Uhalifu, mauaji vyatikisa Dodoma, Polisi watoa onyo

Muktasari:

  • Matukio ya mauaji katika mkoa wa Dodoma yanatajwa kuongezeka katika siku za hivi karibuni, huku sababu za mauaji hayo zikitofautiana na baadhi ya watu wakilinyooshea kidole Jeshi la Polisi kuwa linashindwa kutimiza wajibu wake

Dodoma. Matukio ya mauaji katika mkoa wa Dodoma yanatajwa kuongezeka katika siku za hivi karibuni, huku sababu za mauaji hayo zikitofautiana na baadhi ya watu wakilinyooshea kidole Jeshi la Polisi kuwa linashindwa kutimiza wajibu wake

Mbali na mauaji hayo, visa vya watu kujeruhiwa kwa mapanga na nondo vinatajwa kuongezeka katika mitaa ya katikati jijini Dodoma licha ya Polisi kukiri kuwakamata waharifu wengi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Onesmo Lyanga, alikiri kuwapo kwa matukio hayo ambayo yanahusisha pia wizi wa magari, pikipiki na kukamatwa kwa nyara za Serikali na dawa za kulevya. Mpaka sasa watu watu 67 wanashikiliwa.

Kati ya Februari 25,2022 hadi Machi 11, 2022 kulitokea mauaji ya watu wawili kwenye maeneo tofauti, moja likihusisha mwanamke aliyekatwa mapanga asubuhi akienda kazini Mtaa wa Mtumba na mvulana mwenye umri wa 22)ambaye aliuawa katika ugomvi wa kugombea Sh400 ambayo ilikuwa chenji ya sigara.

Mchungaji asimulia mwanawe alivyouawa

Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Anglikana na baba mzazi wa Lydia Mgogolo, Peter Mgogolo alisema kuwa mwanawe aliuawa kikatili na watu wasiojulikana ambao walitumia mapanga kumkatakata kichwani, baada ya kuwa amepigwa na kitu kizito na hivyo kumsabibishia kifo chake.

Mchungaji Mgogolo anasema Lydia (41) alitoka nyumbani kwake Mtaa wa Mahomanyika kwenda Mtumba ambapo ni jirani kwa ajili ya kufanya kazi ya usafi katika majengo ya Wizara ya Katiba na Sheria walikokuwa wamepangiwa na kampuni ya usafi.

Anasema mwanzoni mwa 2020, Lydia aliingia mkataba wa kazi na kampuni ya Pahita Enterprises Company akiwa miongoni mwa waliokuwa wakifanya usafi kwenye majengo ya Serikali kupitia kampuni hiyo na wakati wote alikuwa akitoka nyumbani kwake Mtaa wa Mahomanyika kila siku asubuhi na kurudi jioni.

“Siku ya tukio alitoka na mwenzake asubuhi na mapema hapa kuelekea kazini kwake, walipofika njiani wakakutana balaa hilo, walipigwa mapanga saa 12 asubuhi wakatupwa kwenye mfereji, bahati nzuri mwenzake alikutwa hajapoteza maisha,” anasema Mchungaji Mgogolo.

Alisema mtoto wake aliuawa na watu ambao idadi yao inakisiwa ni wawili hadi watatu, ingawa ukweli anasema atakuwa nao mwenzake ambaye bado hajapata fahamu hadi sasa akisema wanamwombea usiku na mchana madaktari wamsaidie ili akipona wapate ukweli.

“Lydia hakuwa na ugomvi na mtu, hakuwahi kutuambia kama ana kisa na mtu, lakini wamemuua mwanangu akihangaika na maisha yake kwa ajili ya watoto watatu ambao amewaacha bado wakimtegemea, inauma, inasikitisha lakini Mungu ndiye mgawaji wa yote,” anasema Mchungaji Mgogolo.

Mauaji mengine

Katika mauaji mengine, kijana ambaye hakutajwa jina lake aliuawa kwa kupigwa na bomba kichwani upande wa nyuma katika ugomvi wa chenji ya Sh400 ambazo marehemu alikuwa anadai baada ya kununua sigara.

Katika tukio hilo ambalo Polisi wamekiri kumshikilia muuza duka, taarifa zinasema Machi 8,2020 majira ya mchana katika Mtaa wa Tofiq Kata ya Viwanda, kijana wa miaka 22 mwendesha bajaji mkazi Swaswa alikwenda kununua sigara aina ya nyota ambayo inauzwa Sh100.

Kwa mujibu wa mashuhuda, marehemu alitoa Sh500 ndipo akaanza kuomba chenji ya Sh400 ndipo muuzaji (mtuhumiwa) akagoma kutoa kwamba hakuwa amepewa Sh500 na katika majibizano alichukua bomba lililokuwa chini ya meza na kumpiga kisogoni na kufariki papohapo.

Matukio ya kupigana mapanga

Katika mitaa ya Chang’ombe na Mtaa wa Mwaja, kunatajwa kuwa na matukio ya watu kupigwa mapanga mchana kweupe huku sababu zake zikiwa ni kugombea wanawake na wengine wakieleza kugombea mbwa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwaja Athuman Makuka alisema tukio la hivi karibuni vijana wa mitaa jirani walifanya vurugu katika eneo la soko la Bonanza hadi kwenye kituo cha Polisi cha eneo hilo lakini sababu kubwa ikiwa ni ugomvi wa kugombea mbwa.

Makuka alisema kulitokea mabishano ya vijana waliodhurumiana mbwa ndipo wakaanza ugomvi uliopelekea kujikusanya kwa waendesha bodaboda na kuanza vurugu mtaa mzima.

Polisi yakiri matukio

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Onesmo Lyanga alisema katika kipindi hicho, walikamata wahalifu 67 akiwamo mtuhumiwa wa mauaji ya mwendesha bajaji, wizi wa pikipiki, nyara za Serikali, dawa za kulevya na wasichana watatu wanaojihusisha na biashara ya kuuza miili yao.

Kamanda Lyanga alisema alisema matukio hayo yamekuwa yakitokea kwa nyakati tofauti lakini Polisi iko macho kwani wanafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na wananchi.