Utekelezaji wa Dira 2050 kupimwa kwa KPIs
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wkati akiwasilisha taarifa ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma leo Alhamis Juni 11, 2026. Picha na Said Khamis
Muktasari:
- Utekelezaji wa Dira 2050 unatarajiwa kuanza Julai Mosi, 2026, hivyo kukamilika kwa Dira 2025 Juni 20, 2026 itakuwa ndiyo mwanzo wa safari ya maendeleo kupitia Dira 2050, inayolenga kufikia uchumi wa Dola za Marekani 1 trilioni kufikia mwaka 2050.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imebainisha mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 (Dira 2050) yatapimwa kwa kuzingatia viashiria vya matokeo (KPIs) kwa kila sekta na tayari imeandaa nyenzo kufikia mafanikio hayo.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi, Juni 11, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/27.
Utekelezaji wa Dira 2050 unatarajiwa kuanza Julai Mosi, 2026, hivyo kukamilika kwa Dira 2025 Juni 20, 2026 itakuwa ndiyo mwanzo wa safari ya maendeleo kupitia Dira 2050, inayolenga kufikia uchumi wa Dola za Marekani 1 trilioni kufikia mwaka 2050.
Profesa Kitila amesema Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026 ni nyenzo ya kwanza katika kuanza utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/27 – 2030/31 na Dira 2050. Amesema Serikali imekamilisha nyenzo zote muhimu za utekelezaji wa Dira 2050.
“Mafanikio ya utekelezaji wa Dira 2050 na mikakati yake yatapimwa kwa kuzingatia viashiria vya matokeo (Key Performance Indicators – KPIs) kwa kila sekta na siyo wingi wa shughuli au michakato ya utekelezaji.
“Katika kufikia azma hii, Sekretarieti ya Tume itajielekeza na kujikita katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo (Delivery Bureau)” amesema profesa Kitila wakati akiwasilisha taarifa hiyo.
Amezitaja nyenzo hizo ni Mpango Elekezi wa Muda Mrefu (2026/27 – 2050/51); Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/27 – 2030/31); Mwongozo wa Kitaifa wa Uandaaji Mipango; na Mwongozo wa Kitaifa wa Uidhinishaji wa Miradi ya Maendeleo.
Nyenzo nyingine ni Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo na Mkakati wa Mawasiliano wa Dira 2050 wa Miaka Mitano 2026/27 – 2030/31.
“Kufuatia kukamilika kwa nyenzo hizo za utekelezaji wa Dira 2050, kazi iliyo mbele yetu sasa ni moja tu: kutekeleza,” amesema.