Ufaransa, Tanzania zashuhudia ukuaji wa uchumi, biashara na uhusiano

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frédéric CLAVIER

Muktasari:

  • Leo, katika kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Ufaransa, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frédéric CLAVIER, amefanya mahojiano na gazeti la Mwananchi na kuweka wazi shauku ya Ufaransa katika kuboresha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na Ufaransa.

Leo, katika kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Ufaransa, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frédéric CLAVIER, amefanya mahojiano na gazeti la Mwananchi na kuweka wazi shauku ya Ufaransa katika kuboresha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na Ufaransa.

Swali: Mheshimiwa Balozi, Siku ya Kitaifa ya Ufaransa ina maana gani kwa Wafaransa na dunia nzima?

Jibu: “Kihistoria, Siku ya Kitaifa ya Ufaransa imewekwa kusherehekea ushindi wa watu wa Ufaransa dhidi ya mifumo dhalimu na kandamizi ya kisiasa, ushindi ambao ulisababisha kuwa na haki ya kujitawala kwa taifa la Ufaransa. Tangu wakati huo, siku hii imekuwa ni tukio la kutukumbusha kiini cha misingi yetu na wito wa taifa la Ufaransa: yaani Uhuru, Usawa na Udugu.

Kwa mazingira hayo, Ufaransa na Tanzania zina misingi mingi inayofanana, ambayo imeziwezesha kuwa na maelewano kati ya nchi zetu mbili na uhusiano wa kuaminika tangu kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika Disemba 9, 1961.

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frédéric CLAVIER (mbele, mwenye suti nyeusi), Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Ufaransa na Tanzania, Christophe Darmois (mbele, mwenye suti ya bluu) wakiwa katika picha ya pamoja na timu ya wafanyakazi wa Ufaransa mbele ya o_si za ubalozi wa Ufaransa nchini. (Picha na Loveness Bernard).

Imani hii ambayo tumeijenga kwa miaka yote inatupa fursa ya kufurahia mahusiano bora katika nyanja muhimu kadhaa ambazo ni; uchumi, siasa, jamii na utamaduni. Mfano halisi wa hivi karibuni ni kazi tuliyoifanya kwa pamoja na mafanikio katika Jukwaa la Usawa wa Kijinsia lililofanyika Paris kati ya Juni 30 hadi Julai Pili mwaka huu na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango, ikidhihirisha nia thabiti ya Tanzania katika kushughulikia masuala ya usawa wa kijinsia.”

Swali: Mheshimiwa, unaweza kutueleza hali ya kiuchumi ya Ufaransa na Tanzania na ushiriki-ano wa kibiashara wa nchi hizo ulivyo?

Jibu: “Biashara baina ya nchi hizi mbili, Ufaransa na Tanzania inaongezeka, lakini bado, kwa maoni yangu, bado haiakisi ubora wa uhusiano wetu wa pande mbili, ingawa tulishuhudia ukuaji wa biashara katika miaka michache iliyopita.

Mwaka 2020, jumla ya kiwango cha biashara kati ya Ufaransa na Tanzania kilifikia Dola za Marekani milioni 150. Zaidi ya asilimia 90 ya mauzo ya nje ya Ufaransa yalitegemea sekta kuu nne ambazo ni: vifaa vya kimakanika, vifaa vya umeme, elektroniki na Tehama, huku upande wa mauzo ya nje ya Tanzania kwenda Ufaransa yalitoka katika sekta za bidhaa za viwanda vya chakula kitokanacho na kilimo, misitu na uvuvi.

Ili kuongeza chachu ya ushirikiano bora zaidi wa kiuchumi baina ya pande hizi mbili, Chama cha Wafanyabiashara wa Ufaransa na Tanzania (FTCC) kilianzishwa Januari 2020 kikiwa na lengo la kukuza mahusiano baina ya makampuni ya nchi hizi mbili.

Nina uhakika kuwa mabadilishano baina ya nchi zetu mbili yataongezeka maradufu katika miaka ijayo hususan tunaposhuhudia juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuufanya uchumi kuwa kitovu cha sera za nje za Tanzania na hamu yake ya kuboresha hali ya biashara nchini na kukuza ufanyaji biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Swali: Sekta gani ambazo kampuni za Ufaransa zimewekeza vya kutosha hivi karibuni nchini Tanzania?

Jibu: Mpaka sasa, kuna zaidi ya kam-puni 40 za Ufaransa zilizoanzishwa nchini Tanzania zikiwamo kampuni 13 za kimataifa. Katika miaka michache iliyopita, kampu-ni za Ufaransa zimewekeza zaidi katika sekta za nishati, uchukuzi na teknolojia.

