Umasikini watajwa kuwa chanzo watoto wa mitaani

Rais wa SOS Children Village International, Dereje Wordofa akifutlrahia bidhaa zilizotengenezwa na vijana waliolelewa katika vijiji hivyo.

Muktasari:

  • Rais wa Shirika la kimataifa la SOS Village, Dereje Wordofa amesema umasikini uliokithiri na ukosefu wa maadili vimeathiri malezi ya watoto, akitaka Serikali duniani akitaka zitekeleze Malengo na matokeo endelevu (SDGs).

Dar es Salaam. Umasikini uliokithiri na ukosefu wa maadili katika jamii vimetajwa kuwa chanzo cha kukithiri kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu. 

Hayo yameelezwa leo Septemba 19 na Rais wa Shirika la kimataifa la SOS Village, Dereje Wordofa anayesimamia matawi katika nchi 138 duniani, akitokea nchini Austria. 

Amesema tangu alipofika Tanzania ameshuhudia kuwepo kwa watoto walioathiriwa na malezi na kuishauri Serikali na wadau kutekeleza wajibu wao ili kukabili tatizo hilo. 
“Kwa Tanzania kuna watoto wako mitaani, wengine wamegeuzwa kuwa watu wazima wakilea watoto wenzao. Hili ni suala muhimu linalohitaji ushirikiano, kuongezwa kwa program za watoto na kuhakikisha wanapata matunzo, wanakwenda shule ili wajifunze wawe na maisha mazuri. 
“Watoto wanapata malezi duni kutoka wa wazazi wanaoishi kwenye umasikini, wakikosa msaada katika elimu, afya, matunzo ili kuhakikisha kesho yao inakuwa bora,” amesema.  
Hata hivyo, amesema changamopto hizo hazipo Tanzania pekee bali katika nchi nyingi duniani, akizitaka Serikali duniani kutekeleza Malengo na matokeo endelevu (SDGs) ili kukabili umasikini. 
“Kumekuwa na umasikini na kumekuwa na kuvunjika kwa familia na watoto wanaathiriwa kimalezi na wengine wamathiriwa hata na maambukizi ya Uviko-19. 
“Tunahitaji kufanya juhudi za pamoja kujadili jinsi ya kuondoa umasikini uliokithiri,” amesema. 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya SOS Children’s Village Tanzania, Haruna Masebu amesema katika kukabiliana na janga la watoto wasio na makazi wamekuwa wakiwakusanya kulingana na rasilimali na kuwapa malezi kwenye vijiji vyao. 
“Mfumo wetu zamani ulikuwa ni kuchukua watoto na kuwaweka kwenye vijijiji, kunakuwa na mama anayewalea na wanasoma na wengine wamefika hadi chuo kikuu. Tumefanya tangu mwaka 1991.
“Lakini sasa tukiangalia watoto wanaohitaji malezi ni wengi na hatuwezi kuwachukua wote, hivyo tukaanzisha matunzo ya familia, tunakwenda kwenye jamii kina mama wanapoweza kusaidia kuwa na biashara kisha tunawaomba kuwa na watoto,” amsema. 
Amesema katika mfumo wa pili, watoto wanapata malezi ya uhalisia, kwani wanakaa na familia. 
“Tunao huo mfumo hapa, Arusha na Zanzibar,” amesema.