Ubalozi wa Ufaransa kuleta neema kampuni changa nchini
Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Nabil Hajalaoui (wa kwanza kushoto) akifafanua jambo kwa ujumbe wa watu 12 walipomtembelea nyumbani kwake jijini Dar es Salaam kuelezea safari yao.
Muktasari:
- Ubalozi wa Ufaransa nchini umejitosa kuleta wawekezaji kuwekezaji kwenye ubunifu na teknolojia katika kampuni changa nchini ili kuziba pengo lilopo katika uanzishwaji wa miradi.
Dar es Salaam. Ubalozi wa Ufaransa umeonyesha nia ya kusaidia kuanzishwa kwa mtandao wa wawekezaji wa malaika kwenye kampuni changa za ubunifu wa teknolojia ya kidijitali nchini kukabiliana na upungufu wa mitaji miongoni mwa kampuni hizo.
Ili kufanikisha hilo, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Nabil Hajlaoui, amesema kwamba atazungumza na Chama cha Biashara cha Tanzania na Ufaransa (FTCC) kupanga mkutano maalum kwa ajili hiyo.
Balozi Hajlaoui alikuwa akizungumza na ujumbe wa watu 12 uliozuru nchini Ufaransa hivi karibuni kupitia mradi wa Innoversity ulipoenda kumtembelea nyumbani kwake mjini Dar es Salaam hivi wiki hii.
“Tutawasiliana na Chama cha Wafanyabiashara wa Ufaransa na Tanzania (FTCC) na kupanga mkutano maalum na wawekezaji wenye uzoefu wa kufadhili miradi na hivyo kuzisaidia kampuni changa za Tanzania,” amesema.
Naye Ofisa Mkuu wa Operesheni wa Sahara Ventures (COO), Musa Kamata amesema kwa sasa wanajifunza jinsi ya kutumia vyema mfumo na uzoefu wa mtandao wa wawekezaji wa malaika wa Ufaransa ili waweze kuanzisha mtandao kama huo nchini ili kuleta fursa zaidi na ufadhili wa kuanzisha biashara za ndani.
"Kwa kuwa sote tunaelewa kuwa hatuna mitaji madhubuti ya ubia nchini na kutumia njia zao inaweza kuwa fursa nzuri ya kuanzisha kitu kama hicho na kwenda zaidi ya ushauri na kuanza kutoa ufadhili kwa wanaoanzisha," amesema.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sahara Ventures (CEO), Jumanne Mtambalike, ambaye pia alikuwa sehemu ya ujumbe wa watu 12 waliotembelea ubalozi huo amesema kuwa kuna uhaba wa wawekezaji kwenye kampuni changa za ubunifu wa kidijitali nchini ni jambo linalosababisha kutokuwepo uwekezaji zaidi kutoka taasisi na kimataifa.
“Hakuna wawekezaji wa ndani wanaoonyesha nia ya kuingiza fedha katika kuanzisha biashara, hivyo badala ya kuwa na mtandao wa washauri, lengo letu ni ya kuanzisha mtandao wa washauri na wawekezaji ambao watatoa pesa za awali za kuendesha kampuni changa ili kuwapa imani wawekezaji wakubwa wa kimataifa na kikanda,” alisema.
Ujumbe huo ulijumuisha watu watatu kutoka Sahara Ventures, kutoka vyuo vilivyonufaika na wanafunzi sita, wawili kila mmoja, kutoka vyuo ambao waliushukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa kupewa fursa ya kuwa sehemu ya programu hiyo.
Mradi wa Innoversity ni mradi wa miaka miwili unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania kwa thamani ya Sh1.4 bilioni na unatekelezwa na Sahara Ventures. Vyuo vikuu vitatu vinanufaika na mradi huo ambavyo ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (Arusha) na Chuo Kikuu cha Iringa.