Siwezi kutaja kampuni zote, kwa mfano, kila mtu alisikia kuhusu ushiriki wa TotalEnergies katika mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP). Bomba hili litasafirisha mafuta kutoka Uganda kwenda Tanga Tanzania kwa ajili ya kuyauza katika masoko ya dunia, ni moja ya mradi mkubwa zaidi unaoendelea hivi sasa Afrika Mashariki.

Utapita mikoa minane (8) nchini Tanzania na unatarajiwa kutengeneza ajira takriban 10, 000. Pia niizungumzie kampuni ya Maurel & Prom, ambayo inafanya kazi nchini tangu mwaka 2006 katika moja ya maeneo matatu (3) yenye utajiri wa gesi nchini, au hii kampuni ya Engie Energy Access, iliyoanzishwa mwaka 2020 ili kuunganisha pamoja shughuli za kampuni za usambazaji wa umeme wa nje ya gridi, ujenzi wa gridi ndogo na usambazaji wa vifaa vya umeme wa jua majumbani.

Katika sekta ya uchukuzi, CMA-CGM inasimamia asilimia 12 ya huduma za usafirishaji kwa njia ya baharini nchini katika bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Zanzibar. Bolloré Transport & Logistics imeamua kuendesha shughuli zake za bandari kavu Dar es Salaam, na usafirishaji wa mizigo kwa barabara kwenda nchi ambazo hazina bahari katika upande wa magharibi.

Pia, Kampuni ya Airbus iliuza ndege mbili aina ya Airbus A220-300 kwa kampuni ya ndege ya Tanza-nia mwaka 2018 na 2019 na pia ina mpango wa kuongeza ndege nyingine mbili, ndani ya mwaka huu.Mwisho, ni hii kampuni ya Carwatt inayobadilisha magari ya mafuta kuwa ya umeme - iliyoanzishwa Tanzania kupitia E. motion Africa, iliyoanzishwa mwaka 2019, ikiwa na lengo la kusambaza umeme katika mtandao wa mabasi wa Dar es Salaam na magari yote ya utalii yanayaozunguka katika hifadhi za wanyama.”

Swali: Licha ya msaada wa kiuchumi, ni miradi gani mikubwa iliyotekelezwa na Ufaransa hapa nchini?

Jibu: Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) limekuwa likifanya kazi nchini Tanzania kwa miaka 25, likijikita zaidi katika kufadhili miundombinu ya sekta ya nishati, maji na uchukuzi. Utengaji fedha kwa miradi ya maendeleo ume-ongezeka mara tatu katika miaka mitatu, ikifikia Dola za Marekani 180 milioni kila mwaka. Hali hiyo inaonyesha, imani ya Ufaransa katika hatua za maendeleo ya Tanzania. Kwa miaka mitatu ijayo, mkakati wa AFD ni kuendelea kujikita katika sekta za maji na usafi wa mazingira, nishati na uchukuzi, lakini pia kuelekeza fedha zake katika uhifadhi wa bayoanuai na kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi na endelevu.”

Swali: Ufaransa imekuwa ikisaid-ia nchi zinazoendelea, hususan Afrika kukabiliana na athari za Uviko 19. Je! Ufaransa iliisaidiaje Tanzania?

Jibu: “Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron aliandaa Mkutano wa kuwezesha kifedha chumi za Afrika, Mei 18 2021 mjini Paris. Huu ndiyo ulikuwa mkutano wa kwanza kimataifa kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa njia ya mtandao. Lengo la Mkutano huo lilikuwa kutafuta njia za kukabili athari za kiafya na kiuchumi ambazo janga hilo limesababisha barani Afrika. Rais Macron aliunda “Mpango Mpya kwa ajili ya Afrika”, akipendekeza pamoja na mambo mengine kwamba nchi tajiri zihamishe sehemu ya haki zao maalumu (SDR) kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuelekezwa katika uchumi wa Afrika ili kukusanya angalau Dola za Marekani Bilioni 100 kwa ajili ya Afrika.

Siku chache baadae, kwa niaba ya Serikali ya Ufaransa na mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, nilitia saini Mpango wa Kusimamisha Deni (DSSI). Mpango huo, uliozinduliwa na Rais Emmanuel Macron unakusudia kuchelewesha ulipaji wa deni, ukitoa fursa kwa Serikali kutumia fedha ilizonazo kupunguza athari za kiuchumi zilizotokana na Uviko 19.

Mwisho, kaulimbiu ya Mkutano wa 28 wa Ufaransa na Afrika utakaofanyika Ufaransa mwezi Oktoba, itakuwa “Miji Bora kwa Maisha Bora” ukiwa na lengo la kukuza ushirikiano mpya wa kisiasa, kiuchumi, na kubadilishana maarifa katika mipaka na miji endelevu lakini pia ushirikiano mpya katika nyanja zingine, kama vile; huduma ya afya, elimu, mipango miji na utamaduni.