Ucheleweshaji malipo, ukosefu mitaji vyawaleta pamoja makandarasi kujadili
Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Mwanga Hakika Bank akifafanua jambo katika mkutano na wanahabari. Kulia ni Katibu Mkuu wa Umoja Chama Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania ( Tucasa), Baraka Materu
Muktasari:
- Chama chao, Tucasa, chasema kimeanza kushughulikia baadhi ya changamoto hizo huku kikiamini kongamano la wanachama wake litatoa fursa kwa mawazo na mapendekezo zaidi ya kupata ufumbuzi wa kudumu.
Dar es Salaam. Chama cha Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (Tucasa) kimeiwata wadau wa sekta ya ujenzi kushiriki kongamano la kujadili na kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hiyo, zikiwemo za ucheleweshaji wa malipo na ukosefu wa mitaji.
Licha ya kuwa Tucasa imesema imeanza kushughulikia baadhi ya changamoto hizo, imesema kongamano hilo litatoa fursa kwa wadau kutoa mawazo na mapendekezo zaidi ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa kuboresha mazingira ya sekta ya ujenzi.
Katibu Mkuu wa Tucasa, Baraka Materu amewaambia wanahabari leo Jumatatu Julai 6, 2026, ucheleweshaji wa malipo bado katika kazi za ujenzi zinazoendelea vimekuwa changamoto muda mrefu, hivyo kongamano hilo litakalofanyika Julai 31, 2026 jijini Dodoma litatoka na suluhisho.
Amesema makarandasi wanaofikia hatua fulani ya ujenzi wanapohitaji fedha ili kuendelea na shughuli hiyo hawazipati kwa wakati.
“Kumekuwa na uchelewashaji wa malipo unaosababisha miradi kuzorota. Pia suala uhaba wa mitaji na upatikanaji wa mikopo ya bei nafuu, kwa sababu sasa hivi tuna ushindani mkubwa kati ya makandarasi wazawa na wageni,” amesema.
“Miradi ya ujenzi huwa inategemea mikopo ya benki ambayo inakuja na riba kubwa ambnayo baadhi ya makandarasi wanashindwa kustahimili,” amesema Materu.
Juni 8, 2026 Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alisema Serikali inatoa kipaumbele cha malipo kwa makandarasi wa ndani kama mkakati wa kuimarisha uchumi wa taifa na kuendeleza uwezo wa kitaalamu, akisema hadi sasa Sh90 bilioni zimeshalipwa.
“Tucasa tumeshachukua hatua kadhaa za namna ya kutatua changamoto hizi, ikiwemo kupendekeza kwa Serikali kutunga sheria ya malipo itakayopunguza tatizo la ucheleweshaji wa malipo na kuleta unafuu,” ameeleza.
Mbali na hilo, Materu amesema Tucasa ipo katika mchakato wa kuandaa mfuko maalumu ili kupata mtaji wa makandarasi, ikisema hatua hizo, zote zitajadiliwa kwa kina katika kongamano hilo.
“Kongamano la mwaka huu litakuwa la kipekee kwa sababu halitakuwa na kiingilio, tofauti na yale mawili yaliyopita. Lengo ni kutoa nafasi kwa wadau wengi zaidi kushiriki, kubadilishana uzoefu na kujadili masuala yanayoigusa sekta yetu,” amesema Materu.
Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Mwanga Hakika Bank inayofadhili kongamano hilo, Lucy Kisasa amesema benki hiyo na Tucasa, wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali kwa muda mrefu zinazolenga kuisaidia jamii.
Pamoja kudhamini ‘Tucasa Day’, Kisaswa amesema benki hiyo Juni 23 ilizindua kampeni ya ‘benki kwa zero’ inayowagusa Watanzania wote kwa kurahisishwa huduma mbalimbali.