Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAGUZI CCM 2015: Dk Hussein Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Muktasari:

Dk Mwinyi alianza safari yake ya elimu ya Msingi jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1972 – 1976, Shule ya Msingi Oysterbay. Kati ya mwaka 1984–1985 wazazi wake walimhamishia Misri na akasoma katika Shule ya Msingi “Manor House Junior” ambako alihitimu elimu ya msingi. Shule hii ilikuwa na hadhi ya “Middle School za Tanzania” kwa wakati huo. Mwinyi alipelekwa Misri kwa sababu baba yake, Ali Hassan Mwinyi, alikuwa balozi wa Tanzania nchini Misri wakati huo.

Historia yake

Dk Hussein Mwinyi alizaliwa Desemba 23, 1966 huko Unguja, Zanzibar (Desemba mwaka huu atatimiza miaka 49). Dk Mwinyi ni mtoto wa Mzee Ali Hassan Mwinyi (Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na mama Sitti Mwinyi. Kwa sasa Dk Mwinyi ni Mbunge wa Kwahani Zanzibar na ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk Mwinyi alianza safari yake ya elimu ya Msingi jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1972 – 1976, Shule ya Msingi Oysterbay. Kati ya mwaka 1984–1985 wazazi wake walimhamishia Misri na akasoma katika Shule ya Msingi “Manor House Junior” ambako alihitimu elimu ya msingi. Shule hii ilikuwa na hadhi ya “Middle School za Tanzania” kwa wakati huo. Mwinyi alipelekwa Misri kwa sababu baba yake, Ali Hassan Mwinyi, alikuwa balozi wa Tanzania nchini Misri wakati huo.

Aliporejea Tanzania, alipelekwa Shule ya Sekondari Azania na kuendelea na masomo ya kidato cha I – IV mwaka 1982 – 1984. Alipohitimu kidato cha nne alipelekwa Shule ya Sekondari Tambaza kusoma kidato cha tano peke yake mwaka 1984 -1985.

Dk Mwinyi tangu zamani ni mtu wa kupenda kusaidia watu, aliomba na kuchaguliwa kusomea utabibu wa binadamu. Alianza masomo ya udaktari nchini Uturuki mwaka 1985 kwenye Shule ya Utabibu ya Chuo Kikuu cha Marmara na kuhitimu Shahada ya Utabibu wa Binadamu mwaka 1992.

Kwa sababu hakumaliza kidato cha VI, alipokuwa huko ughaibuni alipitia masomo ya mwaka mmoja ya kujiandaa na udahili wa Chuo Kikuu “Pre University Studies”. Chuo cha Marmara kinapokea hata wanafunzi wa kidato cha nne kuanza kusomea shahada ya utabibu lakini lazima wapitie mwaka mmoja wa maandalizi kama alivyofanya Mwinyi.

Alipohitimu shahada ya kwanza alirejea Tanzania na kufanya kazi kwa mwaka mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Mwaka 1993, Mwinyi aliendelea na masomo ya juu ya utabibu kwa kuunganisha, safari hii akipelekwa Uingereza katika Hospitali ya Hammersmith ambako alihitimu shahada ya uzamili ya utabibu mwaka 1994 na kuunganisha shahada ya uzamivu ya udaktari hapohapo Hammersmith na kuhitimu mwaka 1997.

Alirejea nchini kwa mara nyingine na kufanya kazi katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Herbert Kairuki (HKMU) kwa miaka miwili hadi mwaka 1999.

Mwaka 2000, Dk Mwinyi alizidisha nguvu yake ndani ya CCM kwa kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), akashinda na mwaka 2007 aligombea tena NEC na kushinda na tangu wakati uo aliteuliwa kuingia kwenye Kamati Kuu ya CCM hadi leo hii.

Dk Mwinyi amemuoa Mariam Herman na wana watoto wanne; Ibrahim, Jamila, Tariq na Sitti.

Mbio za ubunge

Dk Mwinyi alijitosa kwenye siasa mwaka 1999 akiliwania Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani (Bara) na kushinda. Alipokuwa mbunge, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, alikaa katika wadhifa huo hadi mwaka 2005.

Dk Mwinyi alijitosa tena jimboni mwaka 2005, lakini safari hii siyo Mkuranga! Aliombwa akagombee nyumbani kwao Zanzibar, Jimbo la Kwahani, alipambana na wagombea sita kutoka vyama vingine. Kwa sababu jimbo hili ni ngome ya CCM, alishinda kirahisi kwa kupata kura 6,239 (asilimia 85.6) akifuatiwa na Mussa Haji Khamis wa CUF aliyeambulia kura 921 (asilimia 12.6).

