Ukamataji kimya kimya wa polisi wazua utata

Makada wa Chadema wakiwa pamoja na mhamasishaji wa Bavicha, Twaha Mwaipaya (asiyevaa viatu katikati) mara baada ya kuachiwa na polisi kwa dhamana Julai 5, mwaka huu. Picha na mtandao

Muktasari:

Utaratibu wa karibuni wa Jeshi la Polisi kukamata watu kimya kimya na kuwaacha ndugu na jamaa wa waliokamatwa wakihangaika vituoni kuwatafuta umewaibua wadau wa sheria na haki za binadamu wakitaka jeshi hilo kuzingatia sheria na kanuni za ukamataji.

Dar es Salaam. Utaratibu wa karibuni wa Jeshi la Polisi kukamata watu kimya kimya na kuwaacha ndugu na jamaa wa waliokamatwa wakihangaika vituoni kuwatafuta umewaibua wadau wa sheria na haki za binadamu wakitaka jeshi hilo kuzingatia sheria na kanuni za ukamataji.

Hoja hizo zimeibuka baada ya polisi kumkamata mratibu wa uhamasishaji wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Twaha Mwaipaya, kabla ya kumwachia kwa dhamana baada ya siku tano huku ndugu na wanachama wenzake wakihangaika vituoni Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam bila kuelezwa mahali alipo.

Hali kama hiyo imeshajitokeza kwa watuhumiwa kadhaa, wakiwemo Erick Kabendera, Mdude Nyagali, Peter Madereka, Freeman Mbowe na wengineo ambao awali polisi walikana kuwashikilia, lakini baadaye wakaonekana walikuwa mikononi mwa Jeshi hilo.

Mara kadhaa, jeshi hilo limelazimika kuwafikisha watuhumiwa hao maharakamani, licha ya awali kukana kuwa nao, baada ya mawakili wao kufungua mashauri ya kuomba mahakama iliamuru jeshi hilo ama kuwaachia huru au kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Hali hiyo inaelezwa na watetezi wa haki za binadamu na wanasheria kuwa ni ukiukaji wa haki za mtuhumiwa kisheria na kikatiba.

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, SACP David Misime amekanusha madai ya jeshi hilo kukamata watu kimya kimya.

“Ni wapi ambapo Jeshi la Polisi limekamata mtu, likaulizwa likashindwa kutoa taarifa? Au ni wapi sheria imetuelekeza kwamba baada ya dakika moja au mbili nikimkamata mtu nitoe taarifa? Usipouliza siwezi kuja nyumbani kwako kugonga hodi,” alisema Misime kwa njia ya mwaswali.


Sakata la Mwaipaya

Mwaipaya alikamatwa Juni 30 akiwa na viongozi wenzake wa Bavicha wanakula eneo la Msamvu, Morogoro walipotokea watu waliojitambulisha ni maofisa wa polisi na kumkamata

Baadaye waliokuwa naye walielezwa angesafirishwa kwenda Dodoma alikotenda kosa.

Hata hivyo, hakukuwa na taarifa rasmi kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro.

Alipotafutwa na Mwananchi Julai 2, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa alikuwa kwenye kikao.

Ilipofika Julai 4, Muslim alikiri jeshi hilo kumkamata Mwaipaya na kueleza kwamba alisafirishwa kwenda Dodoma lakini viongozi waBavicha walidai kuzunguka vituo vikubwa vya polisi mkoani humo bila mafanikio.

Kutokana na hali hiyo, Chadema ilifungua kesi Mahakama Kuu Dodoma, ikitaka polisi wamwachie Mwaipaya, ambayo imepangwa kusikilizwa Jumatatu, lakini Julai 5 mtuhumiwa huyo aliachiwa na polisi kwa dhamana.


Lazima wajitambulishe

Akizungumzia utaratibu wa kukamata mtuhumiwa, Wakili Joseph Kidumbuyo wa mkoani Arusha, alisema polisi wanaokwenda kumkamata mtuhumiwa lazima wajitambulishe, kumweleza mtuhumiwa kosa analokabiliwa nalo na kumuweka chini ya ulinzi.

“Polisi wanamkamata mtuhumiwa papohapo au kumuarifu afike kituoni, wanapoondoka na mtuhumiwa ni pale ambapo kosa limetendeka mbele yao na si vinginevyo,” alisema.

“Mtuhumiwa akisema hayupo tayari kuhojiwa atapewa dhamana kulingana na utaratibu wa Jeshi la Polisi.


Matukio mengine

Tofauti na tukio la Mwaipaya, ukamataji wa kimyakimya ulitokea kwa Tito Magoti, mfanyakazi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na mwenzake Theodory Giyan.

Wawili hao walikamatwa Ijumaa Desemba 20, 2019 kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam na watu waliovaa kiraia bila familia na waajiri wao kujua.

Baada ya watu wa karibu, ikiwemo LHRC kupaza sauti kwenye mitandao ya jamii kuwa wametekwa, Kamanda wa Polisi wa Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alithibitisha hawakutekwa bali wamekamatwa.

Mwingine aliyewahi kukumbwa na hali hiyo ni Mdude Nyagali, ambaye Mei 2019 alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana na Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, George Kyando aliliambia Mwananchi hakuwa na taarifa ya kukamatwa kwake, lakini alipatikana siku chache baada ya mawakili wa chama hicho kulishtaki Jeshi la Polisi.

Aprili 23 mwaka huu, uliibuka utata wa kukamatwa kwa Wakili Peter Madeleka aliyekuwa akikosoa utendaji wa polisi na Uhamiaji.

Taarifa zilieleza Madeleka alikamatwa katika hoteli ya Serena alipokuwa akihudhuria mkutano na viongozi wa polisi, walipoulizwa kuhusu kukamatwa kwake walianza kurushiana mpira kabla ya baadaye kuibukia mikononi mwa polisi na kufikishwa mahakamani.

Utata kama huo ulitokea Julai 21, 2021 baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kukamatwa jijini Mwanza na siku iliyofuata alisafirishwa hadi Dar es Salaam ambapo awali viongozi wa Chadema walimtafuta vituo kadhaa kabla ya kubainika yuko Oysterbay kisha kufikishwa mahakamani.

Hata alipokamatwa mwanahabari, Eric Kabendera Julai 29, 2019 hali ilikuwa hivyohivyo, hadi kelele zikawa nyingi mitandaoni, ndipo ikawekwa wazi yuko mikononi mwa polisi na akafikishwa mahakamani.