Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Una dalili lakini huna ujauzito? Tatizo liko hapa

Muktasari:

Inachangiwa na mabadiliko ya mfumo wa homoni kutokana na sababu za kisaikolojia

Dar es Salaam. “Nimekuwa nikipata dalili mbalimbali za mimba, kama vile kushindwa kuona siku zangu hata kwa miezi mitatu mfululizo, kutapika hasa nyakati za asubuhi na jioni, uchovu, kukosa hamu ya kula, matiti kuongezeka na kuuma na nyinginezo, lakini kila ninapofanyiwa vipimo ninagundulika sina ujauzito.”

 Hiyo ni kauli ya Julieth Jackson, binti mwenye umri wa miaka 25 ambaye amedai kusumbuliwa na changamoto hiyo kwa takribani miezi nane sasa.

Si Julieth pekee anayepata changamoto hiyo, bali Halima Kiombezi anadai kupata hali hiyo ya kuhisi dalili za mimba, ikiwemo kukosa hedhi miezi kumi iliyopita, baada ya ujauzito wake wa kwanza kuharibika na anapofanya vipimo huonyesha hana ujauzito.

Hali hiyo wanayokutana nayo Julieth na Halima huwakuta baadhi ya wanawake na kuwasababishia kupata msongo wa mawazo.

Wataalamu wanahusisha hali hiyo na tatizo la kisaikolojia ambalo kitaalamu hujulikana kama ‘Pseudocyesis’, ‘false pregnancy’, ‘phamtom pregnancy’ au mimba ya neva ambayo husababisha mwanamke kuwa na muonekano wa dalili zote za ujauzito, wakati kiuhalisia hana ujauzito.

Mwanamke anaweza kuwa na dalili zote za ujauzito kama kuhisi kizunguzungu, kutapika mara kwa mara, shida ya kulala na hata kukosa hedhi, lakini vipimo vikaonyesha kutokuwepo kwa ujauzito.

Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, hali hiyo hutokea kutokana na mabadiliko katika mfumo wa homoni za mwili kutokana na sababu za kisaikolojia.

Tovuti ya American Pregnant Assosiation inaeleza sababu hizo ni pamoja na mwanamke kuharibikiwa na mimba mara kwa mara, kutokuwa na uwezo wa kupata mtoto kutokana na sababu mbalimbali pamoja na watoto kufariki dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Flo health, hakuna sababu maalumu ya kutokea kwa hali hiyo kwa baadhi ya wanawake, lakini imekuwa ikihusianishwa na changamoto za kisaikolojia zinazosababishwa na mwanamke kutamani sana kupata ujauzito na kuweka matumaini makubwa ya kupata ujauzito.

Tovuti hiyo pia inaeleza tatizo hilo si jipya, lilianza kuwasumbua wanawake tangu miaka ya 1940.

Pia tovuti ya healthline inaeleza hali hiyo huweza kumkumba mwanamke yeyote yule, lakini mara nyingi huwakumba wanawake kati ya umri wa miaka 33 hadi 45 na theluthi ya wanawake wanaokabiliwa na changamoto hiyo wanakuwa na historia ya kuwahi kupata ujauzito katika siku za nyuma.

Pia imeeleza kuwa tatizo hilo hujitokeza mara nyingi katika maeneo ambayo tamaduni zake zimeegemea katika thamani ya mwanamke kuhusianishwa na uwezo wake wa kushika mimba.

Akizungumzia hali hiyo, mwanasaikolojia Charles Nduku anasema ugonjwa huo haufahamiki kwa watu wengi, lakini unapompata mwanamke humfanya apate dalili zinazomfanya afikiri kuwa ni mjamzito.

Anasema dalili zinaweza kudumu kwa muda wa mrefu, jambo linaloweza kusababisha watu walio karibu naye kuamini kuwa ni mjamzito.

“Dalili zake huwa kama zile za ujauzito kama vile kukosa hedhi, uchovu uliopindukia, kutapika hasa nyakati za asubuhi na jioni, maumivu katika matiti na dalili nyingine ambazo wanawake wajawazito hupata,” anasema.

Anasema hali hiyo mara nyingi husababishwa na mwanamke kutamani kwa muda mrefu kupata ujauzito, ili mwisho wa siku apate mtoto na kushindwa kufanya hivyo.

“Akili yake mara nyingi huwaza jambo hilo, hivyo anapopatwa na mabadiliko kidogo katika mwili wake, hasa baada ya siku za hatari kupita huyahusianisha na kuwa mjamzito,” anasema mwanasaikolojia huyo.

Wengine huhusisha na imani za kishirikina. Salha Abdallah, mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam anasema aliwahi kukutwa na hali hiyo ya kuhisi dalili za ujauzito na kila alipopima aligundulika kuwa hana ujauzito.

Kwa mara ya kwanza aliihusisha na imani za kishirikina, lakini anasema baadaye alipata daktari aliyempa elimu kuwa tatizo hilo ni la kisaikolojia.

Mwanasaikolojia Charles Mhando anasema hali hiyo pia inaweza kusababishwa na changamoto nyingine katika mwili kama vile kuvurugika kwa homoni na mzunguko wa hedhi.

Hivyo anatoa wito kwa wanawake wanaopitia hali hiyo wasipuuzie wala kuhusisha na imani za kishirikina na badala yake waende katika vituo vya afya kwa ajili ya vipimo na ushauri wa kitaalamu.

Anasema vipimo ndivyo vinaweza kuthibitisha kuwa dalili hizo zimesababishwa na tatizo la Pseudocyesis au matatizo mengine ya kiafya.

Anaongeza kuwa baada ya mhusika kugundulika kuwa na Pseudocyesis, matibabu yake hutegemeana na hali ya mgonjwa, lakini mara nyingi hufanyika kwa njia ya kumpatia ushauri nasaha.

“Wepesi wa kutoweka kwa hali hiyo humuhitaji zaidi mhusika kukubaliana na hali halisi kuwa hana ujauzito,” anasema.

Pia anasema hali hiyo si tu inamuathiri mwanamke pekee, bali hata wanaume kwa kuwasababishia msongo wa mawazo pale anapopata matumaini makubwa ya kupata mtoto baada ya kuona mkewe au mpenzi wake ana dalili za ujauzito na vipimo kuonyesha hana.