Uhuru, Ruto ni vita ya urais na hofu ya kupelekana jela

Muktasari:

  • Licha ya kurushiana maneno na mivutano ya kisiasa ya hapa na pale kati ya wanaowania nafasi za uongozi na wafuasi wao, Rais Uhuru Kenyatta ameahidi uchaguzi utakaofanyika wiki ijayo utakuwa huru na wa haki hivyo kuwataka Wakenya wajitokeze kwa wingi kupiga kura

Wakati zikiwa zimebaki siku nane Wakenya kupiga kura ya kuwchagua viongozi wao, kadiri tarehe ya uchaguzi inavyosogea, ndivyo joto linavyoongezeka, munkari unateka hoja za kampeni.

Sasa sura ya kiti cha urais ni mapambano ya kufa au kupona baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais, William Ruto.

Sura ya kampeni za urais Kenya hivi sasa zinajenga picha kuwa kama Rais Uhuru atashuhudia Ruto akishinda kiti, atakuwa kwenye wakati mgumu wa kisheria, vivyo hivyo kwa Ruto kama atakuwa shuhuda mpinzani wake, Raila Odinga, akiapishwa kuwa Rais wa Tano wa Kenya.

Dhamira ya Serikali itakayoundwa na Ruto kumfungulia mashtaka Uhuru, imeshawekwa bayana na Mgombea Mwenza wa urais wa United Democratic Alliance (UDA), Rigathi Gachagua.

Wiki mbili zilizopita, Gachagua akizungumza na maneno yake yakirushwa moja kwa moja kwenye runinga na kutazamwa nchi nzima, alisema kuwa Uhuru ndio mhusika mkuu wa vitendo vya ufisadi wa mali za umma.

Chama cha UDA kipo ndani ya ushirikiano wa Kenya Kwanza Alliance. Gachagua aliahidi kuwa baada ya Ruto na yeye (Gachagua), kushinda kiti cha urais, serikali itakayoundwa na Kenya Kwanza, itaunda Tume ya uchunguzi wa ufisadi wa mali za umma na wahusika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Gachagua aliyasema hayo kwenye mdahalo wa wagombea wenza wa kiti cha urais. Waongozaji wa mdahalo, James Smart na Sophia Wanuna, walimuuliza mara kwa mara Gachagua kama lengo la Serikali ya Ruto ni kumfungulia mashtaka Uhuru, akawa hatoi jibu la moja kwa moja.

Bila kusema ndio au hapana, Gachagua alijibu kuwa serikali ya Kenya Kwanza itawashughulikia wahusika wakuu wa ufisadi wa mali za umma na familia zao, akasisitiza kuwa Uhuru ni mnufaika wa unyonyaji wa mali za umma.

Kwa miaka mingi, tangu Rais wa Kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta, familia ya Kenyatta imekuwa ikitajwa kuwa na utajiri mkubwa ambao iliupata kwa kujilimbikizia mali za umma. Kenyatta ni baba mzazi wa Uhuru.

Mama mzazi wa Uhuru, Ngina Kenyatta, amekuwa akihusishwa na utajiri mkubwa pamoja na wanaye, akiwemo Uhuru. Gachagua anaposema Uhuru ni mhusika mkuu wa ufisadi wa mali za umma, kisha kutoa ahadi ya kuwashughulikia wahusika wa ufisadi na familia zao, moja kwa moja taa nyekundu inawaka kwa familia ya Kenyatta.


Ruto naye matatani

Hoja za Gachagua kuwa watamuundia tume Uhuru na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, haijapita tupu. Mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya Coalition, Raila Odinga, alisema akishinda urais, atataka Ruto ajiekeze alipataje ardhi ekari 2,500 ya Shamba la Mata, lililopo kaunti ya Taifa Taveta.

Kabla ya Raila kuzungumza kwenye mkutano wa hadhara, Katibu Mkuu wa Azimio la Umoja One Kenya, Junet Mohamed, alishamwandikia barua Waziri wa Ardhi, Farida Karoney, akimtaka ashughulikie suala la ekari 2,500 ambazo Ruto anamiliki Taifa Taveta.

Farida pia ni mkuu wa Tume ya Maadili na Mapambano Dhidi ya Rushwa, hivyo Junet alimwandikia: “Tume ya Maadili inapaswa kupewa mamlaka, iingilie kati, kisha itoe mapendekezo ama hati za umilili zilizotolewa kwa Ruto zifutwe au ardhi husika irudishwe serikalini kwa manufaa ya wananchi wa Taifa Taveta.”

