Ukikamatwa bodaboda, gari yako inaishia huku
Muktasari:
- Utata umeibuka kuhusu hatima ya pikipiki na magari yanayokamatwa na Jeshi la Polisi nchini kwa makosa mbalimbali, huku kukiwa na madai ya vyombo hivyo vya usafiri kupigwa minada kwa bei ndogo baada ya mmiliki kushindwa kukomboa au kutofahamu wapi pa kuanzia kudai.
Dar/Mikoani. Utata umeibuka kuhusu hatima ya pikipiki na magari yanayokamatwa na Jeshi la Polisi nchini kwa makosa mbalimbali, huku kukiwa na madai ya vyombo hivyo vya usafiri kupigwa minada kwa bei ndogo baada ya mmiliki kushindwa kukomboa au kutofahamu wapi pa kuanzia kudai.
Idd Said, aliyezungumza na Mwananchi, amesimulia jinsi pikipiki yake aina ya TVS ilivyokamatwa na kisha kuuzwa, kwa kushindwa kulipa Sh 400,000 kama fidia.
Anasema hataisahau siku hiyo katika maisha yake, kwakuwa alikamatwa akiwa Kariakoo baada ya kumgonga mtu na hakuwa na leseni wakati huo kwa sababu tu aliisahau nyumbani.
“Nilikamatwa na kupelekwa kituoni na baadaye nikaachiwa kwa dhamana, lakini shida ikaja kwenye kufuatilia hiyo pikipiki. Ikafika hadi miezi sita nikawa nimechoka kufuatilia. Mwisho kuna siku niliyokwenda nikaambiwa nitoe Sh400,000 ili niachiwe. Kwa hiyo nikashindwa,” anasema Said.
Anaongeza kuwa alipokwenda kufuatilia tena aliambiwa muda wa kukaa pikipiki kituoni hapo umeisha na kwamba, imeingizwa kwenye pikipiki ambazo zinatakiwa ziuzwe kwa mnada.
“Kwa hiyo hivyo ndo nikawa nimepoteza pikipiki yangu ambayo niliipata baada ya kumaliza mkataba na bosi wangu nikawa naimiliki mwenyewe,” anabainisha.
Stanford Erick anasema miaka miwili iliyopita alipoteza pikipiki yake kwa kosa la kusingiziwa.
Anasema alikamatwa na kuambiwa kuwa pikipiki yake imetumika katika wizi uliotokea Kigogo Mburahati, jijini Dar es Salaam.
Anafafanua kuwa alipokamatwa aliambiwa pikipiki yake itakuwa chini ya ulinzi mpaka pale upelelezi utakapokamilika.
“Nikawa kila nikienda naambiwa upelelezi haujakamilika. Nikafuatilia mpaka nikachoka, ukapita mwaka mzima ndo nikaambiwa eti imeshauzwa katika mnada bila kufahamu na sikujua lolote kuhusu huo upelelezi,” anasema.
Polisi wakamata 319
Hivi karibuni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema kwa muda wa wiki moja hadi kufikia Agosti 9, mwaka huu jeshi hilo limekamata pikipiki 319 na madereva sita wa pikipiki walifikishwa mahakamani.
Aliyataja makosa hayo kuwa ni kutovaa kofia ngumu (helmet), kupakia abiria zaidi ya mmoja (mshikaki), kutokuwa na leseni ya udereva, kupita taa nyekundu, pikipiki mbovu na makosa ya kupita barabara ya mwendokasi DART.
Hata hivyo, wamiliki wa pikipiki na magari wamelalamikia polisi wanavyovikamata vyombo hivyo vya usafiri na wakati mwingine hulazimisha makosa (uonevu).
James John, mmoja wa waendesha bodaboda alisema alikamatwa na kuambiwa amevuka wakati taa nyekundu imewaka, jambo ambalo anasema halikuwa kweli.
“Nimekamatwa bila makosa kwa kuambiwa eti nimepita taa nyekundu, kitu ambacho sio kweli kabisa,” anasema John.
Isiaka Juma anasema kitendo kinachofanywa na jeshi hilo sio kizuri, kwani wanategemea biashara ya pikipiki kuingiza kipato kwaajili ya familia zao.
Huko Moro kukoje?
Nako kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya madereva wa magari na bodaboda wakisema wanalazimika kupoteza mali zao kutokana na Polisi kuwarundikia makosa na kutozwa faini zisizoeleweka.
