Ukilima mazao haya pesa nje nje

Ukilima mazao haya pesa nje nje

Muktasari:

  • Ikiwa unataka kuwekeza kwenye kilimo na hujui ni mazao gani yatakupatia fedha haraka, basi unaweza kuanza kufikiria kilimo cha mazao ambayo bado hayajapewa kipaumbele kinachostahili nchini.

Ikiwa unataka kuwekeza kwenye kilimo na hujui ni mazao gani yatakupatia fedha haraka, basi unaweza kuanza kufikiria kilimo cha mazao ambayo bado hayajapewa kipaumbele kinachostahili nchini.

Kwa sasa Serikali imeanisha mazao ya kimkakati yakiwamo kahawa, mkonge, pamba, tumbaku, chai, karafuu na korosho, kwa kuwa ya yanaonekana kuingiza fedha nyingi za kigeni nchini, lakini yapo mengine yana soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya wakulima wanasema wanapata faida kubwa na haraka kwa kulima mazao kama vile kakao, parachichi, soya, vanilla, zabibu, michikichi na alizeti.

Mapato yatokanayo na ulimaji wa mazao hayo, yanaongezeka sababu zikitajwa kuwa ni kuongezeka kwa mahitaji kwenye masoko ya ndani na yale ya kimataifa.

Hata hivyo, ni mafanikio ya kipatoa kwenye mazao haya, hayapatikani kwa kulima kwa mkumbo. Mkulima anapaswa kukaa chini na kufuata hatua zote za kilimo bora na cha kisasa kama wanavyoelekeza wataalamu wa kilimo. Ni mazao gani hayo yanayolipa kwa sasa na sokoni hali ikoje?


Kakao

Unalifahamu zao la kakao maarufu Kiingereza kama cocoa? Hili ni maarufu kwa kutengeneza chokoleti na bidhaa nyingine. Hivi sasa wadau wanasema bei yake imeongezeka mara mbili. Miaka mitatu nyuma mkulima wa zao hilo alikuwa anauza kilo kwa Sh2000.

Lakini Agosti mwaka huu baada ya Soko la Bidhaa (TMX) kuanza kuuza kakao kwa njia ya mtandao, bei iliongezeka hadi kufikia Sh4, 964 kwa kilo.

“Hii imekuwa furaha kwa wakulima ambao walikuwa wakiacha kakao yao shambani hadi inaharibika, kwa sababu ya ukosefu wa wanunuzi au mteja akifika anatangaza bei ya chini ambayo haiwezi kurudisha gharama hivyo wakulima walikuwa wakiacha mazao yao,” anasema Mrajisi wa vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Kenneth Shemdoe.

Kwa mfano, wakati mfumo wa TMX ulipoanza kwa mara ya kwanza, wakulima hawakuwa na imani. Hivyo, walianza kwa kuuza tani 5.4 tu za zao hilo. Lakini, baada ya kuona bei inaongezeka, waliongeza na kufikia tani 30.1 kwenye minada minne mpaka Septemba mwishoni.

Kwa hapa nchini, kakao inalimwa huko Malinyi, Ifakara, Mvomero na Turiani ( Morogoro), Kyela na Tukuyu (Mbeya) Tanga na maeneo mengine nchini.


Zabibu

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Eva,s Farm Ltd), Irine Madeje, anasema bei ya zabibu za mezani ni Sh3, 000 kwa kilo. Lakini ikifungashwa vizuri kwenye maduka inauzwa hadi Sh15, 000 kwa kilo.

Madeje anasema bei ya zabibu imeimarika baada ya wakulima kuanza kulima zabibu ya mezani na kuziuza katika maduka makubwa.

‘’Kilimo hiki kina manufaa makubwa na watu wanaweza kupata pesa. Kwa bahati mbaya, wengi wanajua zabibu hutumiwa tu kutengeneza mvinyo,’’ anasema na kuongeza:

“Ni kweli zabibu hutumiwa kutengeneza mvinyo. Lakini, zinaweza pia kutumiwa kutengeneza juisi, inawekwa kwenye keki na pia huliwa kama tunda. Lakini uwezo huu mkubwa bado haujatumiwa kikamilifu.


Alizeti na mchikichi

Mwenyekiti wa Chama cha Wasindikaji wa Alizeti Tanzania (TSPA), Ringo Iringo, anasema wakati uzalishaji wa alizeti nchini umepungua kwa sababu kadhaa ikiwemo mvua kubwa (ambayo sio nzuri kwa alizeti) na ukosefu wa mbegu zilizoboreshwa.

“Tunatarajia kuongeza uzalishaji mwaka ujao kufuatia mpango mkakati wa Serikali wa kuboresha uzalishaji wa zao hilo kwa kutoa ruzuku kwa bei ya mbegu,” Iringo anasema.

Anasema bei ya zao hilo kwa kilo iliongezeka kutoka Sh500-900 mnamo 2019 hadi Sh1,600, mwaka jana.

Anabainisha kuwa Serikali imepanga kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutokana na kuwapo kwa soko kubwa katika nchi za Rwanda, Burundi, Zambia, Comoro na DR Congo.

“Pia, masoko mapya ya zao hilo yametokea Afrika Kusini na India, na tunapanga kufaidika na hilo,” anasema.

Kuhusu kilimo cha mchikichi, alisema Serikali kwa sasa inafufua zao hilo kutokana na kuwa na fursa kubwa kwenye soko, na sasa italimwa kimkakati katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Tanga na Kigoma.

Meneja Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido), Mkoa wa Kigoma Gervas Ntahamba, anasema uzalishaji wa kila mwaka wa zao la michikichi kwa sasa ni karibu tani 33,640, wakati bei ya mafuta ghafi ya mawese ni kati ya Sh20,000 -55,000 kwa lita 20 kulingana na msimu.

Vanila

Kwa upande wa vanilla, mtafiti wa kilimo cha maua Dk Daudi Mbongo anasema kuwa vanilla ina faida ikiwa watu wataelimishwa kikamilifu kuhusu ukuzaji na utunzaji wake shambani.

“Inachukua miaka miwili hadi mitatu kuvuna vanilla, na ikiwa huna ujuzi wa kutosha juu ya kilimo chake, huwezi kuikuza kwa mafanikio.”

Dk Mpoki Sichwele kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) anasema vanila ya sentimita 30 hadi 40 kama mbegu huuzwa kwa Sh4,000-5,000; lakini matunda yake yanapokuja kuvunwa mkulima kwa kilo hupata Sh500,000-Sh850,000. Anasema bei hiyo ni kwa sasa, lakini miaka mitano iliyopita kilo iliuzwa kati ya Sh150,000 hadi 300,000

Parachichi

Meneja wa Sagcot Center Ltd, Tullah Mloge, anasema takwimu kutoka kwa Wizara ya Kilimo zinaonyesha kuwa jumla ya tani 9,000 za parachichi zilizalishwa nchini Tanzania mwisho mwaka.

Anasema pia kwamba bei za parachichi ziliongezeka hadi Sh2000 kwa kilo mwaka jana, kutoka Sh1,600-1,800 mwaka uliopita. Ni zao linalohitajika sana Ulaya, Hong Kong, Afrika Kusini na Kenya.

“Soko la Ulaya hivi sasa ni dhaifu kutokana na janga la Uviko-19, lakini, mipango imewekwa ya kuingia katika masoko ya China na India na kupanua soko la Afrika Kusini, anasema.