Ukatili chanzo watoto wa mitaani

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Martin Otieno akimkabidhi box la pampers mlezi wa kituo cha kulea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu Denis Shao ikiwa ni mwendelezo wa siku 16 za kupinga ukatili Msalato, Dodoma

Muktasari:

  • Wakati matukio ya ukatili yakitajwa kupungua katika Mkoa wa Dodoma, wananchi wametakiwa kuyaacha kabisa  ili kupunguza idadi ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

Dodoma. Licha ya matukio ya ukatili wa kijinsia kupungua mkoani Dodoma kutoka asilimia 55, mwaka  2022 hadi kufikia asilimia 44 mwaka huu, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Martin Otieno amesema bado matukio hayo yanachangia ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Mwaka 2022 Kituo cha sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kiliutaja Mkoa wa Dodoma kuongoza kwenye matukio ya ukatili wa kijinsia.

Otieno ameyasema hayo leo Disemba 6,2023 wakati akizungumza kwenye tukio la kutoa msaada katika kituo cha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Tumaini Jema, ikiwa ni mwendelezo wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Otieno amesema bado jamii inapaswa kuelimika juu ya kutojichukulia sheria mkononi, hasa kwa wazazi wenye watoto ambao ndio waathirika wakuu wa matukio ya ukatili.

“Ingawa matukio ya ukatili yamepungua kutoka asilimia 55 mwaka 2022 hadi asilimia 44 mwaka huu, lakini niiombe jamii kupunguza vitendo vya ukatili kwa sababu mtoto anapofanyiwa ukatili anaona kuishi nyumbani sio sehemu salama,” amesema Otieno.

Naye, Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF-NET) mkoani Dodoma, Eva Stesheni amesema kazi ya jeshi hilo ni kuwa karibu na jamii, hivyo  kuwatembelea wahitaji na kutoa misaada ni sehemu moja wapo ya kutengeneza mahusiano kati ya jamii na jeshi hilo.

Mlezi wa kituo hicho, Padri Denis Shao amesema kituoni hapo kuna  watoto 30 waliopatikana kwa njia mbalimbali ikiwemo ustawi wa jamii ambapo matukio ya ukatili huripotiwa.

Shao ameiomba jamii kuwa na desturi ya kuwatembelea watoto hao na kuwapa faraja ili wajione kama wengine pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu ambayo ni muhimu.

Miongoni mwa misaada iliyotolewa na Jeshi la Polisi ni mafuta ya kupaka na kupikia, mchele, unga, vifaa vya usafi, vifaa vya shule, sukari, sabuni, mikate na  taulo za kike.