Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utitiri wa michango unavyokimbiza wanafunzi shule za umma

Dar es Salaam. Wadau wa elimu wamependekeza kuongezwa kwa ruzuku kwenye elimu kwa kile wanachodai fedha inayotolewa na Serikali haikidhi mahitaji ya shule.

Mwananchi limebaini jambo hilo linaathiri shule za umma, hivyo kusababisha viongozi wa shule na kamati kulazimika kuwahusisha wazazi na walezi kusaidia baadhi ya mahitaji ya shule kwa kutoa michango, ambayo Mwananchi limebaini baadhi imekuwa sababu ya wazazi kukacha kupeleka watoto kuandikishwa.

Ufuatiliaji katika baadhi ya maeneo nchini umebaini bado idadi kubwa ya wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu hawajaripoti shule ikiwa tayari zimepita zaidi ya siku kumi tangu kuanza kwa mwaka mpya wa masomo Januari 8, 2024.

Mfano hadi Januari 18, 2024 zaidi ya robo ya wanafunzi hawakuripoti shuleni wilayani Kondoa.

Ofisa uhusiano wa Halmashauri ya mji wa Kondoa, Sekela Mwaisubila akusena wanafunzi 593 kati ya 1,782 wa kidato cha kwanza waliopangiwa katika halmashauri ya mji wa Kondoa hawajaripoti shuleni hadi kufikia jana.

Huko Songwe asilimia 57 ya wanafunzi waliopaswa kuanza kidato cha kwanza katika Kata ya Chitete iliyopo Wilaya ya Momba mkoani Songwe hawajaripoti shule.

Kutokana na changamoto hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda ametoa siku saba kwa uongozi wa Wilaya ya Momba kufanya msako wa nyumba kwa nyumba katika Kata ya Naming’ong’o na Chitete na kuwachukulia hatua wazazi au walezi ambao watoto wao hawajaripoti shule.

Kwa mujibu wa wazazi na walezi gharama za mahitaji, huweza kufika hadi Sh400,000 kulingana na mahitaji ya shule.

“Ni marufuku kwa shule yoyote kuweka michango ya lazima ambayo mzazi au mtoto asipotoa mchango huo mtoto atakatazwa kwenda shuleni,” Nukuu ya Profesa Adolf Mkenda.

Katika shule mbili za kutwa jijini Dodoma, fomu ya kujiunga na shule, zilionyesha kwa mtoto wa kike anatakiwa kuwa na sketi ndefu na shati, fagio za ndani na nje, jembe, reki, ndoo ndogo ya lita 10, rimu moja ya karatasi nyeupe, madaftari makubwa.

Pia, mwanafunzi anatakiwa kitambulisho cha shule ambacho gharama yake ni Sh5,000 na kufanyiwa uchunguzi wa afya ambapo gharama za uchunguzi zinafikia hadi Sh65,000.

Katika shule nyingine ya kutwa iliyoko Mkoa wa Tabora, wanafunzi wa kiume wanatakiwa wawe na jembe, fagio na ndoo.

Vifaa vingine ni daftari kubwa (counter book) 11, kilo 4.5 za mchele kwa kila mtoto, maharage kilo mbili Sh2000 kwa ajili ya kumlipa mpishi na kununua chumvi pamoja Sh2,000 malipo ya mwalimu wa sayansi na Sh100 kila mwezi kwa ajili ya kulipa mlinzi.

Kwa shule za msingi nyingi zina utaratibu wa madarasa ya mitihani (darasa la nne na la saba) kuanzisha kambi ya masomo au kwa wale wa shule za kutwa hulazimika kubaki shuleni.

Kufidia haya shule zinalazimika kuweka michango kwa wazazi ili watoto wapate chakula mchana au wanapokuwa kambini.

“Kwenye kikao cha wazazi na kamati ya shule, tulikubaliana kuchangia mahitaji ya watoto ili waanze kula chakula mchana shuleni,” alisema Zuhura Shabani mzazi mwa mwanafunzi wa darasa la saba katika moja ya shule wilayani Kondoa, Dodoma.

Mzazi huyo alisema wamekubaliana kupeleka mahitaji yatayotosheleza kwa miezi mitatu na gharama zake zinafika hadi Sh100,000.