Hata hivyo, Kaimu Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Morogoro, Ahimidiwe Msangi anasema kwa sasa tatizo la madereva au wamiliki kutelekeza vyombo vyao hivyo sio kubwa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Sababu kubwa ya kupungua kwa tatizo hilo ni kushuka kwa faini kutoka Sh30,000 hadi kufikia Sh10,000 kwa kosa moja, hivyo madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri wamekuwa wakimudu gharama za faini na hivyo kuchukua vyombo vyao mapema baada ya kukamatwa na Polisi,” anasema Msangi.
Kuhusu Polisi kupiga mnada vyombo vya usafiri vilivyotelekezwa kwa kushindwa kulipa faini, Msangi anasema utaratibu uliopo kabla ya kupigwa mnada ni kutoa matangazo kwenye magazeti na baadaye kupeleka taarifa hiyo makao makuu ya Polisi na kwenye mamlaka nyingine, zikiwemo TRA na Latra.
“Vyombo vya usafiri vikitelekezwa hapa kwetu kwa zaidi ya miezi sita bila mmiliki kujitokeza sisi tunahesabu hicho chombo hakina mwenyewe, tunalazimika kukipiga mnada kwa kufuata sheria na taratibu zote,” alisema Msangi.
Ameongeza: “Wakati mwingine chombo cha usafiri kinaweza kuhisiwa kwamba kilitumika kwenye uhalifu ama kiliibwa mahali, hapo lazima tufanye uchunguzi wa kina na tujiridhishe, lakini kama mmiliki atakuja na nyaraka zote na hakutakuwa na chembe ya shaka hapo hakutakuwa na mlolongo wowote,” anasema Msangi.
Kwanini askari wahavai sare?
Hapa jijini Mwanza malalamiko yamesikika kwa madereva bodaboda kudai askari wanaokamata hawavai sare za Polisi.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Kiongozi wa nidhamu wa umoja wa waendesha pikipiki Mwanza, Emmanuel Benjamin anasema zaidi ya pikipiki 30 zimekamatwa.
“Nimeshapokea malalamiko ya bodaboda zaidi ya 30 kuhusu kukamatwa na askari tena wasio na sare. Utaratibu huu ni mbaya na unahatarisha maisha ya madereva kwa sababu huwezi kutambua yupi ni askari na asiye askari na mbaya zaidi hawaonyeshi vitambulisho,” anasema Benjamin.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ramadhan Ng’anzi alisema wanaendesha msako wa pikipiki zenye makosa na iwapo itabainika kuwa makosa hayo yanadhaminika, wamiliki wake wataruhusiwa kufanya hivyo.
“Tunakamata pikipiki zenye makosa ya usalama barabarani na yale ambayo yanatozwa yatatozwa Sh10,000 kwa kila kosa kama Serikali ilivyoelekeza,” alisema Ng’anzi.
Alipoulizwa kuhusu askari kutovalia sare, Ng’anzi anasema hiyo ni mbinu mpya ya kukabiliana na madereva wenye tabia ya kukimbia wanapobaini uwepo wa askari wa usalama barabarani.
Operesheni ya Sirro
Agosti 2, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Siro alitangaza siku 30 za operesheni ya kuwakamata madereva wote wa bajaji na pikipiki watakaokiuka sheria za usalama barabarani.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya waendesha pikipiki Mkoa wa Dar es Salaam, Said Kagomba ameunga mkono ukamataji huo akisema madereva wengi hawafuati sheria. Anasema alivyopata taarifa kwamba kuna wenzao wanakamatwa alienda kituoni hapo na kubaini Jeshi la Polisi halikufanya uonevu wowote.
“Mimi nilivyopata taarifa ya kukamatwa kwa wenzetu nilifuatilia mpaka pale makao makuu ya trafiki na nikajionea kila kitu, kwamba kuna baadhi ya madereva wenzetu wa pikipiki wanatembea barabara ya mwendokasi ambayo hairuhusiwi, hawavai kofia ngumu, wengine hawana bima wala pikipiki zao hazina site mirror,” alisema Kagomba.
Hata hivyo, alisema alifika kituo kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam na kubainisha pikipiki zaidi ya 20 zilizokamatwa bila makosa.
Tatu Mohammed, Janeth Joseph, Florah Temba na Hamida Shariff.