria wa Lissu, wanalalamikia matendo ya mdaiwa wa tatu (Mkuu wa Gereza Ukonga) kushindwa kutekeleza kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza inayotoa haki ya washauri wa kisheria kufanya mashauriano ya siri na wateja wao bila kuingiliwa.

Maduhu anadai kuwa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakizuiliwa na maofisa magerereza kukutana na kushauriana na Lissu au kumpelekea nyaraka muhimu zinazohusiana na kesi inayomkabili, huku Mkuu wa Gereza akidai kuwa ni maelekezo ya Kamishna Mkuu wa Magereza.

Kwa upande wao Nkungu na Kisabo licha ya kupata fursa ya kuzungumza na kujadiliana na Lissu masuala ya kisheria, lakini wamekuwa hawana faragha kwani maofisa magereza wamekuwa wakisimama umbali wanaoweza kusikia kila kitu wanachojadiliana.

Pamoja na nafuu nyingine wanaiomba mahakama itamke kuwa maofisa magereza kusikiliza mazungumzao yao na mteja wao Lissu ni kinyume cha kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza, Sheria na Katiba kuhusu haki ya kusikilizwa kwa usawa na faragha na wapewe fursa ya faragha na mteja wao.