Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti kubaini viashiria saratani ya matiti kwa wanaume waanza

Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa yasiyoambukiza  kilichopo katika hospitali ya KCMC, Profesa Blandina Mmbaga akizungumza na wataalamu mbalimbali wa magonjwa ya saratani (hawapo pichani) wakati wa kongamano la ufunguzi wa programu ya Nora and React-Can inayohusisha tafiti mbalimbali za saratani nchini. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Lengo la utafiti huo ni kutoa mwongozo kwa ajili ya kinga dhidi ya saratani hiyo,  pamoja na kuimarisha sera za saratani zilizopo nchini, na kubadili mifumo ya sera hizo endapo itahitajika kufanyika.

Moshi. Kituo cha Utafiti wa Magonjwa Yasiyoambukiza (KCRI) cha Hospitali ya KCMC, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, kimeanza kufanya utafiti wa kisayansi wa kubaini viashiria vya saratani ya matiti kwa wanaume.

Lengo la utafiti huo ni kutoa mwongozo kwa ajili ya kinga dhidi ya saratani hiyo,  pamoja na kuimarisha sera za saratani zilizopo nchini, na kubadili mifumo ya sera hizo endapo itahitajika kufanyika.

Akizungumza leo Jumatatu Julai 29, 2024 katika kongamano la ufunguzi wa programu ya Nora and React-Can, ambayo inalenga kuwanoa watafiti wa sayansi ya saratani nchini, mkurugenzi wa kitengo hicho, Profesa Blandina Mmbaga amesema utafiti uliofanywa kwa miezi mitatu na wataalam wa kituo hicho umebaini wanaume 29 wamefika hospitalini kupata matibabu ya ugonjwa huo.

"Saratani ya matiti sio kwa wanawake tu, hata wanaume pia. Kwa kipindi hiki ambacho tumekuwa tukifanya utafiti hapa kwetu, tumeweza kubaini tunao wanaume wengi wana viashiria vya saratani ya matiti," amesema Profesa Mmbaga.

Amesema ndani ya miezi mitatu, utafiti walioufanya umebaini wanaume 29 walikuwa wanaenda kwenye matibabu ya dawa.

"Tunajua saratani inaweza kusababishwa na mabadiliko ya homoni, lakini sasa hivi hatuwezi kuliweka hilo wazi, tunataka kulifanyia kazi zaidi, hivyo hatuwezi kusema zaidi mpaka hapo baadaye tutakapoweza kujua viashiria ni nini," amesema Profesa Mmbaga.

Akizungumzia tatizo la saratani nchini, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani na Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Saratani Tanzania, Jerry Ndumbalo amesema takwimu zinaonesha wanaume 99 wana ugonjwa wa saratani hiyo ya matiti na jitihada za kupambana na ugonjwa huo zinahitajika.

"Sasa hivi tunaona idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani inaongezeka sana Tanzania. Kwa mwaka jana, takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) zimeonesha tuna wagonjwa zaidi ya 44,000 na vifo takriban 28,000," amesema Dk Ndumbalo.

Naye Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Kikristo cha Tiba, Kilimanjaro (KCMUCo), Profesa Ephata Kaaya, amesema chuo hicho kitaendelea kuweka mazingira rafiki kwa watafiti bingwa wa magonjwa hayo ya saratani.

"Kwa wale ambao wanaendelea na tafiti za saratani katika chuo na hospitali yetu ya KCMC na taasisi nyingine za Msamaria Mwema, ni kwamba chuo kimejizatiti kuweka mazingira mazuri katika utafiti na sisi kama chuo tumedhamiria kuwaunga mkono katika safari yenu ya kuwa na watafiti bingwa wa magonjwa ya saratani," amesema Profesa Kaaya.