Prime
Usiyoyafahamu chumba cha malkia ndani ya jengo la KNCU
Muktasari:
- Miongoni mwa simulizi zinazovutia ni jEngo la Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa Kilimanjaro (KNCU) lenye Hoteli ya Coffee Tree (CTH)
Moshi. Mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro umebeba historia na simulizi nyingi zilizojificha nyuma ya majengo yake ya zamani.
Miongoni mwa simulizi zinazovutia ni jengo la Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa Kilimanjaro (KNCU) lenye Hoteli ya Coffee Tree (CTH).
Jengo hilo lenye ghorofa nne ni mahali ambako hadi leo bado kunatunzwa kumbukumbu ya chumba alichowahi kulala mwakilishi wa familia ya kifalme ya Uingereza miaka ya 1950.
Ndani ya jengo hilo la kipekee Afrika Mashariki, kuna kuta, vyumba, miundombinu ya umeme na samani zinazoizungumzia historia ya harakati, heshima na mafanikio ya wakulima wa kahawa wa Kilimanjaro na ukanda mzima wa kaskazini.
Jengo la Chama Kikuu cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU) lenye hoteli ndani yake, lililoanzishwa na wakulima wa kahawa mkoani humo mwaka 1956, katika Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph.
Miongoni mwa vyumba vinavyovutia wageni wengi ni kile kinachodaiwa kulaliwa na Malkia Margaret, aliyekuwa akimwakilisha Queen Elizabeth II katika sherehe za kumtawaza Mangi wa Wachaga, Thomas Marealle mwaka 1956.
Tangu siku hiyo, chumba hicho kimeendelea kuwa sehemu ya historia inayosimuliwa kizazi hadi kizazi.
Wazee wa Moshi husimulia kuwa wakati huo, ujio wa wageni wa kifalme ulikuwa tukio kubwa sana.
Maandalizi maalumu yalifanyika kuhakikisha wageni hao wanapata huduma bora zaidi na ndipo chumba hicho kikapewa hadhi ya kipekee ambayo bado ipo mpaka leo.
Lakini si wageni wa kifalme pekee walioifanya hoteli hiyo kuwa maarufu bali watu mbalimbali mashuhuri waliwahi kupumzika ndani ya vyumba vyake, jambo lililoifanya kuwa sehemu muhimu ya historia ya kijamii na kiuchumi ya Moshi.
Moja ya vitu vinavyostaajabisha ndani ya hoteli hiyo ni jokofu kubwa la zamani ambalo hadi leo bado linaonekana kuwa la kipekee.
Princess Margaret ambaye alimuwakilisha Queen Elizabeth 11 kwenye hafla ya kumtawaza Mangi Mkuu wa Wachaga, Mangi Thomas Marealle.
Jokofu hilo linaelezwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi nyama ya ng’ombe zaidi ya wawili kwa wakati mmoja kutokana na ukubwa wake.
Wengi wanaamini kuwa, huenda likawa miongoni mwa majokofu ya kwanza kabisa kuletwa nchini miaka hiyo.
Historia ya hoteli hiyo pia imefungamana na mapambano ya heshima ya wakulima wa kahawa wa Kilimanjaro.
Inaelezwa kuwa, enzi za ukoloni, baadhi ya Waingereza waliokuwa wakimiliki hoteli maarufu mjini Moshi walikuwa hawapendi kuwaona wakulima wa Kiafrika wakitumia hoteli hizo, ikiwamo hoteli maarufu ya Livingstone.
Kitendo hicho kilitafsiriwa kama dharau kubwa kwa wakulima waliokuwa wakilima na kuuza zao lililochangia uchumi mkubwa wa eneo hilo.
Ndipo viongozi wa ushirika wa kahawa wakaamua kuwa suluhisho pekee ni kujenga hoteli yao wenyewe, sehemu ambayo ingetumiwa na kila mtu kwa heshima sawa na utu pasipo na ubaguzi. Uamuzi huo haukuwa rahisi.
Lakini nguvu ya umoja wa wakulima ndiyo iliyobadili historia, inaelezwa kuwa, kila mwanachama alikubali kuchangia senti 15 kutoka kwenye mapato yake ya kahawa.
Fedha zikaanza kukusanywa mpaka kufikia Sh2 milioni, zilizokuwa ni nyingi sana kwa kipindi hicho.
Chumba namba 10 alichowahi kufikia Malkia Margaret mwaka 1956, alipomwakilisha Malkia Elizabeth II katika sherehe za kumtawaza Mangi wa Wachaga, Thomas Marealle, katika Hoteli ya Coffee Tree (CTH) iliyopo ndani ya jengo la Chama Kikuu cha Ushirika wa Kahawa Kilimanjaro (KNCU). Picha na Janeth Joseph.
Kwa fedha hizo, wakulima walijenga si tu hoteli, bali alama ya kujivunia. Jengo hilo likawa ishara ya mshikamano, uthubutu na nguvu ya ushirika wa wakulima wa Kilimanjaro.
Hadi sasa, Coffee Tree Hotel na chumba cha malkia bado vinasimama kama ushahidi wa historia hiyo.
Ni ukumbusho kwamba, wakati mwingine majengo hayaongei kwa maneno, bali kwa simulizi zilizofichwa ndani ya kuta zake.
Wazee KNCU wanena
Akisimulia historia hiyo, mmoja wazee wa chama hicho cha ushirika (KNCU), Charles Lyimo anasema jengo hilo lililojengwa kwa nguvu za wanachama wa ushirika lilileta heshima kubwa ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro.
