Ujenzi bomba jipya la gesi kuanza Mtwara

Muktasari:

  • Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza mchakato wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Ntorya hadi Madimba lenye urefu wa kilomita 35.



Mtwara. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza mchakato wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Ntorya hadi Madimba lenye urefu wa kilomita 35.

Mchakato huo umeanza kwa kufanya mkutano wa uhamasishaji kwa wananchi wa kata ya Madimba, Moma, Mbawala na Nanguruwe kuhusu ujenzi wa mradi huo ambao utaanzia kijiji cha Ntorya.

Akizungumza leo Jumatano  Oktoba 5, 2022 kwenye mkutano wa hadhara na wananchi hao,  mkuu wa Wilaya ya Mtwara,  Dustan Kyobya amesema hatua ya awali ya utafiti wa mkuza utakaotumika kupitisha bomba ulishafanyika na kubaini vijiji 12 vitakavyopitiwa na bomba hilo.

Ametaja vijiji hivyo ni Namayakata, Ngorongoro, Mbawala, Mwindi, Nachenjele, Maili kumi, Ding’ida, Likweta, Minyembe, Namidondi na Mendachi.

Amesema  hatua inayokwenda kufanyika sasa ni zoezi la uthamini wa mali kwenye mkuza wa bomba wenye upana wa mita 20.

“Lengo la zoezi hili ni kutambua mwendelezo uliofanyika katika ardhi hiyo ikiwemo nyumba, mazao na mali nyingine  kubaini thamani yake na kuandaa taratibu za  fidia kwa wamiliki,”ameeleza.

Kyobya amewataka wananchi wa maeneo ya yanayopitiwa na mkuza wa bomba kutoa ushirikiano kwa TPDC, wakati watakapopita kwenye maeneo yao katika  uthamini.

Meneja wa biashara ya gesi TPDC, Emmanuel Gilbert amesema utekelezaji wa mradi huo unalenga kuongeza uzalishaji wa nishati ya gesi asilia kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya gesi katika uzalishaji wa umeme, kwenye magari, viwandani na majumbani.