Utajiri wa gesi wanoga TZ

Muktasari:

Matumizi ya gesi ya heliumu

  • Heliamu hutumika kwenye unajimu kupooza vifaa vya satellite, kusafisha injini za roketi na kupooza hewa ya oksijeni na haidrojeni inapokuwa katika hali ya kutiririka ambazo hutumika kurushia ndege za Apollo.
  • Heliumu hutumika kupooza Large Hadron Collider (LHC) na kwenye mashine za kuchukulia vipimo kwa njia ya sumaku ya MRI Scanner.
  • Heliumu pia hutumika kujaza maputo ya sherehe, ya hali ya hewa na ndege kutokana na wepesi wake.
  • Mchanganyiko wa asilimia 80 ya heliumu na asilimia 20 ya oksijeni hutumiwa na wapiga mbizi na wengine wanaofanya kazi kwenye hewa nzito.
  • Gesi ya helium-neon hutumika kubaini alama kwenye maduka makubwa (barcodes).

Dar es Salaam. Wakati ikiwa imeanza kutumia sehemu ndogo ya gesi asilia inayochimbwa nchini, watafiti kutoka Uingereza wamegundua hifadhi kubwa zaidi duniani ya gesi adimu ya heliumu nchini Tanzania.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Oxford na cha Durham kwa kushirikiana na wataalamu wa madini kutoka Norway wamegundua uwepo wa takriban futi bilioni 54 za ujazo za gesi hiyo ya barafu kama inavyofahamika.

Wakati jitihada za kutafuta mafuta zikiendelea, tayari gesi asilia iliyopatikana nchini ni jumla ya mita za ujazo trilioni 55 baada ya ugunduzi katika maeneo tofauti ya nchi.

Gesi ya heliumu ambayo ni adimu, hutumiwa kwenye vifaa vya kitabibu kama mashine ya kuchukulia vipimo ya MRI Scanner, kubashiri moto viwandani, kuunganishia vyuma na nishati ya nyuklia.

Ugunduzi huo umefanyika katika eneo la bonde la ufa la nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), watafiti hao waliwaambia waandishi wa habari jijini Tokyo, Japan kuwa uhaba wa gesi hiyo kote duniani ulikuwa umesababisha taharuki haswa kwa madaktari ambao wanatumia gesi hiyo adimu kuendesha mashine za MRI scanner.

Kabla ugunduzi huo watafiti walikuwa wamebashiri ukosefu wa gesi hiyo baridi ifikapo mwaka wa 2035.

Mnamo mwaka 2010, mwanafizikia aliyeshinda tuzo ya Nobel, Robert Richardson alikuwa ametabiri kumalizika kabisa kwa gesi hiyo.

Ukosefu huo ulikuwa umesababisha wataalamu kuhimiza kutungwa kwa sheria itakayopunguza matumizi yake katika bidhaa zisizo za dharura kama vile kwenye vibofu kutokana na hali ya kuwa gesi hiyo ya heliumu kuwa ni nyepesi kuliko ile ya oksijeni.

‘“Gesi tuliyoipata huko Tanzania inaweza kujaza silinda za gesi 1.4 milioni za mashine za MRI,’’ alisema Chris Ballentine kutoka Chuo Kikuu cha Oxford.

Tovuti ya Indiatoday.com imeripoti kuwa hadi sasa gesi hiyo haijawahi kugunduliwa kwa mkakati maalumu zaidi ya kugundulika kwa bahati wakati wa kutafuta mafuta na gesi nyingine asilia.

Lakini wataalamu hao wa Oxford na Durham wakiwa pamoja na kampuni ya utafutaji gesi hiyo ya Norway inayoitwa Helium One, wamegundua njia mpya ambayo imegundua gesi hiyo katika msako wa kwanza.

Watafiti hao wanasema kadri volcano inavyokuwa inatembea, hutoa joto kubwa ambalo huruhusu gesi hiyo kutoka kwenye miamba ya kale

“Tumeonyesha kwamba volcano kwenye Bonde la Ufa ina jukumu muhimu sana katika kutoa gesi iliyokusanywa kwenye miamba ya kale,” alisema Diveena Danabalan, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu wa Durham akikaririwa na tovuti hiyo.

Katikati ya mwezi huu, Profesa Muhongo alilidokezea Bunge kuwa utafiti unaoendelea umebaini kuwepo kwa gesi hiyo na kwamba kiwango kilichobainika ni mita za ujazo bilioni 52.2.

Alisema utafiti zaidi unaendelea.