Safari hii ilikuwa ni Serikali ya Awamu ya Nne chini ya uongozi wa Jakaya Kikwete na Dk Mwinyi aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais na alidumu hadi mwaka 2008 alipopelekwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alikokaa hadi mwaka 2010.

Aliporejea tena Kwahani mwaka 2010 kusaka ubunge, akakumbana na yuleyule hasimu wake wa mwaka 2005, Haji wa CUF, mara hii vyama vingine havikuweka wagombea na Dk Mwinyi hakupata shida kushinda kwa kura 5,277 (asilimia 83.0) dhidi ya kura 1,085 (asilimia 17.0) za CUF.

Awamu ya pili ya Rais Kikwete ikampa tena Wizara ya Ulinzi kabla ya kumpeleka Wizara ya Afya tena mwaka 2012 na miezi 19 baadaye (yaani Januari, 2014) akarejeshwa tena Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambako ndipo anahudumu hadi leo.

Mbio za urais

Dk Mwinyi hajawatangazia Watanzania nia yake ya kutaka kwenda Ikulu, ila ni mmoja wa wanasiasa ambao wanazungumziwa, kutajwa na kuhisiwa kwamba huenda ni mmoja wa watarajiwa.

Mwenyewe haoni kama jambo hilo ni baya na hakatai au hakubali ikiwa nia hiyo ipo au haipo, anachosisitiza ni kuwa hivi sasa ameelekeza nguvu na akili zake kusimamia wizara aliyopewa na mambo mengine ni majaliwa ya ‘Mungu’ peke yake.

Nguvu yake

Moja ya jambo linalompa Mwinyi nguvu ikiwa atachukua fomu na kuanza kufikiriwa ndani ya CCM ni “kugusa umande vya kutosha”. Mwinyi hakusoma kwa kubahatisha, amesoma bila mikwamo na kupata elimu ambayo kiongozi yeyote duniani analazimika kuwa nayo ili kuongeza ufahamu na ufanisi.

Bahati nzuri, Mwinyi amesomea masuala ‘adhimu’, utabibu wa binadamu. Aina hii ya taaluma inayomfanya mtu awe karibu na watu wenye matatizo makubwa, inaweza kuwa imemuongezea hali ya kujali, kuwajibika na kuwaonea huruma watu wengine, hili ni jambo la kwanza.

Pili, Mwinyi bado ni kijana na kumekuwa na kelele nyingi katika vyama vyote vikubwa hapa nchini kuwa nchi inakoelekea hata kama si uchaguzi huu, lazima kuanza kufikiri kuwakabidhi nchi watu wa kizazi cha hivi karibuni kuliko kushupalia wazee waliotumikia Taifa miaka nenda, miaka rudi.

Mwinyi anakuwa mmoja wa vijana muhimu na watulivu huku mara nyingi akionyesha kama ni mtu mwenye busara kulinganisha na vijana wengine ndani ya CCM. Yeye si mtu wa kupenda umaarufu na kujikweza, ni kijana wa kawaida na dhana hii ya vijana wa kisasa pia inambeba.

Udhaifu wake

Moja ya jambo ambalo linafahamika kuwa limezidi kwa Mwinyi ni upole uliopitiliza. Pamoja na kuwa na busara, lakini upole umemzidia. Watendaji niliozungumza nao katika wizara alizopita wanasema ni kiongozi “mpole mno”.

Kwa maoni yangu na kwa namna ninavyomfahamu na kumuona akiwajibika wizarani, bungeni na kwingineko, upole alio nao si salama kwa Taifa. Tanzania kwa sasa inahitaji Rais atakayekuwa “mkali kama pilipili” kila mambo ya upuuzi yatakapotaka kujiri na “mpole” kwa wakati muafaka, huenda udhaifu huu wa Dk Mwinyi na unaweza kumuathiri kwa safari yake.

Pia, Mwinyi anatajwa kama kiongozi ambaye hufanya uamuzi taratibu hata katika mazingira yanayohitaji “haraka”. Milipuko ya mabomu iliyotokea katika Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 511 KJ, Gongo la Mboto, Dar es Salaam mwaka 2011, yeye ndiye alikuwa Waziri wa Ulinzi.

