Umeme uwanja wa Mkapa waenda na watumishi saba, Tanesco wakwepa lawama

Uwanja wa Benjamini Mkapa uliopo jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Pindi Chana amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kumsimamisha kazi Kaimu meneja wa uwanja huo, Said Mtumbuka na wafanyakazi wengine sita kutokana na kukatika kwa umeme katika uwanja huo katika mechi ya kombe la shirikisho Afrika

Dar es Salaam. Kufuatia kukatika umeme uwanja wa Benjamin Mkapa jana usiku Jumapili Aprili 30, 2023 wakati wa mechi ya robo fainali ya kombe la Shirikisho Afrika, Kati ya Yanga na Rivers United kutokea Nigeria, Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo imemsimamisha kazi Kaimu meneja wa uwanja huo, Said Mtumbuka na wafanyakazi wengine sita.

Taarifa iliyotolewa jana Aprili 30 na wizara hiyo, imesema Waziri Dk Pindi Chana amemwagiza katibu Mkuu wa wizara hiyo hiyo, Said Yakubu kuwasimamisha watumishi hao wakiwamo pia aliyekuwa Mhandisi wa Umeme, Manyori Kapesa na aliyekuwa Afisa Tawala wa Uwanja huo, Tuswege Nikupala.

Aidha, rungu hilo pia limewapitia wafanyakazi wengine wa uwanja huo akiwemo, Gordon Mwangamilo, Gabriel Mwasele, Yanuaria Imboru na Dk Christina Luambano.

Taarifa hiyo pia imesema Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Said Yakubu amemteua Milinde Mahona kuwa Kaimu Meneja wa uwanja huo kuanzia Mei 1, 2023.

Pia, Katibu Mkuu atawasiliana na wadau wote kuwa mechi zote zitakazochezwa uwanjani hapo zipangiwe jioni na sio usiku katika kipindi hiki ambacho maboresho ya mfumo wa umeme na taa unaendelea.

Kwa upande wao Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupitia taarifa yake rasmi iliyotolewa na kurugenzi yao ya Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma imesema haihusiki na kukatika kwa umeme katika uwanja huo.

“Tanesco inawataarifu kuwa uwanja wa Taifa unahudumiwa na vyanzo viwili vya umeme, Tanesco na majenerata ya uwanja huo. Katika mechi ya leo (Yanga na Rivers United) uwanja ulikuwa unahudumiwa na majenereta,”.

Pia, wamesema baada ya majenereta kushindwa kufanya kazi katikati ya mchezo ndipo walitumia umeme wa Tanesco na mechi ikaendelea