Usasa unavyowahatarisha watu kuambukizwa

Muktasari:

  • Hapa nchini hili limeonekana kufanywa zaidi na mastaa wa tasnia ya burudani.

Siku za hivi karibuni imekuwa ni fahari au kawaida kwa watu wengi kuishi pamoja na mbwa au paka ndani ya nyumba zao.

Tunaweza kusema ni usasa, kwani wakati mwingine, mbwa hao wamekuwa wakibebwa na kubembelezwa mithili ya binadamu, wakati mwingine hata kulala kitandani katika viti na wengine kupewa mahitaji yote ya kibinadamu.

Hapa nchini hili limeonekana kufanywa zaidi na mstaa wa tasnia ya burudani.

Baadhi wamekuwa wakiambatana na mbwa hao kila sehemu wanayokwenda, kuwabeba mikononi na kuwabusu pale wanapoona inastahili.

Miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakionekana kuambatana na mbwa wao kila sehemu ni msanii Wema Sepetu, ambaye kuna kipindi mbwa wake maarufu kwa jina la Manunu alipotea na kutangaza dau la Sh milioni moja kwa atakayemuona.

Pia msanii Zarina Hassan, maarufu Zari amekuwa akionekana kuwa karibu na mbwa wake kiasi cha watoto wake pia kuwazoea na kuwachezea wakati wote.

Kituo cha Udhibiti wa magonjwa nchini Marekani ‘Center for Disease Control (CDC)’ kinaonyesha kuwa uwepo kwa mbwa hao katika nyumba husaidia kuwaondolea watu msongo wa mawazo, lakini pia kinatahadharisha uwezekano wa wamiliki kupata magonjwa kutoka kwa mbwa hao.

Hiyo ni kwa sababu mbwa hao wakati mwingine hubeba vijidudu au bakteria ambao husababisha maradhi. Magonjwa hayo wakati mwingine huwa madogo madogo na mengine makubwa.

Kwa mujibu wa CDC, yapo magonjwa, bakteria, minyoo, kupe na viroboti kwa ujumla wake takribani 17 anavyoweza kuambukizwa binadamu kutoka kwa mbwa.

Baadhi ya magonjwa ni kichaa cha mbwa ambacho hutokea mhusika anapong’atwa, lakini bakteria, minyoo na wadudu wengine humuathiri mtu bila kung’atwa.

Yapo magonjwa mengine ambayo binadamu huweza kuyapata kwa kumgusa au kumshika mbwa aliyeathiriwa na ugonjwa huo.

Na magonjwa mengi yaliyotajwa yanaweza kuhamia kwa binadamu, licha ya kuonekana kutokuwa na athari kubwa, lakini huwaathiri zaidi watu ambao kinga zao za mwili ziko chini.

Pia baadhi ya bakteria na minyoo wametajwa kuwa mwiba kwa watoto walio chini ya miaka mitano na watu wazima walio na zaidi ya miaka 65 na walio na magonjwa ya muda mrefu kama saratani.

Baadhi ya magonjwa hayo kwa mujibu wa CDC, hususani yale yanayosambazwa na bakteria husambazwa kwa kugusa kinyesi cha mbwa au kupiga magoti karibu na mbwa alipojisaidia.

Pia kula chakula, kunywa maji vilivyokuwa na chembechembe na kinyesi hicho huwaweka watu hatarini.

Lakini kituo hicho kinabainisha kuwa mtu atakuwa salama ikiwa atafuata taratibu za utunzaji mifugo zinazotakiwa.

Kwa mujibu wa Dk Samwel Shita, suala la umiliki wa mbwa huenda lisiwe na athari ikiwa mfugaji atazingatia maelekezo yote anayopewa na mtaalamu wa mifugo.

Anasema mbwa hupatiwa chanjo mbalimbali kwa maelekezo maalumu, ikiwemo ya kichaa cha mbwa ambacho ni hatari kwa mfugaji pia na anatakiwa kupewa cheti kuwa amechanjwa.

“Mbali na kichaa cha mbwa, wanyama hawa wanaweza kumsababishia mtu mzio kama manyoya yake yanatoka, mtu mwenye mzio akiwa karibu nao katika hali hiyo ni rahisi kupata shambulio,” anasema Dk Shita.

Lakini si mzio tu, hata watu walio na pumu hawawezi kukaa karibu na mbwa ambaye manyoya yake yananyonyoka.

Anasema pia wapo baadhi ya bakteria au minyoo ambao wakati mwingine huweza kutoka kwa mbwa kwenda kwa binadamu na kumuathiri kwa nja mbalimbali.

“Hivyo ili kuepuka haya yote, mtu anapaswa kuzingatia usafi wa mnyama mwenyewe, masharti ya kumsafisha kwa sababu wakati mwingine huwa wanashambuliwa na viroboto na papasi ambao wakimng’ata binadamu hupata homa za hapa na pale,” anasema Dk shita.

Kwa mujibu wa CDC, pia mtu huweza kuepuka maambukizi ya magonjwa mbalimbali kutoka kwa mbwa kwa kunawa mikono yake kila mara anapotoka kumshika, kulisha au kumsafisha.

Pia kumpatia mbwa huduma za afya za mifugo na kufuata maelekezo yote ya wataalamu wa mifugo.

Dk Ramadhani Senga pia anabainisha kuwa kuoshwa mara kwa mara kwa mbwa hao husaidia kuondoa viroboto na kupe wanaoweza kumsababishia binadamu homa.

“Lakini kuoshwa huku pia husaidia kuondoa manyonya yanayokatika, hii humfanya mtu mwenye mzio kuepuka kiasi kupata shambulio la mara kwa mara.

“Hii ni tofauti na mbwa wale wengine wanaofugwa kienyeji, kwani hata kuoga tu imekuwa ni mtihani kwao, hivyo wao ni rahisi kushambuliwa na magonjwa,” anasema Dk Senga