Utafiti waanika chanzo rushwa ya ngono vyuo vikuu

Saturday November 28 2020
utafitipic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Mmomonyoko wa maadili na matumizi mabaya ya madaraka, vimetajwa kuwa vyanzo vya kuwapo kwa rushwa kubwa ya ngono katika vyuo vikuu viwili nchini- Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Hayo yamebainika kufuatia utafiti uliofanywa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika kipindi cha Januari na Februari mwaka huu.

Akielezea kwa kina matokeo ya utafiti huo, mwendesha mashitaka wa Takukuru, Denis Lakayo alisema kuwa utafiti huo ulihusisha wahojiwa 589, ambapo 352 walitoka UDSM na 237 kutoka Udom.

Alisema utafiti huo ulibaini zaidi ya asilimia 50 ya wahojiwa walieleza kuwapo kwa rushwa ya ngono katika vyuo vikuu hivyo.

“Katika waliohojiwa ambao walionyesha uelewa wa rushwa ya ngono kwa kuitofautisha na nyingine, walisema madaraka yalitumiwa vibaya na wahusika kama nyenzo ya kusukuma wapate wanachokitaka”alisema Lekayo na kuongeza.

“Huku mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi pia ukitajwa kuwa sababu ya kuendelea kuwapo kwa vitendo hivyo”alisema.

Advertisement

Alitolea mfano kilichotolewa ushuhuda na mhadhiri mmoja ambaye alimwita mzazi wa mwanafunzi kujadiliana naye kuhusu mavazi na mwenendo wa kijana wake.

“Alipokuja mzazi ilibidi mhadhiri amsalimie tu badala ya kumweleza alichomuitia kutokana na namna alivyovaa, yeye alikuwa zaidi ya kijana wake”alisema.

Lekayo alisema baadhi ya maeneo walibaini yameoza kabisa, kwani yule aliyepaswa kumsaidia mwanafunzi anayedaiwa rushwa ya ngono, naye hakuwa na msaada.

“Kuna shuhuda moja tuliipata, mwanafunzi alidaiwa rushwa ya ngono na mhadhiri, akaenda kushitaki kwa mhadhiri wa kike, alichojibiwa ni kuwa mpe ni dakika tano unapata shahada yako”alisema.


Sababu nyingine

Alisema matokeo ya utafiti huo yalibainisha sababu nyingine ni mfumo wa utoaji taarifa kutokuwa rafiki, mifumo dhaifu ya kushughulikia rushwa ya ngono na mamlaka ya kutoa alama za mitihani kuachiwa wahadhiri pekee.

Alisema matokeo hayo yanashatiliwa nguvu na baadhi ya shuhuda ambazo wahojiwa walieleza kuwa ni visababishi vya rushwa ya ngono katika vyuo vikuu vilivyofikiwa na utafiti huo.

“Kwa mfano, katika eneo la kutahini, madaraka makubwa wamepewa wahadhiri huku baadhi yao wakiwa hawana mafunzo ya maadili ua ufundishaji hivyo ile dhana ya mwalimu ni kama mzazi haipo ”alisema.

Alisema walielezwa kuwa ili wahadhiri wawapate wanafunzi kingono hawatumii fedha, bali wanatumia nafasi zao za uhadhiri.

Alisema waliohojiwa pia walieleza namna ambavyo mfumo bado siyo mzuri, kwa sababu wanafunzi wengi wanaoripoti matukio hayo wamekuwa wakiishia kufukuzwa chuo.

Alisema pia walielezwa kuna wahadhiri huwataka kingono watumishi wanaofanya usafi katika ofisi zao na wanapokataliwa huwatoa katika nafasi hizo.

“Shuhuda nyingine zilieleza kuwa wahadhiri waliokubaliwa kupewa rushwa ya ngono walikuwa wakifika ofisini saa 11 alfajiri kwa lengo la kupokea rushwa hiyo”alisema.

Alisema hata hivyo wakati wa ufuatiliaji ilibainika kuwapo baadhi ya wahadhiri wanaozingatia maadili ya kazi zao.

Alieleza kuna baadhi ya waliohojiwa walitoa shuhuda kuwa kuna mwanafunzi alimwandikia mhadhiri barua pepe akimuomba amsaidie katika somo lake na atamlipa kitu chochote lakini siyo pesa.

Pia kuna mwanafunzi alikiri kosa la kumfanyia jaribio mwenzake, yule aliyefanyiwa jaribio alipobaini ni kosa linaloweza kumfukuzisha chuo, alimshawishi mhadhiri kingono.

“Mhadhiri alichofanya ni kumkabidhi mwanafunzi huyo kwa mkuu wa idara kwa ajili ya hatua zaidi”alisema Lekayo.

Alisema utafiti ulibaini udhaifu katika mifumo ya udhibiti wa rushwa ya ngono, huku asilimia 10.7 hadi 38.2 walikubali kuwapo kwa sera, miongozo na taratibu za udhibiti wa rushwa ya ngono. Hata hivyo, zaidi ya asilimia 60 waliohojiwa hawakufahamu uwepo wa mambo hayo.

Awali akizungumza katika hafla ya uwasilishaji wa utafiti huo Mwenyekiti wa TGNP, Aseny Muro, alisema rushwa ya ngono inakwamisha na kufuta ndoto za vijana wengi.

Alisema kuwa wapo wengi walioumia na pengine kufa kutokana na rushwa ya ngono.

“Wapo waliokatishwa tamaa, kutishwa na hata kupoteza maisha, kuna waliojitoa kuhakikisha wanapambana na janga hilo ili kulikomesha.

“Likipungua kama siyo kuisha kabisa, itakuwa fursa nyingine ya kupata wasomi bora na waliohitimu kwa vigezo na wasiotumia miili yao na wahadhiri waadilifu wataepukana na dhima hii”alisema Muro.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa WFT, Mary Rusimbi alisema kuwa ili kumaliza tatizo la ngono vyuo vikuu kila mmoja apinge popote pale alipo.

Alisema kupinga ukatili wa kingono kunaanza na kila mmoja na hakuhitaji kusubiri litokee katika familia ya muhusika, bali anapaswa kupambana kwa ajili ya wengine.

“Hili suala ni kubwa na lipo kwa miaka mingi, ili kuliondoa linahitaji nguvu ya pamoja”alisema.


Advertisement