Ubovu wa barabara Dar bado 'fupa gumu'

Magari yakipita kwa tabu katika eneo la Barabara ya Kitunda kwenda Banana, eneo hili limeathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha jambo ambalo limekuwa likisababisha foleni kwa watumiaji wa barabara hiyo. Picha na Aurea Simtowe

Muktasari:

  • Wakati kilio cha mvua kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara kikisikika katika maeneo mbalimbali hususani ndani ya jiji la Dar es Salaam, Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wafunguka.

Dar es Salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, zimeongeza ubovu wa miundombinu ikiwemo barabara, jambo ambalo limewafanya watumiaji na wamiliki wa vyombo vya moto kupaza sauti zao.

Baadhi wameomba hatua za haraka kuchukuliwa katika maeneo korofi ili kuwaondolea adha wanazokutana nazo wanapotumia miundombinu hiyo.


Waendesha pikipiki wakifikiria jinsi ya kuvuka eneo mojawapo kati ya yale korofi kwenye barabara ya Banana-Kitunda Wilaya ya Ilala jana. Barabara hiyo imekuwa kero kwa muda mrefu. Picha na Aurea Simtowe

Wakati wao wakiyasema hayo, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) imebainisha mikakati yake huku Kamati ya Kudumu ya Bunge Miundombinu ikisema Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) pekee inahitaji ya Sh2 trilioni ili kuweka mambo sawa.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti leo Alhamisi, Aprili 11, 2024 wakazi wa jijini Dar es Salaam wameitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha barabara zote zinapitika kwa urahisi mvua zinaponyesha, ili kuwaondolea adha wanazokutana nazo kipindi hiki cha masika.

Mkazi wa Kitunda, James Zacharia ameelezea namna walivyosota kwa saa tatu barabarani katika sehemu ambayo wanaweza kutumia chini ya dakika 20.

“Hii barabara inayokwenda Kitunda kutoka Banana ina shimo kubwa, mvua ikinyesha magari kupita ni mtihani, yanatumia muda mwingi na taratibu kila mtu akiangalia usalama wa chombo chake,” amesema Zacharia.

Amesema hali hiyo iliwafanya kutumia saa 3 siku ya Jumanne usiku wakiwa katika magari jambo ambalo si la kawaida.

“Barabara ni mbaya, ukitaka kutoka nyumbani na gari sasa hivi unawaza mvua ikinyesha itakuwaje lakini pia unawaza ukiacha gari mvua ikinyesha itakuwaje maana usafiri unasumbua,” amesema Zacharia.

Alichokisema Zacharia kiliungwa mkono na Nancy Nzigu ambaye anasimulia namna walivyolazimika kutembea kutoka Banana hadi Kitunda kutokana na kukosa usafiri.

“Ni kama magari yalikwama katika foleni, yakawa hayafiki Banana, tumekaa zaidi ya saa tukisubiri gari bila mafanikio ndipo tuliamua kutembea polepole kama kikundi na kufika nyumbani,” amesema Nzigu.

Kilio kilichopo katika eneo hilo kinafanana na kile kilichopo kwa wakazi wa Msumi, ambao wameendelea kuikumbusha Serikali kwa ajili ya kuwajengea daraja linalounganisha eneo hilo la Madale.

Daraja hilo lilibebwa na maji ya mvua mwishoni mwa Januari mwaka huu na kukata mawasiliano ya pande hizo mbili, huku Tarura ikijenga kivuko cha waenda kwa miguu na pikipiki ikidai kusubiri utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP),  utakaojenga barabara hiyo.

Kupitia utafiti mdogo uliofanywa na Mwananchi, maeneo mengine ambayo barabara zimeharibika ndani ya jiji hili ni Bomba mbili, Mwanagati, Kibeberu, Pugu, Kibamba huku sauti zikipazwa maeneo tofauti kuhitaji hatua za haraka.

Mtendaji Mkuu wa Tarura, Victor Seif amesema mpaka sasa wameshatumia zaidi ya Sh51 bilioni kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara katika maeneo mbalimbali, tangu mvua zilipoanza kunyesha.

“Lakini watu wangu wako kila mahali wanafanya tathmini kile kinachoweza kufanyika haraka ili kuweka urahisi wa kutumika kwa barabara, changamoto ni kuwa mvua inaponyesha kazi nyingi haziwezi kufanyika,” amesema Seif.

Amesema kutokana na mvua nguvu kubwa imewekwa katika tathmini ili zitakapokoma kazi ifanyike.


Waendesha pikipiki wakipita kwa taabu katika barabara ya Banana-Kitunda, karibu na Kituo kidogo cha Polisi Kitunda jana. Maeneo mengine korofi ni Savanna na Matembele ya Kwanza. Picha na Aurea Simtowe.


Katika upande wa barabara kuu, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta amesema wamekuwa wakitumia utabiri wa TMA kufanya tathmini ya maeneo yanayoweza kuathiriwa na mvua, na kuondoa vitu vinavyoweza kuwa sababu.

 “Ili kufanya utatuzi wa haraka kupatikana tumewatambua wakandarasi ambao tunafanya nao kazi kwa karibu mara tatizo linapotokea bila ya kuingia katika mchakato,” amesema Mohamed.

Amesema kutambuliwa kwao kumewafanya kujua majukumu yao pindi dharura inapotokea na kuchukua hatua za haraka.

Amefafanua katika bajeti, Tanroad ilitengewa Sh20 bilioni kama fedha ya dharura lakini alibainisha kuwa ili kuweka mambo sawa zinahitajika  walau Sh280 bilioni.

“Fedha ambazo tunazihitaji walau kurejesha mawasiliano vizuri ni angalau Sh280 bilioni na inaweza kufika hadi Sh300 bilioni," amesema Mohamed.

Wakati haya yakielezwa, wananchi walihoji juu ya kazi inayofanywa na Sh100 inayokatwa katika lita ya mafuta iliyopitishwa na Bunge la Tanzania, kwa kile walichobainisha kuwa wakati huu ndiyo kazi yake ingeonekana.

“Ukinunua mafuta unakatwa Sh100, inaenda wapi, mbona hatuoni kazi yake, kama vipi iondolewe,” amesema Steven Ngonyani mkazi wa Mbezi.

Wakati yeye akiyasema hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Suleiman Kakoso amesema uwepo wa Sh100 katika kila lita ya mafuta umesaidia kufungua baadhi ya maeneo, licha ya kuwa kiasi kinachokusanywa ni kidogo kuliko mahitaji.

“Mahitaji ni makubwa sana katika ujenzi wa barabara ndiyo maana kama kamati tulishauri kuongeza fedha ili mfuko wa barabara uweze kufanya kazi kikamilifu,” amesema Kakoso.

Akitolea mfano wa mahitaji amesema Tanroads pekee inahitaji zaidi ya Sh2 trilioni ili kuweza kukabiliana na hali halisi ya uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mvua.

“Sh100 ikitoka kutakuwa na shida kubwa, kinachopaswa kufanywa ni Serikali kuongeza fedha zaidi, kwani kuna barabara nyingi  zinahitaji matengenezo,” amesema Kakoso.

Akitolea mfano wa baadhi ya barabara zinazohitaji matengenezo makubwa ni ile ya Dar es Salaam kwenda Mtwara, Dodoma kwenda Iringa, Singida – Nzega, Nzega-Mwanza na Makambako – Songea.