Utafiti wabaini mikopo, madeni chanzo msongo wa mawazo kazini
Mkurugenzi wa Body Mind Insights John Ambrose (Kulia) na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Ukusanyaji Mapato Tanzania (Tarewu), Dk Michael Marere (Kushoto) wakisaini mkataba wa makubaliano katika kuimarisha afya ya akili.
Muktasari:
- Utafiti wa Body Mind Insight umebaini mikopo na madeni kuwa chanzo kikuu cha msongo wa mawazo kwa wafanyakazi. Takribani asilimia 70 ya wenye madeni wanakabiliwa na changamoto za afya ya akili, hali iliyosababisha Tarewu kuanzisha programu za ustawi na ushauri nasaha.
Dar es Salaam. Changamoto ya mikopo na madeni imeibuka kuwa moja ya vichocheo vikubwa vya msongo wa mawazo na matatizo ya afya ya akili miongoni mwa wafanyakazi, utafiti mpya umebaini.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyowasilishwa na kituo cha Body Mind Insight, karibu asilimia 99 ya wafanyakazi waliohusika kwenye utafiti huo wanabeba mizigo ya madeni au mikopo, hali inayowaweka kwenye presha ya kifedha ya muda mrefu na kuathiri utendaji wao kazini pamoja na afya zao za akili.
Utafiti huo unaonyesha kuwa kati ya watu hao wenye madeni, zaidi ya asilimia 70 tayari wameanza kuonyesha dalili za msongo mkubwa wa mawazo, ikiwemo wasiwasi wa mara kwa mara, uchovu wa kiakili na kushuka kwa ari ya kazi.
Hayo yamesemwa leo Juni 12, 2026 na Mkurugenzi wa Body Mind Insight, John Ambrose, wakati wa kusaini mkataba wa makubaliano na Chama cha Wafanyakazi wa Ukusanyaji Mapato Tanzania (Tarewu) katika kuimarisha afya ya akili, ustawi wa kisaikolojia na maendeleo ya wanachama wake.
Amesema mzigo wa mikopo unachangia moja kwa moja ongezeko la uchovu wa siri (silent burnout), hali ambayo mtu huonekana anaendelea na kazi kawaida lakini kiakili anakuwa amechoka kupita kiasi.
“Watu wengi wanaishi chini ya shinikizo la mikopo kila siku, wanakwenda kazini wakiwa na mawazo mengi kichwani, hali inayowafanya washindwe kuzingatia kazi na hata kuathiri maisha yao ya nyumbani,” amesema Ambrose.
Amesema utafiti huo pia umebaini hali hiyo imechangia baadhi ya wafanyakazi kuanza kuomba likizo bila malipo ili kupata muda wa kupumzika na kujitunza kiakili.
Kwa mujibu wa Ambrose, takribani asilimia 60 ya wafanyakazi katika taasisi zilizofanyiwa utafiti wameshaomba au wanapanga kuomba likizo za muda mrefu kutokana na msongo wa kazi na changamoto za kifedha.
Wataalamu wa afya ya akili wanaonya kuwa endapo hali hiyo haitadhibitiwa, inaweza kuathiri uzalishaji kazini na kuongeza gharama za afya kwa taasisi na jamii kwa ujumla.
“Baada ya kubaini hali hiyo, taasisi na waajiri wanatakiwa kuweka mikakati ya kusaidia wafanyakazi kukabiliana na msongo wa kifedha na wa kazi, ikiwemo elimu ya afya ya akili na mifumo bora ya usimamizi wa kazi,” amesema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Ukusanyaji Mapato Tanzania, Dk Michael Marere, amesema chama hicho kimejipanga kuimarisha ustawi wa wanachama wake kupitia utekelezaji wa mpango mkakati wake wa pili unaolenga kuboresha afya ya akili, ustahimilivu wa kiakili na mazingira ya kazi.
Dk Marere amesema mpango huo wa pili, ambao utekelezaji wake umeanza mwaka 2026 na unatarajiwa kuendelea hadi 2030, unamweka mwanachama wa chama hicho kama mhimili mkuu wa maendeleo yake.
Amesema chama kimebaini changamoto za afya ya akili, msongo wa mawazo na ustahimilivu mdogo wa kiakili zimeanza kuathiri utendaji kazi katika sekta ya ukusanyaji mapato, hali iliyosababisha uongozi kuchukua hatua za makusudi za kuanzisha programu maalum za ustawi.
“Tumekuwa tukiangalia kwa upana wake na kuona kwamba ili kumwezesha mwanachama wetu kufanya kazi kwa ufanisi, lazima tumpe huduma za afya ya akili, usimamizi wa msongo wa mawazo, pamoja na kujenga mental resilience,” amesema Dk Marere.
Dk Marere amesema afya ya akili sasa ni suala mtambuka linaloathiri hata utekelezaji wa majukumu ya msingi ya sekta ya ukusanyaji mapato.
“Tunawahitaji wanachama wetu wawe na afya bora ya mwili na akili kwa pamoja ili kuongeza tija kazini,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimetangaza kuanzishwa kwa programu maalum iitwayo Mental Health Bootcamp, ambayo itakuwa ikiwafikia wanachama wake nchi nzima, wakiwemo walioko mikoani.
Kupitia programu hiyo, wanachama watapatiwa huduma za kliniki za afya ya akili, ushauri nasaha, pamoja na mafunzo ya jinsi ya kukabiliana na msongo wa mawazo na kuboresha ustahimilivu wa kiakili.
“Bootcamp hii itajikita katika afya ya akili, usimamizi wa msongo wa mawazo na ushauri wa kitaalamu kuhusu afya kwa ujumla,” amesema.
Pia, Dk Marere amesema ushirikiano uliopo utaimarisha ustawi wa wafanyakazi na kuongeza ufanisi kazini, si tu Dar es Salaam bali pia katika mikoa yote nchini, na mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa chama wa kuhakikisha mwanachama anakuwa msingi wa maendeleo, ustawi na uzalishaji.
“Tunaamini kupitia ushirikiano huu tutafikia wanachama wetu wote na kuboresha maisha yao ya kazi na binafsi,” amesema.