Mkazi wa Dodoma Makulu, Mariam Mhoga alisema mtoto wake alikataliwa kupokelewa shuleni hadi hapo atakapokamilisha mahitaji yote yaliyopo katika fomu ya kujiunga na shule.

Alisema hali hiyo imemlazimu mtoto kuchelewa kuripoti shuleni ili kukamilisha mahitaji yote ikiwemo kujaza fomu ya uchunguzi wa afya yake.

Mzazi mwingine, Beatrice Zefania ambaye ana mtoto Shule ya Sekondari ya Sechelela – Dodoma alisema gharama ni kubwa ambazo zinamlazimu kutumia Sh270,000 ili kukamilisha vitu vyote vinavyohitajika.

Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mwaifunga alihoji ada ilikuwa ni Sh20,000 lakini ukiangalia vifaa vya kununua vinazidi Sh300,000 na kwamba vitu hivyo hukatisha tamaa Watanzania.

“Sisi ni wabunge na katika mikoa yetu kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu joining instruction (maelezo ya kujiunga na shule), zinakuja na mahitaji ya gharama kubwa,” alisema.


Walichokisema walimu, wadau

Walimu, wadau wa elimu wamesema, umefika wakati wa Serikali kufanya mapitio ya ruzuku zinazotolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuendana na gharama za sasa za maisha.

Hili linakuja baada ya kutokuwepo kwa mabadiliko ya kiwango cha ruzuku kwa mwanafunzi tangu ilipoanzishwa zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Licha ya kuwa utekelezaji wa kiwango cha juu ulionekana tangu 2016, fedha hiyo haikubadilika hivyo kuwaibua wadai wanaosema zinashindwa kununua baadhi ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia huku shule zikiwa hazina uwezo wa kuchangisha wazazi.

Mwalimu wa taaluma kutoka moja ya shule mkoani Morogoro alisema michango, inasaidia kutatua changamoto zinazoikumba shule, huku ikilenga kuboresha kile kinachotolewa na Serikali kama ruzuku.

Paresso aibua hoja ya elimu bure bungeni

“Wahitimu kidato cha nne walikuwa 90 pekee, wanaoingia kidato cha kwanza ni 340. Kunakuwa na uhaba wa madarasa na madawati wakati fedha ya ruzuku inabaki ile ile” alisema.

Alisema baadhi ya shule kulingana na jiografia ya eneo husika zimekuwa zikikabiliwa na uhaba wa walimu, jambo ambalo hufanya wazazi kukubaliana kuchangishana fedha kwa ajili ya kumuajiri mwalimu.

Alisema hata utekelezaji wa mchango husika unapoanza huku akitolea mfano wa chakula, huwa unasimamiwa na kamati yenyewe na walimu wa shule hukaa pembeni.

Akikazia suala hilo, mwalimu mkuu wa shule nyingine alisema michango hiyo inaboresha baadhi ya vitu ikiwemo kuongeza vifaa.

“…mara nyingi haichukuliwi fedha bali kitu husika, tukisema mtoto aje na karatasi ni kwa ajili ya maendeleo yake ya kujipima kila wakati,” alisema.


Kauli ya Serikali

Akizungumzia suala la uongezaji ruzuku, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa alisema, wakuu wa mikoa wameagizwa kufanya mapitio ya bajeti zao ili shule ambazo zina changamoto kama suala la chakula, serikali ya mkoa wagharamie yenyewe.

“Tunataka kila mtu awajibike katika eneo lake, mipango ya maendeleo ianzie kwao wajadili wapitishe na kuona uhitaji wao ni shilingi ngapi, katika bajeti zao waone wanahamisha wapi kwa sababu sisi kama Tamisemi hatuwezi kujua nchi nzima kuna uhitaji gani, kupitia wao ndiyo tutajua wilaya hii na hii kuna shida hii na kujua nini cha kufanya,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa, alisisitiza wanafunzi hawaruhusiwi kuzuiliwa kisa michango na endapo suala hilo litafika mezani kwake, litamweka katika kaa la moto mwalimu mkuu. .na Ofisa elimu wa eneo husika.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema ni marufuku kwa shule kuweka michango ya lazima inayowanyima watoto fursa ya kuhudhuria masomo.