Ukinywa dawatiba na huumwi, sasa utaripotiwa

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Jamii yatakiwa kutoa taarifa haraka kwa mamlaka pindi wanapoona watu wanatumia dawa tiba bila kuumwa au kuandikiwa na daktari.

Arusha. Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeitaka jamii kuwatilia mashaka na kutoa taarifa haraka kwa mamlaka pindi wanapoona watu wanatumia dawa tiba bila kuumwa au kuandikiwa na daktari, ili kuwanusuru na uraibu wa dawa za kulevya.

Miongoni mwa dawa tiba hizo ni pamoja na zile za kuondoa maumivu kwa haraka kama vile Morphine, Tramadol, Fentanyl, Codeine sambamba na zile za kuleta usingizi ikiwemo Valium.

Wito huo umetolewa leo Machi 26, 2024 na  Ofisa Elimu jamii wa DCEA Mkoa wa Arusha, Shaban Miraji kwenye mdahalo wa miaka mitatu ya Rais Samia.

Miraji amesema vita dhidi ya dawa za kulevya inazidi kuwa kubwa hasa baada ya vijana kuwa wabunifu na kuanza kutumia dawa tiba kwa ajili ya kulewa,  baada ya kuadimika kwa dawa zilizozoeleka hasa heroin.

 “Kuadimika kwa dawa za kulevya aina ya heroin watu siku hizi wanatumia dawa tiba kwa ajili ya kulewa, hivyo jamii watilieni shaka na muwaripoti mnapomuona mtu anatumia dawa hizi nyingi tena mara kwa mara ili kuwaokoa wapendwa wenu haraka na uraibu” alisema Miraji.

Amesema watu wanaotumia dawa tiba zenye asili ya kulevya, hulazimika kubadili dozi ya kawaida inayotolewa na daktari na kuifanya ya juu zaidi hivyo kuleta pia madhara kwa jamii kutokana na kuadimika kwa dawa hizo katika mzunguko.

 "Mfano dawa aina ya Tramadol inayotumika kutibu maumivu, dozi yake ni kati 50mg hadi 100mg ambapo mgonjwa atatumia kati ya mara mbili  hadi mara tatu  kwa siku kwa muda maalumu. Ila sasa watumiaji wa dawa hizo kwa kujifurahisha wanaweza wakatumia kati ya 500mg hadi 1000mg kwa siku na matumizi haya yanachukua muda mrefu zaidi" amesema Miraji.

Mbali na kuwa waraibu, Miraji amesema matumizi ya dozi kubwa kwa muda mrefu huweza kuleta madhara makubwa kwa watumiaji ikiwemo magonjwa ya figo, ini, kushusha kiwango cha upumuaji na hatimaye kifo.

Amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu DCEA imefanikiwa kukamata zaidi ya kilo 1.965 milioni za dawa za kulevya za mashambani na viwandani. Pia tani 376.03 na lita 1120 za kemikali bashirifu zimezuiliwa kuingia nchini.

“Mwaka 2023 pekee ndio mwaka tuliokamata madawa mengi zaidi kwa mkupuo ambayo ilikuwa ni zaidi ya tani tatu za heroin ambazo zingeweza kuathiri zaidi ya watu milioni 70 kama zingetumika hapa nchini ,” amesema Miraji

Katika  kanda ya kaskazini wamefanikiwa kukamata gunia 237 na kilo 310 za mbegu za bangi wilayani Arumeru ambazo zote kwa pamoja walifanikiwa kuziteketeza.

Kwa upande wake,  Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa amesema kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni hatari kwa afya ya vijana, ambao Serikali inawategemea katika kulisukuma gurudumu la maendeleo mbele.

Mtahengerwa amesema Serikali  imekuwa ikifanya uwekezaji mkubwa wa kuhakikisha vijana wengi wanaondoka vijiweni na kujishughulisha na shughuli za kujipatia kipato chao na hatimaye familia nzima.

“Miongoni mwa uwekezaji huo ni kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini na kuwasaidia kuwekeza kwenye kilimo, lakini pia kupanua masoko makubwa ya kimataifa sambamba na kununua ndege ya mizigo kusafirisha bidhaa hizo nje kwa biashara,”amesema Mtahengerwa.