“Hoteli hii ilikuwa ndiyo jengo refu kuliko yote ya hoteli hapa mjini, lilikuwa na lifti. Kwa wakati huo, hakukuwa na jengo jingine lililokuwa na lifti zaidi ya hili la KNCU Afrika Mashariki nzima ilikuwa hakuna,”anasema.
Moja ya majokofu yaliyokuwa yakitumika miaka ya 1950 katika Hoteli ya Coffee Tree (CTH), ambako aliwahi kufikia mtoto wa familia ya kifalme, Malkia Margaret, aliyemwakilisha Malkia Elizabeth II katika sherehe za kutawazwa kwa Mangi Mkuu wa Wachaga, Thomas Marealle, mwaka 1956. Picha na Janeth Joseph.
Lyimo anasema lifti hiyo ilikuwa ya kwanza kuwekwa katika jengo refu la hoteli kwa wakati huo na lilikuwa miongoni mwa majengo makubwa na ya kisasa zaidi Afrika Mashariki iliyokuwa na nchi za Kenya, Tanzania na Uganda.
Sababu KNCU kujenga hoteli
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Lyimo anasema wakulima wa Kilimanjaro waliwahi kubaguliwa sana na wakoloni wa Kizungu.
“Kulikuwa na hoteli maarufu mjini Moshi iliyoitwa Livingstone Hotel (baadaye ikijulikana kama Moshi Hotel), iliyokuwa maalumu kwa ajili ya wazungu pekee. Wazungu walikaa ghorofani huku Waafrika wakizuiwa hata kuingia katika maeneo hayo,”anasema.
Anasema hali hiyo iliwaumiza na kuwakasirisha sana wakulima wa Kilimanjaro.
“Kwanini sisi tusiruhusiwe kukaa ghorofani kama wao?” ndipo walipoamua kuanzisha hoteli yao wenyewe kupitia ushirika wa wakulima.
Mmoja wa wahudumu wa Hoteli ya Coffee Tree (CTH) iliyo ndani ya jengo la Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa Kilimanjaro (KNCU), mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, akijaribu kufungua mlango wa lifti katika jengo hilo. Picha na Janeth Joseph.
Lyimo anasema kila mkulima alikubali kuchangia kwa kukatwa senti 15 kutoka kwenye mauzo ya kahawa, fedha zilizotumika kujenga hoteli kubwa ya KNCU, ambayo wakati huo ilikuwa ndiyo jengo refu zaidi kuliko yote Afrika Mashariki.
"Baada ya hoteli hiyo kukamilika, wakulima waliinuka na kuonesha kuwa, nao wanaweza. Walikaa ghorofani, wakila nyama na kunywa bia huku wakiwaangalia wazungu waliokuwa chini.
“Hii ilikuwa ishara ya kujivunia utu wao na kuonesha kuwa Waafrika pia wanaweza kujenga, kumiliki na kuendesha majengo makubwa kama walivyofanya wazungu,"anasema.
Ujio wa malkia
Lyimo anasema mwaka 1956, Malkia Margaret alipofika katika hoteli hiyo, alilala chumba maalumu namba 10 kilichokuwa na huduma zote alizostahili kupewa malkia.
Anasema ndani ya hoteli hiyo kulikuwa na majokofu makubwa na ya kisasa kwa wakati huo yaliyoweza kuhifadhi nyama zaidi ya ng'ombe wawili.
Lyimo anasema majokofu hayo yalikuwa ni ya kipekee na ya kwanza kuingia nchini yakitokea Ujerumani.
"Majokofu hayo yalikuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi nyama zaidi ya ng’ombe wawili waliokuwa wamechinjwa. Kwa kipindi hicho cha Tanganyika, ilikuwa mojawapo ya jokofu za kisasa na za kipekee kabisa kuingizwa nchini," anasema Lyimo.
Mzee mwingine, Gabriel Ulomi anasema mwaka 1956 wakati malkia huyo anakuja Kilimanjaro walikuwa wamepiga hatua kubwa za kimaendeleo ikiwamo ujenzi wa hoteli aliyolala na mpaka sasa ameweka historia ndani ya Mji wa Moshi.
"KNCU ilikuwa hoteli ya kwanza kuwa na lifti katika Kanda ya Kaskazini na Afrika Mashariki kwa jumla, na pia ndiyo ilikuwa miongoni mwa hoteli za kwanza kuwa na vifaa vya kisasa mjini Moshi kipindi hicho. “Kufikia mwaka 1956, hoteli hiyo ilikuwa tayari imefunguliwa na ikawa sehemu muhimu ya mapokezi ya viongozi na wageni wa hadhi ya juu waliotembelea Mkoa wa Kilimanjaro," anasema Ulomi.
"Mwaka 1956, Malkia Margaret alilala katika Hoteli ya KNCU wakati wa ziara yake Moshi. Wakati huo, hoteli hiyo ilikuwa miongoni mwa hoteli bora zaidi katika eneo lote la Kaskazini mwa Tanzania. Uwepo wake uliendelea kuonesha hadhi ya KNCU kama taasisi kubwa inayomilikiwa na wakulima wa Mkoa wa Kilimanjaro na mchango wake mkubwa katika uchumi wa kahawa."
Kupitia ubora wa kahawa yake, KNCU ilijijengea sifa kubwa duniani kama chama kinachozalisha na kusimamia kahawa bora. Umaarufu huo uliifanya Kilimanjaro na Tanzania kwa jumla kutambulika kimataifa kupitia biashara ya kahawa iliyokuwa chini ya usimamizi wa ushirika wa wakulima.