Taarifa zilizoandikwa na vyombo vya habari wakati huo zinaonyesha kuwa mabomu yale yalilipuka kutokana na uzembe na hatua ya Serikali kutoteketeza baadhi ya mabomu ambayo hayakuhitajika tena kwa kisingizio cha ukosefu wa bajeti ya suala hilo.

Maisha ya raia yalipotea, nyumba za watu ziliharibiwa na nyingi hazijalipwa hadi leo au zimelipwa kiduchu na kulikuwa na hofu kubwa. Ikumbukwe kuwa kadhia ya ulipukaji wa mabomu haikuanza 2011. Hata mwaka 2009 Mwinyi akiwa Naibu Waziri wa Ulinzi kulitokea mlipuko wa aina hiyo Mbagala.

Akiwa waziri (mwaka 2011) angekuwa amelifuatilia jambo hilo vizuri na kuchukua hatua za kuteketeza mabomu yale mapema kutokana na mafunzo ya milipuko ya Gongo la Mboto ya mwaka 2009, hakika kadhia ya 2011 isingelitokea, kuchelewa kwa wizara kuchukua hatua kulisababisha yote haya na hata Dk Mwinyi aliposhinikizwa na wananchi kujiuzulu wadhifa wake wa kisiasa kama alama ya kuonyesha kuguswa na uzembe huo, alikaidi na kutamka hadharani kuwa hawezi kufanya hivyo.

Anaweza pia kupimwa kama mtu anayefanya uamuzi taratibu wakati alipokabidhiwa Wizara ya Afya. Migomo ya madaktari ilipopamba moto na wagonjwa wakifariki kwa kukosa huduma, Dk Mwinyi alichelewa mno kufanikisha diplomasia za kutatua mgogoro ule, ikumbukwe kuwa madai ya madaktari yalikuwa halisi na yanayomgusa kila mwana jamii, hata pale madaktari walipoweka msimamo wa kumkataa katibu mkuu wa Wizara ya Afya wakati huo, Mwinyi hakuweza kuwashawishi “mabosi” wake wamuondoa haraka ili kurudisha uhusiano, kutatua mgogoro na kuokoa maisha ya raia na hata hakusikika kutoa kauli juu ya katibu huyo. Ufanyaji uamuzi wa polepole ni tatizo kubwa kwa Dk Mwinyi.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?

Jambo moja litakalomsaidia Dk Mwinyi kuvuka kizingiti cha mchujo wa wagombea ni uzoefu wa kutosha, tena wa kuongoza wizara nyeti kabisa. Tangu mwaka 2001 hadi leo (miaka 15), Dk Mwinyi ameweza kuhimili vishindo vya uongozi wa wizara tofautitofauti zikiwamo zile nyeti (Ulinzi na Afya).

Mara zote yalipofanywa mabadiliko ya mawaziri wakati wa Mkapa na hata Kikwete, yeye “alisavaivu” na kurejeshwa kwake mara kadhaa kwenye wizara ya ulinzi ya nchi kunamfanya aonekane kama mtu anayeijua vizuri nchi hii na hivyo anafahamu mambo mengi nyeti tofauti na wanasiasa wengi.

Jambo la pili, Dk Mwinyi ni Mtanzania mwenye asili ya Zanzibar (Mzanzibari) na kama tunavyofahamu, kumekuwa na majadiliano makubwa juu ya nafasi ya Zanzibar katika Muungano. Serikali ya CCM inaona isipotengeneza uwezekano wa Wazanzibari wengine kupewa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku za mbele, Zanzibar inaweza kukata tamaa kuendelea na Muungano wa upande mmoja. Kati ya marais wanne walioongoza Tanzania hadi sasa, Mzanzibari ni mmoja tu, Ali Hassan Mwinyi (baba yake Dk Mwinyi). Ikiwa CCM itaona kuwa huu ni wakati wa Mtanzania kutoka Zanzibar kukabidhiwa Ikulu ya Magogoni kwa mara ya pili, basi Dk Mwinyi anaweza kuwa tishio kubwa kwa wagombea wengine.