Ukiachana na barua hiyo, hoja nyingi ambazo zimekuwa zikitoka Azimio la Umoja kuhusu Shamba la Mata, Taifa Taveta, ni kuwa Ruto amepata mali hiyo kinyume na sheria, kwa hiyo anapaswa kufikishwa mahakamani kwa kuvunja sheria ya maadili ya utumishi wa umma.

Orange Democratic Movement (ODM) ni chama kikuu kinachounda Azimio la Umoja One Kenya Coalition. Naibu Kiongozi wa ODM, Hassan Joho, amepata kusema kuwa Ruto ni mhalifu na anapaswa kushtakiwa kwa uporaji wa ardhi ya wananchi wa Taifa Taveta.

Utetezi wa Ruto kuhusu ardhi hiyo ni kwamba yeye alipewa kama zawadi na mbunge wa Taifa Taveta, Basil Criticos, baada ya kumsaidia changamoto zake za kisheria zilizokuwa zikimkabili.

Joho alijibu kuwa sheria ya maadili ya utumishi wa umma Kenya, inakataza kiongozi kuchukua kiwango kikubwa cha zawadi na inaelekeza kuwasilisha kwa umma. Kwa mujibu wa Joho, ekari 2,500 za Shamba la Mata, linalomilikiwa na Ruto linapaswa kuwa mali ya umma kwa sababu ni zawadi aliyopewa akiwa Naibu Rais.


Ruto amvaa Uhuru

Mashambulizi ya Azimio kuhusu ekari 2,500 za Shamba la Mata, zimesababisha Ruto kumjia juu Uhuru, akimtaka na yeye aoneshe uthibitisho wa ardhi ambayo familia yake inamiliki eneo la Pwani.

Ruto alisema, yupo tayari kuonesha na kuthibitisha jinsi ambavyo alijipatia ekari 2,500, Taifa Taveta, akampa changamoto Uhuru kufanya kama yeye kwa familia yake kuonyesha uhalali wa umiliki wa ardhi wanayomiliki eneo la Pwani.

Msisitizo wa Ruto ni kuwa yeye akiingia madarakani, ataweza kudhibiti rushwa kwa sababu atafanya taasisi za maadili ziwe huru bila kuingiliwa na mamlaka za juu.

“Lazima tujenge taasisi zenye uwezo wa kuchunguza rushwa, wizi wa rasilimali za umma, ufisadi na mgongano wa masilahi kwa ofisa yeyote wa serikali. Kuna nchi zinawapeleka marais wao mahakamani kwa sababu ya rushwa na tunatakiwa kufikia kiwango hicho,” Ruto aliyasema hayo akiwa kwenye mahojiano na televisheni ya Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC).

Siku 8 zimebaki kuifikia siku ya uchaguzi Kenya, utakaofanyika Agosti 9, Uhuru amejiweka timu moja na Raila. Imani ni kwamba Waziri Mkuu huyo wa zamani akishinda urais, kwake itakuwa salama. Ushindi wa Ruto ni balaa.

Ilani ya Uchaguzi ya Kenya Kwanza, inaeleza kuwa ndani ya siku 30 baada ya kuingia madarakani, zitaanzishwa mamlaka za kuhoji hadharani ili kubaini uwepo wa ufisadi wa mali za umma.

Uhuru, Raila na Mgombea Mwenza wa Azimio la Umoja, Martha Karua, wamekuwa wakimtupia tuhuma Ruto kuwa mhusika mkuu wa kupanda gharama za maisha ya Wakenya kwa sababu hupandisha bei ya unga wa mahindi.

Ahadi ya Uhuru ni kuendesha uchunguzi ambao utakomesha hujuma za kupandisha bei ya bidhaa hasa unga wa mahindi na kusababisha Wakenya wale ugali wenye gharama kubwa.

Uhuru alisema, Martha ni mwanamke hodari katika mapambano dhidi ya rushwa, hivyo anaamini watu wote wanaojinufaisha kwa mgongo wa Wakenya maskini, watashughulikiwa ipasavyo.

Raila amesema akichaguliwa, Martha sio tu atakuwa Naibu Rais bali pia Waziri wa Sheria.