Jambo la tatu linaloweza kumvusha ni “dhana ya kuwa muumini wa Muungano” na hata kuziishi faida za Muungano kwa ukaribu. Dk Mwinyi ni mwanasiasa wa pekee ambaye amekuwa mbunge katika Bunge la Tanzania akiwahi kuwakilisha wananchi kutoka Bara (Mkuranga) na baadaye Kwahani (Zanzibar). Bahati ya namna hii ukiongeza na namna ambavyo amekuwa mmoja wa watu wanaotoka katika familia zinazoamini katika Muungano, inaweza ikawa sababu nyingine ya kuvushwa na kupewa uteule wa CCM kwenye urais hapo Oktoba huku wakubwa wakijua nchi imewekwa katika mikono salama “kwa masilahi yao”.

Pamoja na kuwa katika wadhifa wa juu serikalini na kwenye baraza la mawaziri kwa miaka 15, na hivyo kufahamiana na wanasiasa wengi wa ngazi ya juu, Dk Mwinyi hakuwahi kujipambanua au kushabikia kundi lolote la wasaka urais, amejiweka mbali na makundi yanayosigana na hali hiyo inaweza kumfanya aonekana kama “afadhali” ukilinganisha na wenzake.

Mwisho, kwenye mchujo wake, ile dhana ya “kuwahi kuwa mtoto wa Rais mstaafu” inambeba. Dhana hii si ya kudharau, watoto wengi wa watu waliowahi kuongoza nchi, nao walikuja kuwa viongozi wa nchi, George Bush (Jr) - Marekani, Uhuru Kenyata – Kenya, Joseph Kabila – DRC, Amani Karume – Zanzibar, mifano ipo lukuki tu. Sielewi falsafa ya utaratibu huu lakini sote tunakubaliana kuwa duniani kote hauhojiki kwa sababu majibu yake ni kuwa “amechujwa kwa utaratibu tuliojiwekea ndani ya chama/nchi” na “ana haki kama raia wengine wa kawaida”.

Nini kinaweza kumwangusha?

Mambo mawili makubwa yanaweza kumwangusha Dk Hussen Mwinyi, la kwanza ni kuwa na mtandao dhaifu ndani ya CCM hususani Tanzania Bara. Jambo hili litamwathiri ikiwa makundi yenye nguvu ndiyo yatabainisha namna ya kumpata rais kupitia CCM kwa sababu hana ufuasi mkubwa ndani ya chama hicho na si mwanasiasa maarufu (hasa Bara).

Pili ni “Uzanzibari”. Kitendo cha Mwinyi kutokea Zanzibar kinaweza kuwa kitisho kwake, hasa ikiwa CCM haitaona manufaa yoyote kumtoa Rais Zanzibar kwa kuhofia kuwa anaweza kupambana na mgombea wa Ukawa ambaye ni Mtanzania wa asili ya Bara. Hofu ya CCM inaweza kuzidi ikiwa itajihakikishia kuwa watu milioni 45 wa Tanzania Bara ya leo hawatakubali kirahisi kuongozwa na Rais atokaye Zanzibar.

Asipopitishwa (Mpango B)

Ikiwa Dk Mwinyi hatapitishwa kugombea urais kupitia CCM nadhani itampasa atazame masuala mengine muhimu ya kufanya na kulisaidia Taifa. Ameshakuwa mbunge kwa miaka 15, ni muda muafaka kuwaachia wengine nao watatue changamoto za wananchi kwa sababu “ikiwa umeshindwa kutatua mambo fulani kwa miaka 25, ukiongezewa mitano hutaweza kabisa”.

Moja ya jambo muhimu ambalo Dk Mwinyi anaweza kulipa kipaumbele akiachana na siasa ni kuisaidia nchi katika masuala ya kidiplomasia kwa kutumia uzoefu wake wa kuongoza wizara nyeti au pia kurudi na kutibu wanadamu (taaluma aliyoisomea). Lakini namuona Dk Mwinyi kama mtu anayeweza kuwa kitisho cha wasaka urais wa Zanzibar miaka mitano ijayo na jambo hili pia lisipuuzwe.

Hitimisho

Hakika, Dk Hussein Mwinyi si mtu wa kubeza, kiuadilifu, kiuchapakazi, kimienendo, kiuzoefu na hata kiutulivu. Safari yake ya kisiasa inaweza kuwa ndefu bado ikiwa hatachukua uamuzi wa kupumzika, nasisitiza kuwa namuona kama kiongozi mkubwa zaidi, hasa upande wa Zanzibar miaka ijayo. Vyovyote vile iwavyo, namtakia kila la heri.

Julius Mtatironi Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759.
Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni yake binafsi.